STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 5, 2018

Simba kazi wanayo kwa Azam

Kocha Masudi Djuma akimkumbatia nahodha msaidizi, Mohammed Hussein 'Tshabalala', huku aliyekuwa Kocha Mkuu Joseph Omog na Mratibu, Abbas Ali wakishuhudia
Wachezaji wa Simba wakijifua mazoezini

RAHIM JUNIOR
HAKUNA namna ila kushinda tu. Ndivyo ambavyo Simba inapaswa kufanya wakati kesho Jumamosi itakaposhuka Uwanja wa Amaan, mjini Unguja kupepetana na Azam katika mechi ya kisasi itakayoamua hatma yao ya kutinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani hapa.
Simba ambayo ilipata ushindi wa kishindo usiku wa jana kwa kuikandika Jamhuri Pemba kwa mabao 3-1, itavaana na Azam usiku wa kesho na timu yoyote ikishinda itajihakikishia nafasi ya kutinga nusu fainali na kusubiri kujua itaungana na nani.
Azam inayotetea taji hilo ililolipata mwaka jana kwa kuichapa Simba kwa baoa 1-0 katika fainali, huo utakuwa ni mchezo wao wa mwisho na kwa sasa ikiwa na alama sita baada ya mechi tatu, kutokana na kupigwa 1-0 jioni ya leo na URA ya Uganda.
Simba yenyewe ipo nafasi ya tatu katika Kundi B ikiwa na alama nne baada ya mechi mbili, huku URA wakiongoza msimamo na pointi zao saba baada ya mechi tatu. Pambano la mwisho la Waganda hao litakuwa ni dhidi ya Simba  litakalopigwa Jumatatu jioni.
Hata hivyo Simba chini ya Kocha, Masudi Djuma imeonyesha kuwa na mabadiliko makubwa kulinganisha na ilipokuwa chini ya Mcameroon, Joseph Omog aliyetimuliwa na kama itacheza kama ilivyocheza mechi yao iliyopita, Azam ni lazima ijipange kwa Vijana hao wa Msimbazi.
Mrundi huyo aliyewapa taji Rayon Sports ya Rwanda, anatarajiwa kuendelea kumtegemea nahodha wake, John Bocco 'Adebayor' kuongoza mashambulizi akisaidiana wa nyota wengine, huku beki kiraka, Asante Kwasi aliyetupia kambani jana katika mechi yake ya kwanza akiwa na uzi wa Simba akitarajiwa kufanya yake.
Kwasi alisajiliwa na Simba hivi karibuni akitokea Lipuli na ameanza kuonyesha makeke yake na kuwafanya mashabiki wa Simba kutabasamu kwa kuamini kuwa timu yao inazidi kunoga, ikiwa siku chache tangu watolewa na kutemeshwa taji la Kombe la FA kwa kufungwa na timu ya Daraja la Pili, Green Warriors.
Azam iliyokuwa haijafungwa bao lolote katika michuano hiyo tangu mwaka jana walipobeba taji bila kupoteza, sio ya kubeza kwanui ukuta wake unaoongozwa na Mghana, Yakubu Mohammed na safu kali ya ushambuliaji chini ya Mghana mwingine, Bernard Arthur na chipukizi Paul Peter na Zayd na Shaaban Idd huenda isikubali kirahisi kupoteza mchezo huo na kutemeshwa taji la michuano hiyo.
Mbali na mchezo huo mapema jioni Singida United itakuwa uwanjani kupepetana na JKU katika mechi nyingine.

No comments:

Post a Comment