Kocha wa Simba Abdallah Kibadeni akiwa kwenye mazoezi ya timu hiyo |
Akizungumza na MICHARAZO, Kibadeni alisema amelazimika kuitisha mkutano huo kutokana na baadhi ya magazeti kuripoti taarifa 'mbaya' dhidi ya kambi yake na benchi nzima la Simba kitu alichodai kinachafua taswira ya Simba na kuleta sintofahamu miongoni mwa wanachama na mashabiki wao.
Kibadeni aliyeichukua timu hiyo baada ya Mfaransa Patric Liewig kutimuliwa alisema mkutano huo utafanyika majira ya saa 5 asubuhi ya kesho kwenye makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi.
"Kuna baadhi ya wanahabari wamekuwa wakituchonganisha Simba, hivyo nimeitisha mkutano kesho nizungumze kuweka mambo sawa, kadhalika kuelezea maandalizi ya jumla dhidi ya pambano leo na Prisons," alisema Kibadeni maarufu kama King Mputa.
Kibadeni aliongeza kuwa, kuanza sasa wanahabari watakaotaka kujua chochote kuhusu Simba ni lazima wapate taarifa hizo kwa Msemaji wa Klabu, Ezekiel Kamwaga hata yale ya ufundi ambapo atakuwa anawauliza benchi la ufundi na kutoa majibu kwa wanahabari ili kuhofia kuivuruga Simba inayoongoza Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na pointi 15.
Naye Msemaji wa Simba, Kamwaga alithibitisha kuwepo kwa mkutano huo wa kesho, akidai kocha wao hajafurahia na baadhi ya taarifa zinazoripotiwa zinazoonekana kama zina lengo la kuivuruga timu yao.
No comments:
Post a Comment