STRIKA
USILIKOSE
Sunday, November 9, 2014
HUYU NDIYE KHAMISI KAYUMBU 'AMIGOLAS' NYOTA ILIYOZIMIKA!
TASNIA ya Sanaa nchini imeendelea kupata machungu baada ya mmoja wa wanamuziki mahiri nchini, Khamis Kayumbu maarufu kama 'Amigolas' kufariki usiku wa kuamkia leo baada ya kuugua ugonjwa wa Moyo uliomfanya alazwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa siku kadhaa.
Mwanamuziki huyo aliyekuwa mkali wa utunzi na uimbaji aliyewahi kuziimbia bendi ya Bicco Stars, Chezima, African Stars kabla ya kutua Ruvu Stars aliyokuwa na mauti akiwa ndiye kiongozi wake.
MICHARAZO ina bahati ilifanya mahojiano maalum na mwanamuziki huyo katikati ya mwaka huu ambapo aliweka bayana mahali alipotoka, alipo na mipango yake ya baadaye, ingawa ndoto hazijatimia baada ya mauti kumkumba akiwa katika harakati za kuingia studio kurekodi nyimbo tatu za mwisho za bendi yake.
Ebu chungulia mahojiano hayo yaliyozaa makala iliyotoka kwenye gazeti la NIPASHE sambamba na kwenye blogu hii;
NYOTA wa muziki wa dansi nchini aliyewahi kutamba na bendi kadhaa ikiwamo African Stars 'Twanga Pepeta', Khamis Kayumbu 'Amigolas' amesema katu hatausahau mwaka 1995 maisha mwake.
Unajua kwanini?
Amigolas anasema mwaka huo ndiyo alipohamia rasmi katika bendi ya African Stars na kudumu nayo hadi mwaka 2013 ikiwa ni zaidi ya miaka 10 kabla ya kutua Ruvu Stars aliyepo kwa sasa kama kiongozi.
Anasema pia ni mwaka ambao alikaribia kwenda Ahera baada ya kuvamiwa na majambazi nyumbani kwake na kucharagwa mapanga mwilini mzima na wakora hao kabla ya kuokolewa na majirani zake.
"Itanichukua muda mrefu kuusahau mwaka huu, nilikuwa nife kama siyo majirani kuwahi kutoka baada ya mayowe tuliyopita, ila wakora hao waliofahamika kama Komando Yosso walinijeruhi," anasema.
Mtunzi na muimbaji huyo aliyewahi kuzipigia bendi za Bicco Stars na Chezimba Band, anasema anashukuru majirani hao walisaidia kuwafanya majambazi hayo kushindwa kumpora mali yoyote.
"Hawakufanikiwa kupora chochote zaidi ya kutujeruhi mimi na familia yangu, ilikuwa balaa na pengine ningekuwa marehemu kwa sasa kama siyo majirani kutoka mapema na kutuokoa," anasema.
Mwanamuziki huyo aliyevutiwa kisanii na gwiji, Hassan Rehani Bitchuka anasema anashukuru matibabu aliyopata yalimsaidia kumrejeshea uhai wake na kudunda mpaka leo akimshukuru Mungu.
Amigolas anashukuru muziki kumsaidia kwa mambo mengi ikiwamo kupata umaarufu na kutembelea mataifa mbalimbali duniani anasema kila akikumbuka tukio hilo usisimkwa kwa asivyoponea chupuchupu.
AMINATA
Amigolas anayependa kula wali na ugali kwa dagaa, kisamvu, samaki au kuku anasema licha ya kutojikita sana kwenye utunzi amewahi kutunga nyimbo chache zilizomjengea jina kubwa kwa mashabiki.
Moja wa nyimbo hizo ni 'Aminata' alioutunga Twanga Pepeta ambao unaendelea kutamba mpaka sasa, nyingine zikiwa ni 'Kila Mja Ana Kilio Chake' na sasa anajiandaa kuibuka na 'Kioo' akiwa na Ruvu.
"Nashukuru moja ya nyimbo zangu, Aminata mpaka sasa unatamba na kusumbua kuanzia redioni hadi videoni," anasema.
Shabiki huyo wa klabu ya Simba na Chelsea ya England anasema muziki wa Tanzania umepiga hatua kubwa, lakini bado hakuna umoja, upendo na mshikamano baina ya wanamuziki na wamiliki wa bendi.
"Pia watangazaji na hata Wizara inayohusisha na sanaa na Utamaduni na Michezo imeupa kisogo sana muziki wa dansi, kitu ambacho kinakatisha tamaa," anasema.
MARUFUKU
Amigolas mwenye mke na watoto wanne, watatu wa kike na mmoja wa kiume anasema anashukuru wanae kutokuwa na mzuka wa muziki na hatamani wanae kujiingiza kwenye fani hiyo.
"Sitaki hata kidogo wanangu wawe wanamuziki na ninashukuru hakuna hata mmoja mwenye mzuka na fani hii," anasema.
Mkali huyo anayejishughulisha na biashara zinazosimamiwa na mkewe, baada ya kutambulishwa na Bicco Stars aliokaa nao tangu 1991-94, alihamia Chezimba kabla ya 1995 kutua African Stars.
"Nimekaa Twanga Pepeta nikishiriki karibu albamu zote na mwaka jana nikaona ngoja nibadilishe upepo na nina matumaini makubwa ya kupiga hatua kimafanikio na kimuziki nikiwa na Ruvu Stars," anasema.
Mwanamuziki huyo anawashukuru mama yake mzazi, Asha Suleiman, familia yake yaani mke na wanawe pamoja na rafiki zake hasa Marcus toka Uswisi anayedai amekuwa akimsapoti kwa muda mrefu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment