KLABU ya Barcelona
imepata pigo kubwa kuelekea katika mchezo wao wa ufunguzi wa La Liga
dhidi ya Elche utakaochezwa leo Jumapili kutokana na taarifa za kukosekana
kwa Neymar katika mchezo huo wa Camp Nou kutokana na majeruhi.
Nyota
huyo wa kimataifa wa Brazil, ndio kwanza alikuwa ameruhusiwa kucheza na
madaktari wa timu hiyo baada ya kupona majeruhi ya mgongo aliyopata
katika Kombe la Dunia lakini sasa anakabiliwa na majeruhi
mengine.
Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa klabu hiyo, imedai
kuwa Neymar alikuwa akilalamika maumivu katika kifundo chake cha mguu wa
kushoto na baada ya vipimo imegundulika kuwa ana matatizo ambayo
yatachukua muda kidogo kupona.
Taarifa hiyo imeendelea kudai kuwa
kurejea mazoezini kwa mchezaji huyo kutategemea kumalizika kwa maumivu
hayo hivyo ni wazi hatakuwepo katika mchezo wa leo.
Neymar alicheza
mechi 26 za La Liga msimu uliopita na kufunga mabao saba lakini msimu
huu unaonekana tayari ameuanza vibaya kwa maumivu.
Kipute cha ligi hiyo ya Hispania kilianza usiku wa jana kwa kushuhudiwa Malaga wakitamba nyumbani kwa kuitandika Athletico Club bao 1-0, Sevilla ikilazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Valencia, huku Granada ikivuna ushindi nyumbani dhidi ya Deportivo la Coruna kwa kuilaza mabao 2-1 na Almeria na Espanyol wakitishana nguvu kwa kufungana bao 1-1.
No comments:
Post a Comment