*Kenya vs Rwanda, Zambia na Burundi, Zanzibar yaaga
Na Somoe Ng'itu, Nairobi
TIMU ya Taifa ya Uganda imemaliza mechi za hatua ya makundi kwenye michuano ya Kombe la Chalenji 2013 bila kupoteza mchezo wowote baada ya jana kuichapa Sudan kwa bao 1-0, hivyo sasa kesho itakutana na Kilimanjaro Stars katika mechi ya robo fainali itakayopigwa Uwanja wa Manispaa ya Mombasa.
Mechi nyingine ya robo fainali itakayopigwa kesho itamkutanisha mwenyeji, Kenya dhidi ya Rwanda ambayo jana iliichapa Eritrea kwa bao 1-0, hivyo kufuzu kama mshindwa bora (best looser) na kuifanya Zanzibar Heroes kuyaaga rasmi mashindano hayo.
Bao pekee la Rwanda katika mechi hiyo liliwekwa kimyani na Micheli Ndahinduka.
Mechi hizo za robo fainali zitaendelea Jumapili kwa Zambia inayoshiriki michuano hiyo kama timu alikwa ikivaana na Burundi wakati Ethiopia ikiwa na kibarua kigumu dhidi ya Sudan.
Wakati huo huo Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen, amesema haihofii timu yoyote watakayokutana nayo katika michuano hiyo inayoelekea hatua ya robo fainali nchini hapa.
Poulsen aliliambia NIPASHE jana asubuhi baada ya mazoezi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Wavulana ya Starehe kuwa, wachezaji wake wako tayari kuivaa timu yoyote.
Alisema kila timu itahofia mpinzani wake na kwamba amekipanga kikosi chake kucheza mfumo wa pasi nyingi fupi fupi badala ya ndefu.
Alisema ushindi wa mechi ya juzi dhidi ya Burundi, umekiimarisha kikosi chake na umewaongezea wachezaji wake hali ya kujiamini na kuona kwamba hakuna kinachoshindikana.
"Tuko tayari kuivaa timu yoyote, tumejiandaa vyema na tunataka kufanya vizuri zaidi mwaka huu, hatuna hofu na yoyote tutakayekutana naye," aliongeza kocha huyo.
Alisema pia timu yake inatarajia kusafiri leo mchana kuelekea mjini Mombasa tayari kwa mechi hiyo ya mtoano.
Daktari wa timu hiyo, Mwankemwa Mwanandi, alisema wachezaji wote wako vizuri na wamefanya mazoezi kama ilivyopangwa.
Jana katika mazoezi ya asubuhi Kim aliwagawa wachezaji hao katika makundi matatu, la kwanza likiwa ni la makipa, Ivo Mapunda, Deogratius Munishi na Aishi Manula.
Kundi la pili lililoongozwa na kocha msaidizi, Sylivester Marsh lilikuwa na Mbwana Samatta, Mrisho Ngasa, Amri Kiemba, Himid Mao, Said Morad, Frank Domayo, Erasto Nyoni, Salum Aboubakar 'Sure Boy', Thomas Ulimwengu na nahodha, Kelvin Yondani.
Wachezaji wengine waliobakia walikuwa ni Athuman Iddi 'Chuji', Haroun Chanongo, Ramadhan Singano 'Messi', Hassan Dilunga, Elias Manguli, Gambo Ismail na Michael Pius, wao walikuwa wanaongozwa na Poulsen.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment