Haya
ni maelezo binafsi ya Mheshimiwa Ester Amos Bulaya bungeni Dodoma
November 4 2013 kuitaka serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya dawa za
kulevya na kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia wahalifu wa dawa
za kulevya.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 28(8) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la
mwaka 2013, napenda kutoa maelezo binafsi ya juu ya tatizo sugu la
uagizaji, uuzaji na usafirishaji wa dawa za kulevya linaloongezeka kwa
kasi kubwa nchini, lengo likiwa ni kuitaka serikali ifanye
mabadiliko/marekebisho ya sheria ya Dawa za kulevya na kuanzisha
Mahakama Maalum kushughulikia wahalifu wanaojihusisha na usafirishaji na
biashara ya dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika,
Nimeona ni wakati muafaka kutoa maelezo haya, ili Bunge lako tukufu na
Serikali ipate fursa ya kuona uzito wa tatizo hili kutokana na ukweli
kwamba katika miaka ya karibuni tatizo la dawa za kulevya katika nchi
yetu limeongezeka kwa kasi ya ajabu hali inayopelekea athari kubwa za
kiuchumi, kijamii na kiafya. Na mbaya zaidi kundi kubwa linaloathirika
ni kundi la vijana, ambao ndio nguvu kazi ya Taifa letu. Na mbaya zaidi
sasa hivi, wafanya biashara hawa wa dawa hizi haramu wameanza kuwatumia
watoto wa shule za msingi chini ya falsafa yao mpya “wapate wakiwa
wadogo…wafanye watumwa wa dawa za kulevya… na kupata uhakika wa soko la
baadae pale ambapo watakuwa wameajiriwa au wamejiajiri”.
Mheshimiwa Spika,
Tafiti za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba kuna
ongezeko kubwa na la kutisha katika matumizi ya dawa za kulevya aina ya
heroin na kwa njia ya kujidunga katika nchi za Kenya, Libya, Mauritius,
Shelisheli na Tanzania. Halikadhalika, Ripoti ya mpya ya hivi karibuni
ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na mihadarati na uhalifu
(UNODC) imetamka bayana kwamba Tanzania ni kinara wa kupitisha dawa za
kulevya katika nchi za Afrika Mashariki, na Mkoa wa Tanga ukitajwa kama
mkoa hatari zaidi!
Mheshimiwa Spika,
Ripoti hiyo inasema jumla ya Tani 64 za dawa za kulevya aina ya Heroin
ilisafirishwa bila kukamatwa kwenda au kupitia Afrika Mashariki ikiwamo
Tanzania kati ya 2010 na 2013. Na kwa Mkoa wa Tanga, ambao umetajwa wazi
kama eneo hatari zaidi Afrika Mashariki wastani wa ukamataji wa shehena
za dawa za kulevya eneo hilo umefikia KG 1,011 mwaka 2013 toka KG 145
mwaka 2010. Na kwamba Dola za Kimarekani takriban milioni 160 zinatumiwa
na Watanzania na wakenya kila mwaka kwa utumiaji na usafirishaji kwa
mwaka!Hili sio jambo la kufumbia macho, lazima tuchukue hatua sasa.
Mheshimiwa Spika,
Lazima tuchukue hatua sasa, kwa sababu kama nilivyoainisha hapo juu
kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu tu (2010-2013), wakati Tani 64 za
dawa za kulevya zilipita bila kukamatwa…zikiwa mtaani zikiharibu vijana
na watoto wetu katika kipindi hicho hicho, kiasi kilichoweza kukamatwa
ni tani 1.6 tu! Takwimu hizo za kutisha zinatoa picha kwamba sehemu
kubwa ya shehena za dawa za kulevya hupitishwa bila kugundulika au
kukamatwa na vyombo vya dola!
TASWIRA YA NCHI KATIKA JUMUIYA YA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika,
Maelfu ya watanzania wanatumikia vifungo mbali mbali ikiwamo vifungo vya
maisha nje ya nchi, wengine wengi wamepoteza maisha kwa kunyongwa.
Nitatoa mifano michache; China peke yake inasemekana kuna wafungwa 176
(99% – dawa za kulevya) , Brazil kuna wafungwa zaidi ya 103 na Hong Kong
kuna zaidi ya watanzania 200 wenye kesi za dawa za kulevya, ambapo 130
zimeshakwisha hukumiwa na kesi 70 zikiwa zinaendelea!
Mheshimiwa Spika,
Aibu ya hivi karibuni, ambayo hatuwezi kuikwepa ni meli iliyosajiliwa
Tanzania (upande wa Zanzibar- MV Gold Star ) iliyoripotiwa kukamatwa
nchini Italia ikiwa imesheheni tani 30 za dawa za kulevya zenye thamani
ya pauni milioni 50 ( sawa na bilioni 123 za Kitanzania). Mheshimiwa
Spika, uhalifu huu, unaofanywa na mtandao huu wa watu wachache, lakini
wenye nguvu umewafanya watanzania wanaokwenda nje ya nchi kudhalilika
kutokana na upekuzi unaofanywa dhidi yao kwa hofu kwamba yawezekana na
wao wamebeba dawa hizo haramu.
HALI YA DAWA ZA KULEVYA
Mheshimiwa Spika,
Changamoto ya dawa za kulevya sio tatizo letu peke yetu ni tatizo ambalo
hata Jumuiya ya kimataifa imekuwa ikipambana nalo kwa kipindi kirefu
kwani tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 5 ya idadi ya watu wazima
duniani (watu takribani milioni 230) wanakadiriwa kutumia dawa za
kulevya.
Mheshimiwa Spika,
Tukiwa sehemu ya Jumuiya hii ya Kimataifa, Waheshimiwa Wabunge
mtakumbuka kuwa tarehe 19 Desember, 1988 Jumuia ya Kimataifa ilipitisha
Mkataba wa kupambana na dawa za kulevya yaani United Nations Convention
Against Illicit Traffic in Narcotic Drugs and Psychotropic Substances.
Tanzania ni sehemu ya Mkataba huo na hili limewekwa wazi hata kwenye
kifungu cha 55 cha Sheria ya kuzuia dawa za kulevya [sura 95 ya sheria
zetu kama zilivyorekebishwa mwaka 2002]. Mkataba wa mwaka 1988 ulikuwa
unakazia zaidi Mkataba wa mwaka 1961 (Single Convention on Narcotic
Drugs, 1961), Itifaki (Protocol) za 1972 zilizofanyia marekebisho
Mkataba wa mwaka 1971 (Convention on Psychotropic Substances, 1971).
Licha ya juhudi zote, tatizo la uuzaji na usafirishaji wa dawa za
kulevya, limezidi kuwa kubwa.
HALI YA DAWA ZA KULEVYA NCHINI NA MADHARA KWA AFYA YA BINADAMU
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 1995 tulitunga Sheria ya kuzuia biashara ya dawa za kulevya ambayo
ilianza kufanya kazi mwaka 1996 kupitia GN.No.10/1996. Sheria hiyo
inatumika Bara na Zanzibar. Kabla ya Sheria hiyo tulikuwa tuna Sheria
iitwayo the Dangerous Drugs Ordinance (Cap.95). Pamoja na kutungwa kwa
Sheria mpya, tatizo la dawa za kulevya limeendelea kuwa kubwa zaidi hapa
nchini. Ukamataji wa dawa za kulevya kwa miaka ya nyuma ilikuwa kidogo
na idadi ya walioathirika (mateja) ilikuwa ni ndogo kulinganisha na sasa
hivi.
Mheshimiwa Spika,
Ni kwa bahati mbaya sana, licha ya ukubwa wa tatizo, pamoja na athari
zake kwa jamii ya Watanzania, hakuna tafiti zinazoonyesha ukubwa wa
tatizo kwa Nchi nzima, tafiti nyingi zilizofanywa zimejikita katika
maeneo machache yaliyoathirika zaidi na dawa za kulevya . Tafiti
zinaonyesha kwamba Dawa zinazotumika kwa wingi ni bangi, mirungi,
heroine, mihadarati, vidonge na cocaine.Tafiti iliyofanywa na Shirika la
Umoja wa Mataifa linalohusika na mapambano dhidi ya dawa za kulevya
UNODC (United Nations Office on Drugs and Crime) zinaonyesha kwamba 0.2%
ya Watanzania, ambao ni karibia watu milioni 1.2 wameshawahi kutumia
dawa za kulevya aina ya heroine.
Mheshimiwa Spika,
Halikadhalika Shirika la afya duniani (World Health Organisation -WHO)
inaripoti kuwa takribani 0.2% ya Watanzania wameathirika na Ugonjwa wa
TB na takwimu za kitaifa katika program ya Kifua Kikuu na Ukoma Tanzania
zinaonyesha maambukizi ya TB ni 0.4% wakati tafiti katika hospitali ya
Taifa ya Muhimbili inaonyesha kwamba maambukizi ya TB kwa wanaotumia
dawa za kulevya ni 11% ambayo ni mara 44 zaidi ya kiwango cha maambukizi
kwa watu ambao hawatumii dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa maambukizi ya UKIMWI takwimu za mwaka 2011/2012 za TACAIDS
zinaonyesha kwamba 5.1% ya Watanzania wameathirika na virusi vya UKIMWI
wakati tafiti ndogondogo zinaonyesha maambukizi ya virusi ya ukimwi kwa
watu wanaotumia dawa za kulevya ni mara 10 zaidi ya maambukizi ya
kawaida. Kwa mfano 51.9% ya wanaotumia dawa za kulevya kwa njia
kujidunga sindano, 37% wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kuvuta na
kufanya biashara ya ngono na 22.6% kwa wanaotumia dawa za kulevya kwa
njia ya kuvuta.
Mheshimiwa Spika,
Madhara ya kiafya kwa utumiaji wa dawa za kulevya sio tu katika magonjwa
ya TB na maambukizi ya virusi vya ukimwi, bali pia katika homa ya ini.
Japokuwa hakuna tafiti za kitaifa zilizofanyika kuhusiana na mchango wa
matumizi ya dawa katika homa ya ini, tafiti ndogondogo za mwaka 2012
zinaonyesha kati ya 65% mpaka 75.6% ya watumiaji wa dawa za kulevya
wameathirika kwa homa ya Ini, hasa homa ya ini aina ya Hepatitis. Homa
ya ini ni hatari sana katika kupata magonjwa sugu ya ini ikiwepo kansa
ya ini na ini kushindwa kufanya kazi.
UKUBWA WA TATIZO NA UTENDAJI WA VYOMBO VYA DOLA
Kesi kubwa ya kwanza inayohusu dawa za kulevya ni ile ya mfanyabiashara
NURDIN AKASHA @HABAB V.R [1995] TLR. 227 (CAT) ambaye tarehe 20/7/1993
alikamatwa nyumbani kwake Msasani village akiwa na paketi 105 za
menthaqualone (mandrax) alizo ziingiza nchini kutoka Mombasa akitumia
malori yake. Sasa hivi tunaongelea uingizaji wa kilo kadhaa za dawa za
kulevya na siyo paketi tena. Mwezi Machi, 2010 kilo 92 za dawa za
kulevya aina ya Heroine zilikamatwa maeneo ya Kabuku Mkoani Tanga na
tayari washitakiwa 5 wanatumikia kifungo. Tarehe 19/12/2010 kilo 50 za
dawa za kulevya aina ya Heroini zilikamatwa tena wilayani Handeni Mkoa
wa Tanga. Mwezi Septemba, 2011 kilo 179 za dawa za kulevya aina ya
Heroini zilikamatwa Dar es salaam, tarehe 14/6/2011 Kilo 35 za dawa za
kulevya aina ya Heroine zilikamatwa mkoani Mbeya na tarehe Januari kilo
211 za dawa za kulevya zilikamatwa mkoani Lindi.
UTENDAJI WA OFISI YA DPP
Natambua jitihada zinazofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali ya
awamu ya nne katika vyombo vya dola kwa kufanikisha jitihada za
kuwakamata watuhumiwa wanaojihusisha na dawa za kulevya. Kutokana na
jitihada hizo, kuanzia mwaka 2008 mpaka mwaka huu wa 2013 watuhumiwa wa
dawa za kulevya ni kama ifutavyo:-
i) Cocaine kilo 395 zilikamatwa na washitakiwa waliokamatwa ni 1074
ii) Heroini kilo 768.8 na washitakiwa waliokamatwa ni 1130,
iii) Mirungi kilo 56,562 na washitakiwa waliokamatwa ni 3,712,
iv) Bangi kilo 487,472 sawa na tani 487 na washitakiwa waliokamatwa ni 20,255
v) Mandrax kilo 5 na gramu 9 na washitakiwa waliokamatwa ni 20.
Licha ya juhudi za baadhi ya watendaji waaminifu kuwakamata watu walioko
katika mtandao huu hatari kumekuwa na hujuma za dhahiri dhidi ya
wanaopambana na dawa za kulevya. Moja kati ya ofisi inayoshutumiwa kuwa
na maafisa wanaoshirikiana na wanamtandao, ni ofisi ya DPP
MTANDAO KATIKA OFISI YA DPP NA MAHAKAMA
Natambua kazi nzuri na jitihada zinazofanywa na baadhi ya watumishi
wazalendo kwa upande kwa Ofisi ya Muendesha Mashtaka, Majaji na Mahakimu
waaminifu. Lakini katika ofisi hizo za umma, kumekuwa na baadhi ya
watumishi ambao wamekuwa wakihujumu kesi za dawa za kulevya kwa
kushirikiana na watuhumiwa katika kupanga jinsi ya kuwasaidia washinde
kesi kwa kuwapatia taarifa za siri zinazohusiana na ushaidi na jinsi ya
kuharibu ushahidi nzima.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na kupanuka kwa mtandao huu wa kuhujumu, licha ya kushirikiana
na washitakiwa, mtandao uliopo katika Ofisi hiyo ya DPP umekuwa
ukituhumiwa kufanya njama za kushirikiana na baadhi ya watumishi wa
mahakama hasa Majaji kuhamisha kesi kupeleka kwa Majaji ambao wanadaiwa
kuhusika na mtandao huu (sihitaji kutaja majina ya Majaji hapa, baadhi
yao wanafamika na wengine wametajwa mara kadhaa na vyombo vya habari).
Mheshimiwa Spika,
Kwa kutumia mtandao huo, baadhi ya Majaji wamekuwa wanatafsiri sheria
kwa jinsi wanavyotaka na kuwapa dhamana watuhumiwa wa kesi za dawa za
kulevya ambazo hazina dhamana. Mfano mzuri ni kesi Na.6/2011, Jamhuri
dhidi ya Fred William Chonde na wenzake ambao walikutwa na kilo 179 za
Heroine yenye thamani ya shilingi Bilioni 6.5. Washitakiwa hawa
wanashitakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya ambalo kwa mujibu
wa kifungu cha 148(5)(a)(ii) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai
pamoja na kifungu cha 27(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia usafirishaji wa dawa
za kulevya halina dhamana. Kwa tafasiri yoyote ile aliyokuwa nayo
mheshimiwa Jaji, bado asingewapa dhamana kwani kifungu cha
148(5)(a)(iii) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na kifungu cha
27(1)(b) cha Sheria ya Kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya kinazuia
dhamana kwa kosa ambalo thamani ya dawa za kulevya inazidi shilingi
milioni kumi.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na Mahakama kutoa dhamana, washitakiwa wawili raia ya Pakistani
wametoroka na hawapo tena nchini. Aidha, katika kesi ya R. v. Mwinyi
Rashid Ismail @Mkoko, (KLR /IR 4143/2011), mshitakiwa aliomba dhamana
Mahakama Kuu wakati kesi ilikuwa bado ipo Mahakama ya Kisutu ndipo
wakili wa Serikali akamwambia jaji kuwa anaomba kuifuta.
Mheshimiwa Jaji huku akifahamu kuwa kesi hiyo imefika mbele yake kwa
ajili ya kusikiliza maombi ya dhamana tu, na kuwa ilikuwa haijafikishwa
Mahakama Kuu kwa taratibu wa sheria, aliamua kumfutia kesi mshitakiwa na
kuamuru kuwa yuko huru. Sambamba na hilo, katika kesi No. 794/2011
katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala Mheshimiwa Hakimu aliwafunga kifungo
cha nje kwa miezi kumi na tano washikiwa Abdurahman Shaban Sindanema,
said Nassoro Khamis na Abdurahim Haroub Said waliokiri kosa la kuuza na
kusambaza dawa za kulevya aina ya Heroini.
Mheshimiwa Spika,
Adhabu iliyotolewa na Hakimu huyu, haipo kwa mujibu wa sheria. Kwa
mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria ya kuzuia dawa za kulevya, adhabu
iliyowekwa kwa wauzaji au wasambazaji wa dawa za kulevya ni kifungo cha
maisha na si chini ya miaka ishirini (20) jela kwa kipindi hicho. Kesi
nyingine ni Na. 274/2005 Jamhuri dhidi ya Yusuph Hashim Nyose
aliyekamatwa na kilo 1.3 za dawa za kulevya aina ya Heroine alizokuwa
amemeza na kisha kuzitoa kupitia njia ya haja kubwa baada ya kukamatwa
na zilikuwa na thamani ya shilingi milioni kumi na mbili na laki sita
(12,600,000/=). Pamoja na ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi
sita(6) wa upande wa Jamhuri ikiwa ni pamoja na mkemia aliyethibitisha
kuwa ni dawa za kulevya na mashahidi walioshuhudia mshitakiwa akizitoa
kwa njia ya haja kubwa, Hakimu alimuachilia huru.
Mheshimiwa Spika
Katika hukumu yake Hakimu alisema kuwa ameridhika kuwa hizo ni dawa za
kulevya na zina madhara kwa binadamu na kuwa hana ubishi kuwa mshitakiwa
alikutwa nazo. Hata hivyo alimuachilia huru kwa kuwa upande wa mashtaka
umeshindwa kuelezea mbinu walizotumia kumgundua mshitakiwa kuwa alikuwa
amebeba dawa za kulevya kabla ya kumkamata. Mfano mwingine ni hukumu
iliyotolewa tarehe 4/5/2007 inayoihusisha Jamhuri dhidi ya Chriswell
Simon Mobini (561/2007) ambapo mtuhumiwa alikamatwa tarehe 9/4/2007
katika uwanja wa JKNA akiwa na pipi 93 aina ya heroine yenye thamani ya
zaidi ya shilingi milioni 30 za kitanzania. Baada ya kufikishwa Mahakama
ya Kisutu na kufunguliwa mashtaka chini ya kifungu 16 (1) (b) (i) cha
dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika,
Katika shauri hili, Hakimu alimwachia huru baada ya mshtakiwa kulipa
faini ya shilingi milioni 1 za kitanzania kwa maelezo kwamba kwa
kumtazama tu mtuhumiwa, anaonekana ni mgonjwa wa vidonda vya tumbo na
hivyo hawezi kupata huduma nzuri iwapo atapelekwa rumande! Hii ni mifano
michache tu kati ya mingi iliyopo!
KESI ZILIZOKO MAHAKAMANI
Mheshimiwa Spika,
Kama nilivyoainisha hapo juu, na ili kuonyesha msisitizo naomba nirejee
takwimu husika kama ifuatavyo, kwamba kati ya watuhumiwa 26,191
waliokamatwa mpaka sasa kuna jumla ya kesi 89 tu zinazosubiri
kusikilizwa Mahakamani. Katika vikao vya Mahakama Kuu vilivyokaa kuanzia
mwezi Augosti hadi Octoba, 2013 hakuna kesi hata moja ya dawa za
kulevya iliyosikilizwa na kutolewa hukumu, japo zilikuwa zimepangwa.
DHANA YA UHURU WA MAHAKAMA
Mheshimiwa Spika,
Natambua kuwa Mahakama ni muhimili unaojitegemea katika kutenda shughuli
zake na iko huru. Natambua pia kuwa Bunge haliwezi kuingilia shughuli
za Serikali au Mahakama. Lakini pamoja na uhuru huo, Bunge hili limekuwa
linakosoa Serikali pale linapoona imekosea. Kwa ujumla lazima kuwe na
checks and balance. Pamoja na mapungufu niliyoelezea hapo juu kuhusiana
na mwendendo wa Mahakama katika kusikiliza kesi za dawa za kulevya,
Mahakama imekuwa inafanya kazi zake bila kukosolewa na chombo kingine na
ndiyo maana baadhi wamekuwa wakitumia dhana ya uhuru wa Mahakama
vibaya.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na matumizi mabaya ya uhuru wa Mahakama kwa baadhi ya watumishi
wa Mahakama, ni mapendekezo yangu kwamba Serikali iunde tume maalumu ya
kiuchunguzi kuchunguza mwenendo wa kesi hizi za dawa za kulevya ili
watakao bainika kuwa wametumia nafasi /wadhifa/ madaraka yao vibaya
wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuvuliwa madaraka
waliyonayo. Kwa kufanya hivyo, itaonyesha kuwa hakuna aliye juu ya
sheria. Na itakuwa ni fundisho kwa wengine. Na taarifa ya Tume iletwe
katika Bunge lako tukufu kwa hatua zaidi.
KESI KUSIKILIZWA NA MAHAKIMU WASIO NA MAMLAKA
Mheshimiwa Spika,
Kwa ujumla watuhumiwa wote wanaokamatwa wakisafirisha dawa za kulevya
hutakiwa kufunguliwa mashtaka chini ya kifungu 16(1)(b)(i) cha sheria ya
dawa ya kulevya. Kosa hili halina dhamana na husikilizwa na Mahakama
Kuu peke yake. Hata hivyo baadhi ya Mahakimu wamekuwa wakilisikiliza
kesi hizo na wengine kushirikiana na waendesha mashtaka hubadilisha hati
ya mashtaka na kufanya wawe na mamlaka ya kusikiliza kesi hizo. Mfano
ni shauri la Jamhuri dhidi ya Shirima (CC 433/2009).
Mheshimiwa Spika,
Katika shauri hili Mtuhumiwa alikamatwa tarehe 02/05/2009 katika Bandari
ya Dar es salaam akiwa na kilo 1 ya heroine yenye thamani ya Tshs.
18,000,000/=….Tarehe 05/05/2009 alifikishwa Mahakamani na kufunguliwa
mashtaka chini ya kifungu cha 16(1)(b)(i) cha sheria ya dawa ya kulevya,
tarehe 9/05/2009 hati ya mashtaka ilibadilishwa na mashtaka kuwa chini
ya kifungu 12(d) ya sheria ya dawa za kulevya . Tarehe 14/7/2009
aliamriwa kulipa faini ya Tshs. 4, 000,000. Ubadilishwaji wa vifungu vya
sheria katika hati ya mashtaka hulenga kuwasaidia watuhumiwa washtakiwe
na makosa madogo badala ya yale makubwa yenye adhabu kubwa kisheria.
Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 16(1)(b)(i) cha sheria ya dawa za kulevya kinataja kosa la
dawa za kulevya kuwa kosa ambalo halina dhamana. Hivyo waendesha
mashtaka kwa kushirikiana na watuhumiwa hupendelea kuwafungulia mashtaka
madogo chini ya kifungu cha 12(d) cha sheria ya dawa za kulevya. Katika
kesi ambazo watuhumiwa walifunguliwa mashtaka chini ya vifungu ambavyo
haviendani na makosa yao halisi , Mahakama zimekuwa zikitoa adhabu ndogo
ya faini na kuwaachia huru! tena katika mazingira mengine kutoa hukumu
ndogo kuliko ambayo imeainishwa katika sheria.
MAPUNGUFU YA SHERIA
Mheshimiwa Spika,
Sheria ya kuzuia dawa za kulevya haina adhabu kwa mtu anayesafirisha au
anayekutwa na kemikali bashirifu (Chemical precursors). Kemikali hizi ni
muhimu sana katika kutengeza dawa za kulevya aina ya Heroin na Cocaini,
crystal-methamphetamine. Muathirika wa dawa crystal-methamphetamine
hawezi kutibika maishani mwake (Permanent Brain Damage). Kwa sasa hivi
kuna wimbi kubwa la uingizaji wa kemikali hizo zinazoenda kuangamiza
nguvu kazi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
Miongoni mwa matukio ya uingizaji na usafirishaji wa kemikali hizo ni
kesi ya Saada Ally Kilongo aliyekamatwa uwanja wa ndege wa J.K. Nyerere
akiwa na 10 kilo za Ephedrine. Nyingine ni kesi ya Agnes Gerald Delwaya
(Masogange) na mwenzake waliokamatwa Afrika Kusini wakiwa na kilo 150 za
Ephedrine. Aidha, Rumishaeli Mamkuu Shoo na mwenzake wamekamatwa kwenye
Kiwanda cha kutengeza Ephedrine nchini Kenya na tayari alikuwa na kilo
hamsini (50) za kemikali hizo. Hawa watu licha ya madhara makubwa
waliolitelea Taifa, wako mtaani wanapeta na kujipongeza!
Mheshimiwa Spika,
Kama hatutarekebisha sheria mapema iwezekanavyo, tutajikuta tunakuwa na
kiwanda au viwanda vya kutengeneza dawa za kulevya hapa nchini. Hivyo,
wauzaji badala ya kuagiza dawa hizo nje ya nchi, wataanza kutengeneza
hapa na kuna taarifa kwamba pindi dawa za kulevya zinapokosekana
wafanyabiashara huuza kemikali hizo na watumiaji wanatengeza wenyewe na
kutumia.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na mapungufu yaliyojitokeza kama hoja yangu ilivyoeleza, naomba Serikali ifanye mambo yafuatayo:-
1: Iunde Mahakama Maalumu, haraka iwezekanavyo itakayokuwa na jukumu la
kushughulikia kesi za dawa za kulevya tu kama ilivyo Mahakama ya
Biashara na iliyokuwa Mahakama ya Ardhi.
2: Ifanye marekebisho ya sheria ya dawa za kulevya kwa kuongeza makosa ya kusafirisha, kuuza au kukutwa na kemikali bashirifu
3: Iundwe Tume ya kuchunguza baadhi ya watendaji wa Mahakama na Serikali
ambao kwa makusudi wamekuwa wakihujumu kesi za dawa za kulevya pamoja
na jitihada za Serikali katika kupambana na biashara hii haramu na
kuleta taarifa katika Bunge hili tukufu
4: Kiundwe haraka chombo huru chenye nguvu na mamlaka kamili kitakachokuwa na dhamana ya kupambana na dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Spika,
Naomba kuwasilisha.
No comments:
Post a Comment