STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 5, 2018

Chirwa apigwa stop, Kocha Mbao ala kibano

Obrey Chirwa
Kocha wa Mbao, Etienne Ndayiragije
RAHMA WHITE
MZAMBIA Obrey Chirwa ambaye ameididia klabu ya Yanga kucheza na kutimkia kwao Zambia, amesimamishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuitimulia timu yake kwa muda usiojulikana kutokana na utovu wa nidhamu.
Chirwa ameasimamiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi maarufu kama Kamati ya Saa 72 iliyokutana jana Alhamisi na kujadili mechi mbalimbali za Ligi Kuu (VPL) Daraja la Kwanza (FDL) na Daraja la Pili (SDL).
Soma maamuzi ya kamati hiyo na adhabu zake katika ligi hizo;

LIGI KUU YA VODACOMMechi namba 72 (Mbeya City 0 vs Simba 1).Kamishna wa mechi hiyo Billy Mwilima amepewa Onyo Kali kwa kuruhusu mchezaji Hamisi Msabila wa Mbeya City kucheza mechi bila kuonyesha leseni, hivyo kukiuka Kanuni ya 14(16 na 17) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. 
Mechi namba 81 (Ndanda 1 vs Njombe Mji 1). Klabu ya Ndanda imepigwa faini ya sh 500,000 (laki tano) kwa kutowasilisha orodha ya wachezaji wake (team match list) kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre- match meeting) kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 14(2k) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu dhidi ya Ndanda katika mechi hiyo iliyofanyika Novemba 24, 2017 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu.
Pia Kamati imeiomba Sekretarieti ya Bodi ya Ligi kutoa Waraka mwingine kwa klabu kuzikumbusha kuhusu kutoa orodha ya wachezaji kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre-match meeting).
Mechi namba 83 (Yanga 1 vs Tanzania Prisons 1). Tanzania Prisons imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre-match meeting) ikiwa na maofisa watatu badala ya wanne, hivyo kwenda kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi hiyo iliyochezwa Novemba 25, 2017 Uwanja wa Azam Complex ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu.
Wachezaji Lambart Sabiyanka wa Tanzania Prisons na Obrey Chirwa wa Yanga wamesimamishwa kwa kuzingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kutokana na kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu, wakisubiri malalamiko dhidi yao kusikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.
Pia Kamati imeiomba TFF iipatie Bodi ya Ligi uamuzi (ruling) wa Kamati ya Nidhamu juu ya mchezaji wa Yanga kusimamishwa baada ya mechi dhidi ya Mbao FC wakati akisubiri mashtaka yake ili kuufanyia kazi kwa ajili ya mapendekezo ya marekebisho ya Kanuni.
Mechi namba 84 (Mbao 1 vs Mwadui 0). Klabu ya Mbao FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuruka uzio wa ndani na kwenda kushangilia katika eneo lisiloruhusiwa katika mechi iliyochezwa Novemba 25, 2017 Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Adhabu dhidi ya Mbao FC ni uzingativu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 90 (Lipuli 0 vs Tanzania Prisons 1).Mtunza Vifaa wa Lipuli FC, George Mketo amesimamishwa akisubiri suala lake la kuwatukana waamuzi katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 30, 2017 Uwanja wa Samora mjini Iringa kusikilizwa na Kamati ya Nidhamu. Uamuzi wa kumsimamisha umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kuhusu Usimamizi wa Ligi.
Mechi namba 94 (Mbao 2 vs Yanga 0). Kocha wa Mbao FC, Etiene Ndayiragije amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuondolewa kwenye mchezo (ordered off) na Mwamuzi kwa kushindwa kuheshimu taratibu na kuonywa mara tatu.
Adhabu hiyo dhidi ya Kocha Ndayiragije katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 31, 2017 Uwanja wa CCM Kirumba imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 40(11) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.
Pia klabu ya Mbao FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuonyeshwa kadi zaidi ya tano katika mechi hiyo. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(10) kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 96 (Mwadui 2 vs Ruvu Shooting 1).Klabu ya Mwadui imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuonyeshwa kadi zaidi ya tano katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 1, 2018 Uwanja wa Mwadui Complex. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(10) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu

LIGI DARAJA LA KWANZAMechi namba 37 Kundi B (JKT Mlale 1 v Mufindi United 0). Klabu ya Mufindi United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na Kiongozi wake Hussein Turuka kutoa lugha chafu kwa Mwamuzi katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 31, 2017 mjini Songea. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 40 Kundi B (Mawenzi Market 1 v Polisi Dar 0). Klabu ya Mawenzi Market imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kutaka kuwapiga waamuzi na kuwashawishi ball boys kuchukua mipira iliyotoka nje na kuwapelekea jukwaani.  Adhabu hiyo katika mechi hiyo iliyochezwa Desemba 31, 2017 ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Pia Kocha Mkuu wa Mawenzi Market amepewa Onyo Kali kwa kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre-macth meeting) kwa dakika saba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 39 Kundi C (Dodoma FC 3 v Alliance Schools 2). Klabu ya Alliance Schools imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa timu yake kuonyeshwa kadi zaidi ya tano katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 30, 2017 mjini Dodoma. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(10) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mchezaji Shaban William wa Alliance Schools amesimamishwa, hadi suala lake la kumpiga Mwamuzi litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF. Uamuzi wa kumsimamisha umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Usimamizi wa Ligi.
Waamuzi wote wanne; Andrew Shamba, Abdallah Mkomwa, Athuman Athuman na Omari Juma wamefungiwa miaka mitatu kila mmoja kwa kuchezesha mechi hiyo chini ya kiwango. Adhabu dhidi ya waamuzi hao imezingatia Kanuni ya 38(1a) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
Pia Kamishna wa mechi hiyo Mackshem T. Nzunda amefungiwa miaka mitatu kwa kushindwa kutoa taarifa ya mchezo kwa usahihi. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Kamishna.
Kamati imeomba suala la waamuzi hao ambao baadhi yao ni wa Ligi Kuu, kupitia TFF liwasilishwe kwenye chombo chenye dhamana ya kisheria ya rushwa kufanyiwa uchunguzi zaidi.

LIGI DARAJA LA PILIMechi namba 18 Kundi B (Africans Sports 1 v Kitayosce 2). Kitayosce imepigwa faini ya sh. 50,000 (elfu hamsini) baada ya kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre-match meeting) ikiwa na maofisa watatu badala ya wanne, hivyo kwenda kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu dhidi yao katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 29, 2017 jijini Tanga imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu taratibu za Mchezo.
Mechi namba 16 Kundi C (Mighty Elephant 1 v Green Warriors 3). Kocha wa Green Warriors, Azish Kondo amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kuondolewa kwenye mchezo (ordered off) na Mwamuzi kwa kutumia lugha chafu.
Adhabu hiyo dhidi ya Kocha Kondo katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 29, 2017 mjini Songea imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 40(10) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Makocha.
Mechi namba 18 Kundi C (Mkamba Rangers 0 v Boma 1). Klabu ya Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani (pitch).  Adhabu hiyo katika mechi hiyo iliyochezwa Desemba 29, 2017 ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 16 Kundi D (Area C v Nyanza). Timu ya Nyanza FC imeshushwa madaraja mawili na matokeo ya michezo yako yote imefutwa kwa kutofika uwanjani bila kutoa sababu yoyote na kusababisha mechi yao dhidi ya Area C iliyokuwa ichezwe Desemba 29, 2017 mjini Dodoma isifanyike.
Uamuzi huo dhidi ya Nyanza FC umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 28(1) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Kutofika Uwanjani. Pia kwa mujibu wa Kanuni ya 28(2) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Kutofika Uwanjani, imepigwa faini ya sh. 2,000,000 (milioni mbili) ambapo sh. 1,000,000 (milioni moja) itachukuliwa na Bodi ya Ligi, na sh. 1,000,000 (milioni moja) italipwa timu pinzani.
Vilevile Kamati imeiomba Sekretarieti kukiandikia barua Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Manyara (MARFA) ili kujua tatizo la timu hiyo.

MVUVUMWA VS FRIENDS Kamati imeipa Friends Rangers ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Mvuvumwa kuchezesha wachezaji ambao hawajasajiliwa (non qualified) katika mechi ya Kundi A Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya timu hizo iliyochezwa Oktoba 29, 2017. Mvuvumwa ilishinda mechi hiyo mabao 4-1.
Uamuzi huo dhidi ya Mvuvumwa umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(18) na 42(20) za Ligi Daraja la Kwanza. Nayo Friends Rangers imepewa ushindi kwa kuzingatia Kanuni ya 14(37) na ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo. 
Vilevile viongozi wa Mvuvumwa waliohusika kughushi leseni zilizotumiwa na wachezaji hao ambao hawakusajiliwa watafikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi.

ALLIANCE SCHOOLSKamati imepitia malalamiko ya Alliance Schools kupinga uchezeshaji wa Mwamuzi wa mechi yao dhidi ya Dodoma FC iliyofanyika Desemba 30, 2017 Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Baada ya kupitia hoja zote, Kamati haikukubaliana na malalamiko hayo kwa vile hayakuwa na vielelezo wala kanuni za kuyathibitisha. Pia kwa suala la muda, Kamati imejiridhisha kuwa kazi ya kutunza muda ni ya Mwamuzi.



No comments:

Post a Comment