STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, October 10, 2013

Henry, Redondo, Baba Ubaya kuwakosa Prisons

Henry Joseph



Redondo



NYOTA watatu wa Simba, Issa Rashid 'Baba Ubaya', Henry Joseph na Ramadhani Chombo 'Redondo' wamefahamika hawatakuwepo kwenye pambano kati ya timu yao na Prisons-Mbeya siku ya Jumamosi.
Baba Ubaya atalikosa pambano hilo kwa sababu ya kuwa majeruhi sawa na ilivyo kwa kiungo mkabaji Abdallah Seseme na beki wa pembeni Miraj Adam waliovishwa POP.
Henry na Redondo watakosekana katika mechi hiyo kutokana na kuenguliwa kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo Bamba Beach, Kigamboni.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga ni kwamba klabu yao imekuwa na utaratibu wa kuingia kambini kila wanapokabiliwa na mechi na wachezaji wanaofanya vyema kwenye mechi iliyopita na mazoezini ndiyo hujumuishwa kambini kutokana na mapendekezo ya makocha.
Kamwaga alisema hivyo kwa mtazamo wa makocha wao, Henry na Redondo hawakuwaridhisha na ndiyo maana wameungana na makinda wengine waliosajiliwa katika kikosi hicho kutoitwa kambini.
"Huu ni utaratibu wa kawaida na umekuwa ukitumiwa tangu alipokuwepo kocha Patrick Liewig, huwa nasema Simba ya sasa ni 'Simba-LUKU', yaani kadri unavyonunua umeme ndivyo utakavyoutumia na wachezaji kadri wanavyofanya vyema ndivyo wanavyopimwa na makocha," alisema.
Kamwaga alisema hajaelewa ni kwa nini  baadhi ya vyombo vya habari vimeliona tukio la kutoitwa kambini kwa akina Redondo na Henry kuwa kitu cha ajabu wakati ni utaratibu uliopo siku zote Simba.
"Klabu imesajili wachezaji 36 wakiwamo wale wa U20, na kambini huingia wachezaji 25 hasa wanaofanya vyema na kushawishi makocha, hivyo kuachwa kwa akina Henry na Redondo sidhani kama ni issue kubwa wakati msimu uliopita tulikuwa tunaingia kambini bila akina Boban, Kazimoto na watu hawakusema lolote," alisema Kamwaga.
Simba ina kibarua kigumu mbele ya Prisons ambayo imeonyesha kuzinduka hivi sasa ili kuweza kulinda nafasi yao kileleni kwani tayari inapumuliwa na timu za Azam na Mbeya City na iwapo itateleza na Yanga kushinda Kagera siku ya Jumamosi inaweza kuwaengua katika nafasi hiyo.
Mechi nyingine kwa wikiendi hii ni zile zitakazochezwa Jumapili kwa Ashanti kuvaana na Coastal Union kenye uwanja wa Chamazi, Ruvu Shooting kuvaana na Rhino Rangers uwanja wa Mabatini-Mlandizi, Mgambo JKT kujiuliza kwa Mbeya City jijini Tanga, Azam kuwaalika JKT Ruvu kwenye uwanja wa Taifa wakati Mtibvwa itapepetana na Oljoro JKT kwenye mashamba ya Miwa ya Manungu Turiani Morogoro.

No comments:

Post a Comment