Warioba Igombe, Morogoro
WAUMINI wawili wa Kanisa la Moravian mkoani Morogoro wamejeruhiwa
sehemu mbalimbali za miili yao, baada ya kukatwakatwa mapanga katika
vurugu zilizoibuka kanisani.
Inadaiwa kuwa, waumini hao walikatwa mapanga hayo na Jackson Mnyilimi, baada ya kutokea fujo kanisani hapo.
Akizungumzia tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
Leonald Paulo alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo ambazo zilitokea
jana katika Kijiji cha Makelele Tarafa ya Malinyi wilayani Ulanga.
Alisema tayari mtuhumiwa aliyefanya vurugu hizo anashikiliwa na
polisi ili sheria ichukue mkondo wake, baada ya kuhusishwa na tukio hilo
la kujeruhi waumini hao.
Aliwataja waliojeruhiwa ni Maria Silumbwe (47) na Aron Silumbwe (20), wote ni wakazi wa Malinyi.
“Tukio hilo lilitokea wakati waumini wa Kanisa hilo wakiingia
kanisani, ndipo kundi la mzee Ntony Mnyelemi (53), ambaye ni Mwenyekiti
wa Kanisa hilo, liliwanyang’anya ngoma wanakwaya wa kanisa hilo na
kusababisha kutokea kwa fujo kanisani hapo,” alisema Paulo.
Kamanda Paulo alisema kwa mujibu wa taarifa za awali, chanzo cha
vurugu hizo ni mgogoro wa uongozi wa Kanisa hilo, ambapo baadhi ya
waumini hawamtaki mchungaji mpya aliyetokea Mbeya aitwaye Johnson
Silumbwe (50).
Alifafanua, wakati polisi wakimshikilia Mnyilemi, wahutuhumiwa
wengine wanaohusishwa kufanya vurugu hizo walitoroka na jeshi hilo
linaendelea kuwatafuta.
Alisema watakapopatikana watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Naye, Mwandishi Claudia Kayombo anaripoti kutoka Dar es Salaam kuwa,
Kanisa la Moraviani Tanzania Jimbo la Misheni Mashariki limevitaka vyama
vya siasa kutoa wagombea waadilifu kwa kuwa, viongozi wa kisiasa wanayo
nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko kwa taifa kupitia maono, sera na
uadilifu wao.
Katibu Mkuu wa jimbo hilo, Mchungaji Emmaus Mwamakula alitoa kauli
hiyo juzi wakati akitoa salamu za mwaka mpya 2015 kwa Watanzania.
“Natoa mwito kwa vyama vya siasa watoe wagombea waadilifu kwa kuwa,
viongozi wa kisiasa wanayo nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko kwa
taifa kupitia maono, sera na uadilifu wao.
“Kwa kuwa mwaka tunaouanza ni wa uchaguzi katika nchi yetu, ninapenda
kutumia nafasi hii ili kugusia kuhusu uongozi mpya utakaochaguliwa
katika ngazi za udiwani, ubunge na urais.”
“Kwa kuwa, mchakato wa uchaguzi unaanzia ngazi za uongozi wa vyama
husika ambao ndiyo wenye majukumu ya kuwachuja wagombea wao, ningependa
kutoa mwito hasa kwa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu za vyama vya siasa
nchini kuhakikisha kuwa, vinateua majina ya watu walio waadilifu
miongoni mwa watakaojitokeza kugombea kupitia vyama vyao.
“Ni dhahiri kuwa, kila chama kinao mfumo au chombo kitakachowasaidia kumjua mgombea mwenye sifa na mwadilifu,” alisema.
Alibainisha kuwa, vyama ambavyo vitaruhusu rushwa kuamua mshindi
katika michakato yao ya ndani kwa kuwapitisha wagombea waliotoa rushwa
kwa wajumbe wakati wa michakato, vitakuwa vinajijengea mazingira ya
kushindwa kwa kuwa, wananchi watawakataa wagombea wa aina hiyo wakati wa
uchaguzi.
Alisema uongozi ni kazi yenye heshima sana katika jamii yoyote, maana mwanzilishi wa uongozi ni Mungu mwenyewe.
Hata hivyo, alisema katika miaka ya hivi karibuni imejengeka tabia
miongoni mwa wanasiasa na wale wanaowafanyia kampeni kuacha kutangaza
sera zao na kuanza kujihusisha na kampeni chafu kwa njia ya kuwachafua
wenzao.
“Tungependa jamii itambue kuwa, mtu yeyote anayetumia fedha nyingi
katika kuwachafua wenzake wakati wa kampeni, anakuwa amekosa sifa za
uongozi.
“Tunatoa mwito kwa watakaojitokeza kugombea nafasi yoyote ya uongozi
kuepuka kutumia lugha za vitisho na matusi dhidi ya wapinzani wao, iwe
kabla au wakati wa kampeni,” alitanabaisha Mchungaji Mwamakula.
Aidha, alitoa mwito kwa asasi za kiraia kuelimisha jamii katika kipindi cha uchaguzi.
“Nitumie nafasi hii pia kutoa mwito kwa asasi mbalimbali kwa jamii
kuwekeza katika elimu ya uraia wakati wote wa uchaguzi, kwa kuchapisha
wasifu na historia fupi za wagombea ili wapiga kura na wananchi waweze
kuwafahamu.
“Mpango huu utawasaidia wananchi kuwafahamu wagombea wengi, wakiwemo
ambao uwezo wao wa kujitangaza kupitia vyombo vya habari utakuwa ni
mdogo.
No comments:
Post a Comment