STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, November 5, 2013

Kinyambe: Mvunja mbavu aliyegeukia muziki wa Injili

Kinyambe katika pozi zake za kisanii
MWENYEWE anasema baada ya kuwatumikia wanadamu kwa muda mrefu  kupitia fani ya uchekeshaji na muziki wa kizazi kipya, sasa ni wakati wake kuanza kumtumikia Mungu wake.
Mohammed Abdallah au James maarufu kama Kinyambe anasema anaamini ni vyema kukitumia kipaji alichojaliwa kumtumikia na kumtukuza Mungu kupitia muziki wa Injili.
Kinyambe anayesifika kwa kuigiza kama 'jitu zoba' huku akichezesha na kugeuza macho yake kama kinyonga, anasema anaamini njia ya kumshukuru Mungu kwa kipaji alichompa ni kuimba nyimbo za kumtukuza yeye.
"Wazo hili la kuimba muziki wa injili nilikuwa nalo kitambo kirefu, lakini nilibanwa na mambo ya dunia na kujikita zaidi katika kuchekesha na kuimba muziki wa kizazi kipya, ila kwa sasa naona nina nafasi ya kufanya hivyo."
Kinyambe anayetamba kwenye kipindi cha 'Vituko Show' na filamu mbalimbali za komedi anasema kwa kuanza kumtumikia Mungu amefyatua wimbo wa Injili unaoitwa 'Acha ya Dunia' aliomshirikisha muimbaji wa kwaya ya KKKT Makongolosi Chuya mkoani Mbeya, Mederick Sanga.
Mchekeshaji huyo anasema kibao hicho ni mwanzo wa safari yake katika miondoko hiyo, akipanga kutoa wimbo mmoja baada ya mwingine mpaka kukamilisha albamu hapo baadaye.
"Huu ni mwanzo tu, japo nitaendelea kuchekesha na kupiga muziki wa kizazi kipya," anasema.
Msanii huyo anadokeza kuwa, kuimba kwake miondoko ya Injili hakuna maana kwamba ameokoka bali anataka mashabiki wake kupata ladha tofauti.
Kinyambe aliyekuwa amepanga kufunga ndoa Julai mwaka huu kabla ya mipango yake kutibuka baada ya kutemana na mchumba wake, anafichua mchanganyiko wa majina yake kwa maana ya Mohammed na James inatokana na kuzaliwa na wazazi wenye dini mbili tofauti.
"Baba yangu mimi ni muislam na mama yangu ni mkristo. ndiyo maana unaona ninayo majina mawili, ila mie najiona niko kotekote tu kwa sababu ninayemuabudu ni Mungu tu," anasema.
Kinyambe (kushoto) akiwa na mchekeshaji mwenzake, Matumaini

UBUNIFU
Kinyambe anasema aliamua kubuni staili ya kuzungumza kama 'zuzu' na kuchezesha macho katika namna ya ajabu kama njia ya kutaka kusaka  mashabiki na kujitofautisha na wachekeshaji wengine.
"Niliamini bila ubunifu ni vigumu kuhimili ushindani, hivyo nikaibuka na staili hiyo, nashukuru nimepokelewa vema kiasi cha kujivunia," anasema.
Kinyambe anadai pamoja kujifanyisha makengeza na kuyageuza macho kila mara kama kinyonga, ukweli haumii wala kupata tabu kwa sababu ni jambo alilolizoea kulifanya kitambo kirefu.
"Sipati tatizo lolote kuyachezesha au kuyazungusha macho kama kinyonga hii ni kwa sababu nimeshazoea kwani nilianza kitambo kufanya hivyo tangu nikiwa shuleni," anasema.
Kinyambe aliyevutiwa kisanii na N!xau Toma 'Bushman', muigizaji nyota wa Namibia aliyecheza filamu za 'Gods Must Be Crazy', anasema kipaji cha sanaa ni cha kuzaliwa nacho kwani alianza kuvunja mbavu watu tangu akiwa kinda.
"Nilipokuwa mdogo, hasa shuleni nilikuwa kipenzi cha wanafunzi wenzangu kutokana  na tabia ya kuwachekesha, pia nilijishughulisha na sanaa ya uimbaji na uchoraji fani ninazoendelea nazo hata sasa," anasema.

