Kikosi cha Simba |
Kikosi cha Mgambo JKT |
BAADA ya kupata ushindi wa mechi mbili mfululizo, Simba kesho inatarajiwa kushuka tena dimba la Taifa Dar es Salaam kuwakaribisha maafande wa Mgambo Shooting ya Tanga katika pambano pekee la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mgambo iliyoizuia Yanga na kulazimisha sare ya bao 1-1 katika pambano lao la mwisho lililochezwa uwanja wa Mkwakwani, itakuwa inahitaji angalau sare tu ili kuweza kukwepa mstari ya kushuka daraja na kutoa baraka kwa timu za Toto African na Polisi Moro kuungana na African Lyon kurudi Ligi Daraja la Kwanza.
Maafande hao wana pointi 25 na wamesaliwa na mechi nyingine mbili mbali na huo wa Simba ambayo ushindi wake wa mabao 3-1 toka kwa Ruvu Shooting umewarejesha kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo iliyokwishafahamika bingwa wake na wawakilishi wa nchi katika michuano ya kimataifa mwakani.
Simba itautumia mchzo huo wa kesho kama kipimo kizuri cha kuwakabili wapinzani wao wa jadi Yanga wiki ijayo katika pambano la kufungia pazia la msimu huu wa 2012-2013.
Wapinzani hao wataumana kwenye uwanja wa Taifa, Mei 18 wakati pia siku hiyo kutakuwa na pambano mengine sita ya kufungia msimu kabla ya klabu kwenda mapumziko kusubiri msimu mpya ambao utakuwa na timu tatu zilizopanda daraja la Mbeya City, Rhino Rangers na Ashanti United.
Simba ambayo imekuwa na mabadiliko makubwa katika ufanisi wake uwanjani tangu kocha Patrcik Leiwig kuamua kuwatumia kikosi cha vijana na kuwatema 'mafaza', imeapa kuendeleza malengo yao ya kulinda heshima yake baada ya kutemeshwa taji na Yanga kabla ya ligi kumalizika.
Kocha Msaidizi wa klabu hiyo, Jamhuri Kihwelu 'Julio' amekuwa akisisitiza kuwa wataendelea kutoa dozi mpaka msimu unafungwa ili kulinda heshima yao na kuzitahadharisha timu wapinzani wajiandae kwa hilo.
Julio alisema hawatakubali kufedheheshwa siyo na Mgambo tu bali hata Yanga watakaoumana nao Mei 18 akidai ni lazima watoe dozi na kuwatilia mchanga kitumbua cha sherehe za ubingwa za watani wao hao jadi.
Simba ipo kwenye nafasi ya tatu kwa sasa ikiwa na pointi 42 mbili zaidi ya Kagera Sugar ambayo itashuka dimbani Jumamosi, huku Yanga wakiendelea kukaa kileleni na pointi zao 57 wakifuatiwa na Azam wenye pointi 48 na waliosaliwa na mechi mbili ikiwamo ya Jumamosi ijayo ikitokea kwenye michuano ya kimataifa.
Je, Mgambo itatoa baraka kwa Toto na Polisi kushuka daraja au itaendelea kuzipa pumzi za kutumua katika ligi hiyo mpaka pazia litakapofungwa rasmi Mei 18? Tusubiri tuone!
No comments:
Post a Comment