Mgambo JKT |
Kikosi cha Simba |
Mgambo ambao wameshatua jijini tangu majuzi imeshatangaza 'kiama' kwa 'Mnyama' kwamba wasitarajie mteremeko kama ilivyopata kwa Polisi Moro na Ruvu Shooting waliochezea vichapo na kuirejesha Simba katika nafasi ya tatu.
Kocha wa kikosi hicho cha Mgambo kilichoibania Yanga katika mechi yao ya mwisho iliyochezwa Mkwakwani, Mohammed Kampira ametamba kwamba wanachosaka leo ni pointi za kuwavusha kwenye janga la kushuka daraja.
Mgambo ina pointi 25 na inahitaji pointi moja tu ili kujihakikisha kusalia katika ligi hiyo wanayoicheza msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya kupanda toka Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita.
Hata hivyo Simba imesisitiza kuwa dhamira yao ni kuhakikisha wanataka kushinda mechi zao zilizosalia kwa nia ya kulinda heshima yao baada ya kunyang'anywa ubingwa na Yanga kabla ligi haijamalizika.
Simba ambayo haina hata nafasi ya kuiwakilisha nchi mwakani katika michuano ya kimataifa, ipo nafasi ya tayu baada ya kufikisha pointi 42 na kuwaengua Kagera Sugar walioikalia nafasi hiyo kwa kipindi kirefu kidogo pale Simba ilipokuwa ikitetereka kabla ya kuamka na kurejea kwenye makali yake.
Maandalizi ya pambano hilo yamekamilika na TFF imesema mchezo huo utaanza majira ya saa 10.30 jioni na kuhimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia mtanange huo wa aina yake.
No comments:
Post a Comment