WAPO baadhi ya mashabiki wa soka wanaishangaa Simba kwa kuamua kumrejesha kikosini kiungo wao wa zamani, Shaaban Kisiga 'Marlon' kwa kuamini kuwa ni 'zilipendwa'.
Hata hivyo kwa wanaotambua kipaji na uwezo mkubwa wa nyota huyo wa zamani wa Stars aliyetokea Mtibwa Sugar wanajua Simba itavuna nini kwa Kisiga.
Licha ya kuwepo dimbani kwa muda mrefu, bado uwezo wa Kisiga ni ule ule zaidi umeongezeka kutokana na uzoefu alionao na jinsi anavyojitunza kama mwenyewe anavyosema.
"Kisiga ni yule yule, hajabadilika kitu sanasana ameongeza mzoefu zaidi. Nimerejea Simba baada ya miaka 9 ili kuirejeshea heshima," anasema.
Kisiga aliyefanya kazi na Phiri miaka 10 iliyopita anasema Mzambia huyo siyo bonge la kocha tu, bali ni baba mlezi anayejua kukaa na wachezaji na kuwafanya wafanye kazi zao kwa ufanisi dimbani.
"Binafsi nimefurahi kurejea Simba na kukutana tena na Phiri, Simba watarajie makubwa msimu huu chini ya kocha Phiri," anasema.
Kuhusu ushindani ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, Kisiga anasema amejiandaa kupambana akitumia uzoefu alionao kuhakikisha anapata namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza.
"Ndani ya Simba kuna ushindani mkubwa kwani kuanzia namba 6-11 kuna vipaji vikubwa hivyo kufanya kila mchezaji kupambana kujihakikishia namba jambo ambalo hata mimi nalifanya," anasema.
Nyota huyo aliyewahi kucheza soka la kulipwa Umangani, anasema ubinafsi na chuki ndivyo zinavyoua vipaji vingi vya soka nchini na kuikwamisha Tanzania kutamba kimataifa kwenye michuano ya kimataifa.
Anasema wapo wachezaji waliokatishwa tamaa na kuacha soka wangali wana uwezo mkubwa dimbani na kuwataka wadau wabadilike kama wanataka Tanzania ifanye vyema kimataifa.
"Leo vipaji vya akina Said Sued, Nurdin Bakar au Boban (Haruna Moshi) vimepotea kwa sababu ya chuki na ubinafsi, siyo kama soka lao limeisha. Hatuwezi kufika mbali kwa hali hii," anasema.
Anasema uteuzi na usajili wa kujuana na kubebana umekuwa ukifanya timu za Tanzania kuachwa mbali na mataifa hata yaliyokuwa nyuma.
Shabiki huyo wa Liverpool na asiyemhofia mchezaji yeyote dimbani anasema lazima viongozi na wadau wa soka waangalie kile ambacho mchezaji anachokifanya dimbani na siyo yale ya nje ya dimba.
"Wapo watu wanawahukumu wachezaji kwa matendo yao ya mitaani wakati uwezo wao dimbani ni msaada mkubwa kwa taifa, japo ni kweli nidhamu ni kitu cha muhimu katika kila jambo," anasema.
Anasema pia wadau wa soka wamekuwa wakiwabeza wachezaji wazoefu kwa kuwaita 'wazee' wakati Ryan Giggs na wakali wengine wa Ulaya wanazichezea klabu zao hadi wakiwa na miaka zaidi ya 40.
"Watanzania waache tabia hizi, mtu kucheza muda mrefu haina maana mtu ni mzee. Hata wale wanaonibeza sasa ndiyo hao hao watakaokuwa wakinishangilia dimbani kwa sababu soka nalijua na bado nina uwezo mkubwa," anasema.
Juu ya pambano asilosahau, Kisiga anasema ni lile la Nusu Fainali la Kombe la Kagame 2004 kati ya Simba na APR lililochezwa Kigali, Rwanda na Simba kung'olewa kionevu kwa kufungwa mabao 2-1.
"Nalikumbuka kwa jinsi tulivyopambana, lakini wenyeji walikuja kubebwa na kutuondosha mashindano kwa mabo 2-1," anasema.
Kisiga ambaye hana mpango kabisa wa kustaafu kwa sasa anasema anaamini ligi kuu ijayo itakuwa ngumu na yenye ushindani zaidi ya msimu uliopita kwa jinsi timu zinavyofanya maandalizi mazuri.
Hata hivyo anasisitiza kuwa msimu wa 2014-2015 ni wa Simba iwe isiwe kwa sababu wamefanya usajili mzuri chini ya uongozi makini na kocha bora hivyo siyo rahisi kulikosa taji linaloshikiliwa na Azam.
"Naamini ni zamu ya Simba safari hii, tutapambana kuirejeshea ubingwa na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, muhimu tushikamane na kuwa wamoja ndani ya Simba," anasema Kisiga.
No comments:
Post a Comment