Zahoro Pazi (kulia) alipokuwa na kikosi cha Azam kabla ya kupelekwa kwa mkopo JKT Ruvu |
MSHAMBULIAJI wa Azam FC anayecheza kwa mkopo katika klabu ya JKT Ruvu, Zahoro Pazi anatarajiwa kuondoka nchini kwenda Afrika Kusini kwa mara ya pili kujiunga na klabu ya Bloemfotein Celtic ya nchini humo.
Celtic inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo (PSL), ilimuita na kumfanyia majaribio mchezaji huyo mapema mwaka huu na kuelezwa kuwa alifaulu lakini kwa kuwa nafasi ilikuwa ni ya mchezaji mmoja tu, alichukuliwa Mzimbabwe Roderick Mutuma.
Hata hivyo, mara aliporejea nchini Pazi alisema aliahidiwa na klabu hiyo kuitwa tena mara baada ya msimu huu kumalizika ili kuendelea kujifua na timu hiyo kwa ajili msimu ujao na kwamba safari hiyo ingefanyika mwezi Mei.
Akizungumza na MICHARAZO jana, Pazi alisema mapema wiki hii alipigiwa simu na kocha wa klabu hiyo, Clinton Larsen, na kumfahamisha kuwa ajiandae kwenda nchini humo mwezi Juni wakati mazoezi ya kusaka wachezaji wa msimu ujao utakapoanza.
"Ile safari yangu haitakuwa tena Mei, nimepigiwa simu na kocha wa Celtic na kunieleza kwamba mazoezi yao kwa ajili ya kujiandaa msimu mpya yataanza mwezi Juni, hivyo natakiwa niende wakati huo," alisema Pazi.
Alisema kusogezwa mbele kwa safari yake kumekuwa ni nafuu kwake akiamini kutamfanya ajifue zaidi ili atakapoenda awe katika kiwango kile kile kilichoivutia klabu hiyo iliyomuona kwenye michuano ya Kombe la Kagame na Kombe la Hisani nchini DR Congo.
"Ligi yao kama yetu itaisha mwezi ujao, na kwa vile safari itakuwa Juni naamini nitatumia muda uliosalia kujifua zaidi ili niendapo huko niwe katika kiwango kile kile na kufanya niweze kujiunga nao, naamini Mungu ataniwezesha kutimiza ndoto zangu kucheza soka la kulipwa," alisema Pazi.
Mchezaji mwingine wa Azam, Abdulhalim Humud 'Gaucho' naye amefaulu majaribio yake katika klabu ya Jomo Cosmos na atajiunga nao Julai mwaka huu kwa ajili ya msimu mpya.
No comments:
Post a Comment