Yanga watashangilia kama hivi hiyo Jumapili kwa Mbeya City? |
Dua za Mbeya City zitaleta maajabu Taifa mbele ya Yanga Jumapili? |
Yanga na Mbeya City zinazoshika nafasi ya pili na tatu katika msimamo wa ligi hiyo nyuma ya Azam, zitaumana Jumapili kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hizo zitaumana zikiwa na kumbukumbu ya kupata sare katika mechi zao zilizopita Yanga ikitoka suluhu na Coastal Union jijini Tanga na Mbeya City ikibanwa na Ruvu Shooting na kutoka sare ya 1-1 kwenye uwanja wa Mabatini-Mlandizi Pwani.
Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto amenukuliwa jijini Dar es Salaam akisema kuwa timu yao imeenda kuweka kambi Bagamoyo tangu mchana wa leo kwa ajili ya kujiweka vyema kabla ya kuwakabili wapinzani wao.
Yanga inayonolewa na kocha mpya 'Johannes van Der Pluijm, inakumbuka ilipolazimishwa sare ya 1-1 na wapinzani wao katika pambano lao la kwanza lililochezwa Septemba 14, mwaka jana walipoumana uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Watetezi hao waliokuwa nchini Uturuki kwa kambi ya wiki mbili, bado haijawaridhisha mashabiki wake kama kweli walikuwa Ulaya tofauti na duru lililopita waliporejea toka huko na kutoa vipigo vikali kwa wapinzani wao.
Hata hivyo, Kizuguto alisema kikosi chao kipo vyema kwa ajili ya mechi hiyo ya Jumapili ili kuhakikisha wanashinda na kurejea kwenye uongozi wa ligi hiyo uliochukuliwa jana na Azam baada ya kuishinda Rhino Rangers kwa bao 1-0 wakati Yanga ikitoka suluhu Mkwakwani Tanga.
Nayo Mbeya City iliyokwishawasili jijini Dar, imetamba kuwamba wamekuja Dar kuthibitisha kuwa sare walioipata Sokoine walipoumana na Yanga haikuwa ya kubahatisha na hasa ikizingatiwa tayari ligi wameshaizoea tofauti na mechi hiyo ya mwaka jana.
Kabla ya pambano hilo la Jumapili, siku ya Jumamosi kutakuwa na mechi mbili za ligi hiyo ambazo zote zitachezwa jijini Dar kwa pambano la Simba dhidi ya Oljoro JKT katika uwanja wa Taifa na pambano jingine litakuwa uwanja wa Chamazi kati ya Ashanti United dhidi ya Mgambo JKT.
Katika mechi za awali baina ya timu hizo, Simba na Mgambo zilizwasinda wapinzani wao kwa bao 1-0 kila moja na hivyo Ashanti na Oljoror zitakuwa na kazi ya kutaka kulipiza kisasi siku hiyo.
No comments:
Post a Comment