Yanga |
Azam |
Yanga waliopo Mbeya wanatarajiwa kuvaana na Prisons katika pambano litakalochezwa kwenye uwanja wa Sokoine, wakati Azam watakabiliana na maafande wa Ruvu Shooting katika pambano linalotarajiwa kuwa kali litakalochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Timu hizo mbili zilizotoka kwenye majukumu yao ya kuiwakilisha taifa katika michezo ya kimataifa ya Ligio ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho zote zipo kileleni zikiwa na pointi 25, Azam akitangulia kwa kuwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa kulinganisha na wapinzani wao.
Azam wanarejea kwenye ligi hiyo wakiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 5-2 kwenye uwanja wa Chamazi dhidi ya Mtibwa Sugar, wakati Yanga ikitoka kuwafyeka Mtibwa mabao 2-0.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alinukuliwa mapema jana kuwa kikosi chao kipo tayari jijini Mbeya kugawa dozi kwa maafande hao wa Magereza kabla ya kumalizia kazi kwa Mbeya City Jumapili na kuanza safari ya kuwafuata Wabotswana wa BDF XI kwa mechi ya marudiano ya kimataifa.
Azam wenyewe kupitia Meneja wao, Jemedari Said imetamba kuitoa nishai Ruvu Shooting kabla ya mechi yao ya mwisho ya ligi kuanza safari kuelekea Sudan kurudiana na El Merreikh katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo katika mchezo wa kwanza uliochezwa Jumapili walishinda mabao 2-0.
Licha ya Yanga na Azam kutamba kujiandaa kugawa dozi kwa wapinzani, timu za Ruvu Shooting na Prisons inayoburuza mkia nazo zimetamba hawatakubali kufa kikondoo katika mechi hizo za kesho kwani hata wao wanazihitaji pointi tatu toka kwa vigogo hao.
Msemaji wa Ruvu Masau Bwire na Kocha wa Prisonsa, David Mwamaja walisema kwa nyakti tofauti kuwa wanahitaji ushindi kuliko kitu kingine katika mechi hizo za kesho kwa lengo la kujiweka katika nafasi nzuri ndani ya ligi hiyo iliyoanza kushika kasi kwa mechi za duru la pili.
No comments:
Post a Comment