MAFANIKIO
Kinyambe anayependa kula ugali kwa dagaa na kunywa maji na juisi tu, anasema jina lake la Kinyambe lina maana ya mkoba kwa lugha yao ya asili ya kabila la Kiwanji lililopo mkoani Mbeya.
"Niliamua kujiita hivi kama njia ya kumuenzi babu yangu kipenzi aliyekuwa na mkoba (kinyambe) aliokuwa akiutumia kuwekea vitu vyake hivyo nilipojitosa kwenye sanaa mwaka 2000, nilijipachika," anasema.
Kinyambe anasema tangu atumbukie kwenye sanaa hana mafanikio makubwa ya kujivunia, ingawa anashukuru fani imemwezesha kulamba ajira katika kampuni ya Al Riyamy Production na kupata umaarufu mkubwa unaomrahisishia mambo yake.
"Japo sina cha kujivunia, lakini nashukuru sanaa imenipatia ajira na pia kunikutanisha na wasanii wakubwa wenye majina kama akina Mzee Magari, Steven Kanumba, Jacklyne Wolper na wengine," anasema.
Msanii huyo mwenye matarajio ya kufika mbali kisanii pamoja na kimaisha, ili aje kuitunza vema familia yake na kwa sasa amekamilisha filamu zake nne anazotarajiwa kuzitoa moja moja. Filamu hizo ni Nyumba, Chumba cha Maiti, Polisi Feki, Fundi Kinyambe na Fumbafu Thana.
Kinyambe akiwa na msanii mwenzake Masai Nyota Mbofu
MUZIKI
Katika muziki msanii huyo aliyezaliwa mwaka 1985 Uyole mjini Mbeya akiwa mtoto wa pekee wa kiume na wa tatu kati ya watoto saba wa familia yao anatamba na nyimbo kama 'Maumivu' alioimba na Baguje, 'Maimuna' alioimba na Leila Tot na Erick Ivyoivyo na 'Kiduku Mpapaso' aliomshirikisha  Kesse.
Anasema lengo lake ni kufyatua albamu kamili itakayokuwa na nyimbo nane na kusisitiza kuwa, hajabahatisha kuingia kwenye muziki kwani ni fani anayoijua nje ndani kwa muda mrefu.
Tofauti na vijana wengi, Kinyambe anayemzimikia mkali wa zamani wa Daz Nundaz, Ferooz, hana mzuka kabisa na mambo ya soka, akidai hana timu yoyote anayeshabikia wala kufuatilia mchezo huo.
Kinyambe aliyesoma Shule ya Msingi Uyole pia ni mchoraji mahiri kazi aliyoifanya kabla ya kuingia kwenye sanaa miaka 13 iliyopita akipitia makundi mbalimbali, anawataka wasanii wenzake kutokata tamaa na hali nya vikwazo anavyokutana navyo akidai tukio la furaha maishani mwake ni siku alipokubaliwa kujiunga Al Riyamy.
"Kwa upande wa matukio ya huzuni ni vifo vya babu na mjomba wangu niliokuwa naiva  nao na kunisaidia mno," anasema.
Kinyambe akiwa studio akirekidi kazi zake
Baadhi ya makundi aliyopitia msanii huyo ni Ufunguo Sanaa, Greenwood na Mbeya Films na filamu alizocheza awali alipoingia kwenye fani hiyo ni 'Msitu wa Maajabu','Kiapo Changu', 'God is Great', 'Leathal Weapon, iliyomkutanisha na marehemu Steven Kanumba, ndipo akaonwa na Al  Riyamy alikojipatia umaarufu mkubwa.
Kinyambe anayelia na wezi wa kazi za wasanii na kuiomba serikali iwasaidie pamoja na  kuiwekea miundo mbinu itakayowawezesha wasanii kunufaika na kazi zao, anasema fani  ya filamu Bongo imepiga hatua kubwa kwa sasa tofauti na siku za nyuma.
Kinyambe anayependa kutumia muda wake kusikiliza muziki na kuangalia 'muvi', amewamwagia shukrani wazazi wake, bosi wake Khalfan Abdallah, Shery Madhira, Mzee Shebby na wasanii wenzake anaoshirikiana nao Al Riyamy kwa jinsi  walivyomsaidia kwa hali na mali kufika hapo alipo.

No comments:

Post a Comment