BENDI kongwe ya muziki wa dansi ya Mlimani Park 'Wana Sikinde' kwa mara ya kwanza inatarajiwa kutambulisha nyimbo zao mpya ukiwamo 'Kibogoyo' na 'Kukatika kwa Dole Gumba' kwa mashabiki wao wa Sinza na vitongoji vya jirani.
Mlimani inayoendelea kufanya mipango ya kukamilisha albamu yao mpya tangu walipotoa albamu ya mwisho mwaka 2010 watatambulisha nyimbo hizo katika ukumbi maarufu wa Meeda Club, uliopo Sinza Mori.
Katibu wa bendi hiyo, Hamis Mirambo aliiambia MICHARAZO baada ya maombi ya muda mrefu toka kwa mashabiki wao wameamua kupeleka burudani yao kwa mashabiki hao wa Sinza Mori ambapo watazitambulisha nyimbo zote zitakazokuwa katika albamu yao ijayo pamoja na kukumbushia nyimbo za zamani zilizoifanya Sikinde kuwa Mabingwa wa Muziki wa Dansi Tanzania.
Mirambo alisema baadhi ya nyimbo mpya zitakazotambulishwa katika onyesho hilo maalum ni pamoja na 'Jinamizi la Talaka', 'Kibogoyo', 'Kukatika kwa Dole Gumba', 'Deni Nitalipa' na 'Nundu ya Ng'ombe'.
"Pia tutawapigia karibu nyimbo zetu zote za miaka ya nyuma tangu miaka ya 1970 mpaka zile za miaka ya 2000 pamoja na kuwaonyesha jinsi ya kucheza 'Nginde' kwani naamini mashabiki hao watakuwa wamesahau kutokana na kipindi kirufu kutopeleka burudani katika eneo hilo," alisema.
Mirambo alisema, anaamini mashabiki watakabahatika kufika katika onyesho hilo watapata burudani ambayo wameikosa kwa muda mrefu pamoja na kuwaona 'live' wanamuziki wakongwe ambao pengine baadhi ya mashabiki wamekuwa wakiyasikia majina yao kwa miaka mingi iliyopita na ikiwezekana watapiga nao picha kwa ajili ya ukumbusho.
"Fikiria mtu kama Hassani Reheni Bitchuka, Habib Jeff, Ally Jamwaka, Yusuf Benard, Mjusi Shemboza, Othman Mbaraka na wengine wana miaka mingi katika fani hii na majina yao yamekuwa yakisikika, lakini baadhi ya mashabiki wa sasa wa dansi pengine hawawajui kabisa hivyo ni fursa yao kuwaona na kupiga nao picha za ukumbusho," alisema Mirambo anayepuliza tarumbeta katika bendi hiyo.
No comments:
Post a Comment