Dkt. Agnes L. Kijazi |
MWELEKEO WA MVUA KWA KIPINDI CHA OKTOBA - DISEMBA 2014 NCHINI
A: UTANGULIZI
Taarifa hii inatoa tathmini ya mvua za masika (Machi - Mei)
2014 na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa na mvua kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba, 2014(Vuli).
B: TATHMINI YA
MVUA KIPINDI CHA MACHI – MEI, 2014
Katika msimu uliopita wa mvua za Masika Machi hadi Mei, 2014.
Maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa
maeneo machache ya mikoa ya Mwanza, Singida na Dodoma ambayo yalipata mvua za
chini ya wastani. Matukio ya vimbunga hususan Kimbunga ‘Hellen’ kilichotokea
katika Rasi ya Msumbiji kusini magharibi mwa baharí ya Hindi kilisababisha
ongezeko la mvua katika eneo la Pwani ya kaskazini.
Maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka:
Kanda ya Ziwa Victoria: Viwango vya mvua vilivyopimwa katika
vituo vya Bukoba na Musoma vilikuwa juu ya wastani. Kituo cha Shinyanga
kilipima mvua kiwango cha wastani wakati katika kituo cha Mwanza kiwango cha
mvua kilikuwa chini ya wastani.
Nyanda za juu kaskazini mashariki: Vituo vya Arusha, Lyamungo
na Kilimanjaro vilipima mvua juu ya wastani ilihali vituo vya Moshi na Same
kiwango cha mvua kilikuwa cha wastani.
Pwani ya kaskazini na visiwa vya Unguja na Pemba: Vituo vya
Dar es Salaam, Morogoro na Pemba vilipima mvua za juu ya wastani na vituo vya
Zanzibar, Amani, Kizimbani pamoja na Tanga mvua zilikuwa wastani.
Dondoo muhimu
1. Mwelekeo wa mvua kwa kipindi cha Oktoba-Disemba, 2014 Vuli
unaonyesha kuwa;
• Hali ya mvua
inatarajiwa kuwa ya kuridhisha katika
maeneo mengi ya nchi hata hivyo mvua za wastani hadi chini ya wastani
zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya
kusini mwa nchi hususan mkoa wa Ruvuma.
• Msimu huu
mvua zinatarajiwa kuanza mapema mwezi Septemba katika maeneo ya ziwa Viktoria,
nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kasikazini
2. Athari na Ushauri
• Mvua za
kutosha zinatarajiwa kwa shughuli za
kilimo katika maeneo mengi ya nchi.
• Vina vya maji
katika mito na mabwawa vinatarajiwa kuongezeka katika maeneo mengi ya nchi.
• Maji yatumike
kwa uangalifu na kuzingatia taratibu za uvunaji, uhifadhi na matumizi endelevu
ya rasilimali maji
• Matukio ya
migogoro inayosababishwa na mifugo, wanyamapori na shughuli za binadamu na
kilimo hayatarajiwi kujitokeza kwa kiasi kikubwa.
• Vipindi vya
mvua kubwa vinaweza kuongeza matukio ya mafuriko na uharibifu wa mali na
miundombinu.
• Milipuko ya
magonjwa yanayosababishwa na kutuama kwa
maji na utiririshaji wa majitaka usiodhibitiwa inaweza kujitokeza.
• Hatua stahiki
katika utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa maji safi na salama, na usambazaji
wa madawa, maji na chakula ikiwa ni hatua za kujiandaa na kukabiliana na
majanga yanayoweza kutokea
Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:
Nyanda za juu kusini magharibi: Vituo vya Mbeya, Tukuyu, na
Mahenge vilipima mvua juu ya wastani na kituo cha Sumbawanga kiwango cha mvua
kilikuwa cha wastani.
Kanda ya magharibi: Mvua juu ya wastani ilipimwa katika kituo
cha Kigoma ilihali vituo vya Kibondo na Tabora mvua zilikuwa ni za wastani.
Pwani ya kusini: Kituo cha Kilwa kilipima mvua juu ya wastani
na vituo vya Mtwara pamoja na Naliendele
mvua zilikuwa za wastani.
Kanda ya kati: Vituo vya Singida na Dodoma vilipima mvua chini
ya wastani na kituo cha Hombolo mvua za wastani.
Kanda ya kusini: Kituo cha Songea kiwango cha mvua
kilichopimwa kilikuwa juu ya wastani.
C: MIFUMO YA HALI YA HEWA
Katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba, 2014 hali ya
joto la bahari katika maeneo ya magharibi na kusini -magharibi mwa bahari ya
Hindi inatarajiwa kuwa juu ya wastani, upande wa mashariki mwa bahari ya Hindi
hali ya joto la wastani inatarajiwa.
Hali hii inatarajiwa kusababisha
upepo wenye unyevunyevu kutoka bahari ya Hindi kuelekea katika eneo
la Pwani ya Africa Mashariki. Aidha,
hali ya joto la chini ya wastani katika eneo la mashariki mwa bahari ya
Atlantiki (Pwani ya Angola) inatarajiwa kusababisha ongezeko la hewa yenye
unyevunyevu kutoka katika misitu ya Kongo kuelekea katika maeneo ya magharibi
na kusini Magharibi mwa nchi.
Hali ya joto la juu ya wastani katika eneo la Tropikali ya
bahari ya Pasifiki linatarajiwa kuendelea kwa kipindi cha miezi ya Oktoba hadi
Disemba, 2014. Hali hiyo inatarajiwa kuchangia ongezeko la mvua katika baadhi
ya maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua. Hali ya joto la juu ya wastani
katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi linaashiria kuwepo kwa
matukio ya vimbunga katika msimu wa mvua za Vuli kuanzia mwezi Novemba, 2014.
D: MWELEKEO WA
MVUA OKTOBA - DISEMBA 2014:
Kutokana na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa,
mvua za kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2014 zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo:
(i) Mvua za Vuli
(kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua)
Msimu wa mvua wa Oktoba hadi Disemba (Vuli) ni mahususi katika
maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini, kanda ya Ziwa
Viktoria na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Katika msimu huu mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya
wastani katika maeneo ya pwani ya kaskazini (mikoa ya Dar es Salaam, Pwani,
Tanga, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba),
nyanda za juu kaskazini mashariki (mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara)
pamoja na mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga na kaskazini mwa mkoa wa
Kigoma.
Msimu wa mvua za Vuli unatarajiwa kuanza mwezi Septemba, 2014
katika ukanda wa Ziwa Viktoria na kusambaa katika maeneo mengine. Hata hivyo,
mvua hizo zinatarajiwa kuanza mapema katika maeneo ya ukanda wa pwani (Mkoa wa
Tanga na kisiwa cha Pemba) na katika baadhi ya maeneo ya nyanda za juu
kaskazini Mashariki.
Kanda ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita,
Simiyu na Shinyanga): Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili
ya mwezi Septemba, 2014 katika mkoa wa Kagera na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma
na kuendelea kusambaa katika mikoa ya Mwanza,
Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za juu ya
wastani katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mara, Mwanza pamoja na
kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Maeneo mengi ya mkoa wa Shinyanga yanatarajiwa
kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga,
Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Septemba,
2014 katika maeneo ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja
na Pemba na kusambaa maeneo ya mkoa wa
Morogoro. Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika
maeneo mengi.
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro,
Arusha na Manyara):
Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza wiki ya pili na ya
tatu ya mwezi Septemba, 2014 na zinatarajiwa kuwa juu ya wastani katika maeneo
mengi ya mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na kaskazini mwa mkoa wa Manyara. Hata
hivyo, kusini mwa mkoa wa Manyara, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu
ya wastani.
(ii) Mvua za Msimu
(Novemba – Aprili) kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua.
Msimu wa mvua za Novemba hadi Aprili ni mahususi kwa maeneo ya
Magharibi mwa nchi, kanda ya
kati, nyanda za juu kusini-magharibi, kusini mwa nchi na pwani ya
kusini. Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2014 maeneo mengi yanatarajiwa
kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya mwezi Novemba, 2014.
Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani katika maeneo ya mikoa ya Rukwa,
Katavi pamoja na kusini mwa mkoa wa Kigoma. Hata hivyo, maeneo mengi ya mkoa wa
Tabora yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2014
na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Nyanda za juu Kusini Magharibi: (Mikoa ya Mbeya, Iringa,
Njombe na kusini mwa Morogoro):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi
Novemba, 2014 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo
mengi. Maeneo ya magharibi mwa mkoa wa Mbeya, mvua zinatarajiwa kuwa juu ya
wastani.
Maeneo ya kusini na pwani ya kusini (mikoa ya Ruvuma, Lindi na
Mtwara)
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi
Novemba, 2014 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa
maeneo mengi ya mkoa wa Ruvuma, yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini
ya wastani katika baadhi ya maeneo.
Izingatiwe kuwa pamoja na kuwapo kwa uwezekano wa matukio
mengi ya mvua kubwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua juu ya wastani,
hali hiyo pia inaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za
wastani hadi chini ya wastani.
Matukio ya Vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari
ya Hindi yanatarajiwa kuchangia katika mwenendo wa mvua nchini. Maeneo ambayo
hali ya mvua inaweza kuathiriwa zaidi na vimbunga ni pamoja na kanda ya kati,
Nyanda za juu Kusini Magharibi, Magharibi mwa nchi na maeneo ya ukanda wa
Pwani.
E: ATHARI NA USHAURI
Maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi
juu ya wastani isipokua baadhi ya maeneo ya kusini mwa nchi yanayotarajiwa
kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Matarajio ya mvua hizo pamoja na
ushauri kwa baadhi ya sekta za kiuchumi na kijamii zimeainishwa kama ifuatavyo;
Kilimo na Usalama wa Chakula
Katika maeneo mengi ya
nchi hali ya unyevunyevu wa udongo
inatarajiwa kuwa ya kutosheleza shughuli za kilimo. Hata hivyo, kwa maeneo
machache ya kusini mwa nchi (hususan Mkoa wa Ruvuma) vipindi vya upungufu wa
mvua vinatarajiwa mwanzoni mwa msimu na hivyo kuathiri kiwango cha unyevunyevu
wa udongo. Hali ya unyevunyevu wa udongo kupita kiasi inayoambatana na vipindi
vya mvua kubwa inaweza kusababisha
ongezeko la magugu, matumizi makubwa ya pembejeo, hivyo kuongeza gharama za
uzalishaji. Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba na pembejeo mapema pamoja na kuzingatia ushauri wa wataalam wa
kilimo kwa matumizi sahihi ya ardhi na mbegu.
Malisho na maji kwa
ajili ya mifugo na wanyama pori
Hali ya malisho na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo na
wanyama pori inatarajiwa kuwa nzuri katika maeneo mengi nchini. Hata hivyo,
wafugaji wanashauriwa kuzalisha malisho
na kuyahifadhi kwa matumizi wakati wa
kiangazi. Aidha, wafugaji wanashauriwa kufuata maelekezo ya wataalam wa ugani
katika maeneo yao hususan matumizi ya maji na malisho na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza.
Kutokana na hali ya mvua inayotarajiwa, matukio ya migogoro inayosababishwa na
mifugo, wanyamapori na shughuli za
binadamu na kilimo hayatarajiwi kujitokeza kwa kiasi kikubwa.
Maliasili na Utalii
Mamlaka za usimamizi wa shughuli za utalii na hifadhi za
wanyamapori zina shauriwa kuchukua hatua stahiki katika kuzuia uharibifu
wa miundombinu kama barabara na madaraja
ndani ya hifadhi dhidi ya adhari za mvua kubwa na za juu ya wastani katika
maeneo husika. Aidha, wawindaji, wapiga
picha za kitalii na makampuni ya kitalii yanashauriwa kuchukua tahadhari ya
uwepo wa mafuriko kutokana na mvua zinazotarajiwa.
Maji na Nishati
Mtiririko wa maji katika mito na vina vya maji katika mabwawa
vinatarajiwa kuongezeka katika maeneo mengi ya nchi kutokana na mvua za msimu
wa Vuli. Pamoja na matarajio ya kuwepo kwa mvua za juu ya wastani inashauriwa
kuwa maji yatumike kwa uangalifu na kuzingatia taratibu za uvunaji, uhifadhi na
matumizi endelevu ya rasilimali maji.
Mamlaka za Miji
Inashauriwa kuchukua
hatua za kuhakikisha kuwa mifumo na njia
za kupitisha maji zinafanyakazi katika kiwango cha kutosha kuhimili mvua
zinazotarajiwa ili kuepusha maji kutuama na kusababisha mafuriko na uharibifu
wa miundombinu, upotevu wa maisha na mali katika maeneo husika.
Sekta ya Afya
Ushauri unatolewa kwa jamii na sekta husika kuchukua hatua
stahiki katika kuzuia milipuko ya
magonjwa yanayosababishwa na kutuama kwa
maji na utiririshaji wa maji taka usiodhibitiwa katika maeneo yao.
Menejimenti ya Maafa
Mamlaka za maafa na wadau wengine wanashauriwa kuchukua hatua
stahiki katika utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa maji safi na salama, na
usambazaji wa madawa, maji na chakula ikiwa ni hatua za kujiandaa na
kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea kutokana na vipindi vya mvua kubwa na mvua za juu ya wastani
zinazotarajiwa.
Vyombo vya habari
Vyombo vya habari vinashauriwa kufuatilia, kupata na kusambaza
taarifa sahihi za mienendo ya hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA) na kutumia wataalam wa sekta husika katika kuandaa na kufikisha
taarifa za masuala mtambuka ya hali ya hewa kwa jamii. Aidha, jamii nayo
inashauriwa kufuatilia na kuzingatia taarifa sahihi za hali ya hewa na mirejeo
yake kupitia vyombo vya habari.
Angalizo: Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi
kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo,
viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi
katika maeneo madogo utazingatiwa katika
uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi. Watumiaji wa taarifa za
utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia tabiri za saa 24, siku 10 pamoja na wa
mwezi kama zinavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Itaendelea kufuatilia
mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini.
Dkt. Agnes L. Kijazi
MKURUGENZI MKUU
No comments:
Post a Comment