Shomar Kapombe akiwa na tuzo ya Mwanasoka Bora aliyotwaa mwaka jana |
BEKI tegemeo wa Simba na timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), Shomary Kapombe, anatarajia kuondoka nchini mwezi ujao kwenda Uholanzi kwa ajili ya kufanya majaribio na timu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu ya nchini huko na Ligi Daraja la Kwanza.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema kuwa amepokea barua kutoka kwa wakala anayetambuliwa na Chama cha Soka cha Uholanzi na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) aitwaye, Dionis Kadito, akisema kwamba Kapombe atagharamiwa kila kitu akiwa huko kwa muda wa wiki moja.
Mtawala alisema kuwa katika barua ya wakala huyo wameeleza kwamba majaribio hayo ya Kapombe yanatakiwa yaanze Juni 16 mwaka huu na atakuwa chini ya mafunzo maalum kutoka kwa makocha wazoefu wa mchezo huo.
Alisema kuwa pia akiwa huko atafanyiwa vipimo maalum vya afya kabla ya kuanza mazoezi.
Aliongeza kwamba katika majaribio hayo, Kapombe anatarajia kuwa na wachezaji wengine kutoka nchi za Afrika na Ulaya ambao watakuwa wameitwa na mawakala mbalimbali.
"Simba hatuna tatizo na mwaliko huo, na ukiangalia muda huo ligi itakuwa imemalizika, tutamruhusu na akirudi ataungana na wenzake kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Kombe la Kagame," aliongeza Mtawala.
Kapombe aliiambia NIPASHE kwamba hiyo ni nafasi nzuri kwake na atakapofanikiwa kwenda Uholanzi atajifunza mambo mengi na endapo wataridhika na uwezo wake atachangamkia ofa ya kusajiliwa huko kwa sababu kucheza Ulaya ndiyo ndoto yake na ya wachezaji wengi duniani.
Kapombe aliyesajiliwa na Simba akitokea Polisi Morogoro anamaliza mkataba wake mwezi Desemba mwaka huu na kumekuwapo na uvumi kwamba anajiandaa kuondoka bure Msimbazi na kujiunga Azam ambayo iko tayari kumpa dau la Sh. milioni 90.
Chanzo:NIPASHE
No comments:
Post a Comment