Dar es Salaam. Wakati Msemaji wa Taasisi
ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi), Jumaa Almasi
akisema hali ya Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo
Mvungi imeanza kuimarika, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia
amedai kwamba bado hajapata fahamu.
“Hali yake inatia matumaini, ingawa bado
hajapata fahamu lakini madaktari wanaomtibu wameeleza kuwa anaendelea
vizuri. Nami nakubali kwa sababu hali aliyokuwa nayo juzi ilikuwa
tofauti, kwa kuwa najua kusoma mashine za kupumulia, inaonyesha mapigo
yake yanakwenda vizuri,” alisema Mbatia kauli ambayo inapingana na ile
ya Almasi ambaye alisema jana kuwa:
“Hali yake imeanza kuimarika ingawa bado
yupo ICU, ameanza kuzungumza ingawa kwa shida, lakini hamuwezi kumwona
kwa kuwa madaktari wameshauri kwamba anatakiwa kupumzika.”
“Tunajua kwamba Mvungi ni mtaalamu wa
masuala ya sheria, ni kiungo muhimu kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
tunashukuru masheikh na wanazuoni waliofika kumjulia hali. Mapadri pia
wamefika na kumwombea, lakini bado tunahitaji kuendelea kumwombea
zaidi,” alisema Mbatia.
Alisema pia wanaridhishwa na hatua za
kuwasaka watuhumiwa ambazo zinafanywa na vyombo vya ulinzi, ahadi
iliyotolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema ambaye alikuwa
miongoni mwa watu waliofika kumjulia hali.
Dk Mvungi alijeruhiwa usiku wa kuamkia
juzi, baada ya kukatwa mapanga na watu wasiojulikana waliovamia nyumbani
kwake Kibamba Msakuzi, Dar es Salaam.
Asimulia mkasa
Akisimulia mkasa huo, mjukuu wa Dk
Mvungi, Doris alisema babu yake alikabiliana na watu waliovamia nyumbani
kwake na kumwumiza mmoja wao kabla ya kuzidiwa na watu hao.
Alisema jana kuwa babu yake alimjeruhi
mmoja wa watu hao usoni kwa kitu ambacho hakukitaja na kwamba hali hiyo
ndiyo iliyochochea hasira zao na kumshambulia kwa mapanga mfululizo.
“Tulisikia mlipuko nje ya nyumba kwa
mbele, tukapiga kelele na kuamka wote, ghafla mlango wetu ukavunjwa kwa
tofali tukajaribu kutoka na kumkuta babu akiwa chini sebuleni,” alisema
Doris na kuongeza kuwa watu hao waliwaamuru kulala chini.
Alisema akiwa amelala chini alisikia
mmoja wa watu hao akidai kuwa ameumizwa usoni kauli ambayo ilifuatiwa na
mashambulizi mfululizo kwa Dk Mvungi na kisha wakamvutia jikoni huku
wakiendelea kumshambulia.
Doris alisema majambazi hao walikuwa
watatu na hawakuwa wamejifunika nyuso huku mmoja akiwa amevaa kofia na
kwamba laiti kungekuwa na mwanga chumbani wangewatambua. Alisema watu
wengine wawili walibaki nje na walipiga baruti mbele ya nyumba.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Salome
Emmanuel alisema Dk Mvungi alivamiwa nyumbani kwake na watu ambao
anadhani walikuwa wakifuatilia nyendo za mmoja wa wafanyakazi wake.
“Unajua mfanyakazi wake mmoja alikuwa
ndiyo kwanza amerudi kutoka matembezi na baada ya kuingia ndani
haikuchukua muda mrefu mlango ulivunjwa,” alisema Salome ambaye ni mke
wa dereva wa Dk Mvungi.
Salome ambaye wanaishi na mumewe jirani
na Dk Mvungi, alisema baada ya milipuko inayodhaniwa kuwa ni baruti,
alisikia kelele na kuona mwanga wa tochi kali ndani ya nyumba hiyo na
ndipo alipomwamsha mumewe na kuanza kuhangaika kutafuta namba za simu za
polisi.
Salome alisema wahalifu hao walionekana
kuwa na ufahamu mkubwa wa jiografia ya eneo hilo kwani walipita uani
ambako hakuna mwanga wa umeme na kuingia nyumbani kwa Dk Mvungi na hata
walipoondoka walipita jirani na kwao na muda mfupi baadaye walisikia
mngurumo wa pikipiki.
Polisi wakamata watano wakiwa na gongo
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
imesema inawashikilia watu sita wakituhumiwa kuhusika na tukio la
kumshambulia kwa mapanga Dk Mvungi.
Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Suleiman
Kova alisema watuhumiwa, ambao aligoma kutaja majina yao walikamatwa
wakiwa na pombe aina ya gongo lita 17 na kete 15 bangi. Baada ya
kuvamiwa, Dk Mvungi aliporwa bastola na kompyuta.
Kamanda Kova alisema baada ya msako
mkali wa polisi kwa kushirikiana na raia wema waliwakamata watuhumiwa
hao wakiwa karibu na eneo la tukio.
Misa
Kutokana na tukio hilo Mbatia alisema
leo saa 10 jioni kutakuwa na misa maalumu ya kumwombea Dk Mvungi, ambaye
pia ni Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu wa
NCCR-Mageuzi. Misa hiyo inatarajiwa kufanyika katika Kanisa la Mtakatifu
Joseph, Dar es Salaam.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment