STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, February 23, 2014

Hivi ndivyo Extra Bongo ilivyozindua albamu yake Dar Live


Makhirikhiri walikuwepo kutoa burudani jana Dar Live
Kiongozi wa Extra Bongo, Ally Choky (kushoto) na Muumin Mwinjuma wakiimba kwa pamoja katika uzinduzi wa albamu ya Mtenda akitendewa usiku huu Dar Live.
Banza alikuwa kivutio kikubwa siku ya jana
Choki na Montanabe walifanya yao
Ally Choki na Banzastone wakiimba pamoja
BENDI ya muziki wa dansi ya Extra Bongo 'Wazee wa Kimbembe' usiku wa jana ilikata kiu ya mashabiki wa muziki nchini baada ya kuzindua kwa kishindo albamu yao ya  'Mtenda Akiitendewa'.
Uzinduzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Dar Live Mbagala jijini Dar es Salaam huku ukipambwa na makundi mbalimbali ya burudani ikiwamo bendi ya Mashujaa Musica, Linah, Amin, Makhirikhiri na  Khadija Kopa.
Extra Bongo ilipanda jukwaani kuanzia saa nane usiku baada ya makundi hayo kutoa burudani huku mkurugenzi wa bendi hiyo akiingia ukumbini kwa gari la wagonjwa akitanguliwa na waendesha pikipiki ambao ni maarufu kama bodaboda.
Wakati huo wanenguaji wa bendi hiyo walikuwa tayari jukwaani wakifanya vitu vyao kisha Choki akashuka katika gari hilo na kupanda jukwaani na kuonyesha ishara ya kuzima shoo hiyo na kuanza kuimba wimbo wa 'Mtenda Akitendewa'.
Tukio hilo liliwafanya watu waliofurika ukumbini humo walianza kushangilia huku wengine wakimtuza wakati akiimba na pia 'kushambulia' jukwaa sambamba na waimbaji wake akiwamo Banzastone.
Pamoja na uzinduzi huo kupata mashabiki wengi, ulitaka kuharibiwa na wingi wa makundi yaliyoalikwa kutoa burudani ambayo yalichukua muda mrefu jukwaani na hivyo kusababisha uzinduzi huo kumalizika alfajiri.
Baadhi ya mashabiki walisikika wakilalamika kuwa wingi huo wa makundi ya kusindikiza bendi ndiyo uliochangia Extra Bongo ichelewe kupanda jukwaani na hivyo kufanya baadhi yao kuchoka kabla ya kuishuhudia bendi hiyo.
"Choki angealika hata bendi moja tu ingetosha, lakini anachukua makundi mengi ambayo yametumia muda vibaya na sasa Extra Bongo inapanda jukwaani usiku wa maneno wakati sisi tumeshachoka," alilalamika shabiki mmoja.
Alisema kuwa watu walifika kuishuhudia Extra Bongo ikizindua albamu, lakini baadhi yao walijikuta wakichoka na kukata tamaa baada ya kusubiri kwa muda mrefu bila kuona bendi hiyo ikipanda jukwaani.
"Ni kweli kwenye shughuli

Barcelona yapigwa ugenini licha ya Messi kutupia

Messi akiwa hoi baada ya ttimu yake kunyukwa mabao 3-1 jana
Messi akidhibitiwa na wachezaji wa Real Sociedad
LICHA ya Lionel Messi kufunga bao linalomfanya kuzidi kuweka rekodi ya ufungaji mabao ndani ya Barcelona, mabingwa watetezi hao wameshindwa kuepuka kipigo ugenini dhidi ya Real Sociedad baada ya kjunyukwa mabao 3-1.
Kipigo hicho kimeifanya Barca kushindwa kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga na kjuiacha Real Madrid itanue, huku kukiwa na hati hati ya kuporomoshwa hadiu nafasi ya tatu iwapo Atletico Madrid itaibuka na ushindi leo dhidi ya Osasuna.
Bao la kujifunga la Alexander Song katika dakika ya 32, liliashiria balaa kwa wageni japo Messi alilisawazisha dakika nne baadaya baada ya kumalizia kazi nzuri ya Matrin Montoya na kufanya timu ziende mapumziko zikiwa nguvu sawa ya kufungana bao 1-1.
Kipindi cha pili wenyeji walicharuka zaidi na kujipatia mabao mawili yaliyofungwa na Griezmann  katika dakika ya 54 akimalizia pasi ya Carlos Vela, kabla ya Zurutuza kuongeza bao jingine dakika nne baadaye akimalizia pande la Griezmann.
Kwa matokeo hayo Barcelona wamesalia katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 60, baada ya kucheza mechi 25, huku Sociedad ikpanda hadi nafasi ya tano kwa kufikisha pointi 43.
Katika mechi nyingine zilizochezwa jana na mapema leo Celta de Vigo ikiwa nyumbani ilibanwa na Getafe na kutoka nao sare ya bao 1-1, huku Almería na Malaga nazo zikitoshana nguvu ya suluhu ya bila kufungana.
Kivumbi cha ligi hiyo kitaendelea leo kwa michezo kadhaa ambapo Rayo Vallecano itaumana na Sevilla, Real Betis itaialika Athletic Club, Valencia na Granada zitaonyeshana kazi na Osasuna itaialika Atlético Madrid na Jumanne Espanyol itaumana na Villarreal.

Saturday, February 22, 2014

HII NDIYO TOP 10 YA WALIONG'ARA KIDATO CHA NNE

http://1.bp.blogspot.com/-SUcYdsp6pq0/UU7zJboieNI/AAAAAAAAdo4/5fAU57VdG3M/s1600/NECTA.jpg
WASICHANA Wasichana waliofanya vizur kwenye mtihani huo wameongozwa na Robina Nicholaus (Marian Girls), Magrath Kakoko (St Francis), Joyceline Leonard Marealle (Canossa), Safarina W Mariki, Abby T Sembuche na Janeth Urassa (Marian Girls). Wengine ni Angle Ngulumbi (St Francis), Getrude James Mande wa Precious Blood (Arusha), Violet Mwasenga wa St Francis na Catherine Swai kutoka Marian Girls.
WAVULANA
Wavulana waliofanya Vizuri ni Sunday Mrutu wa Anne Marie, Nelson Rugola Anthony na Emanuel Mihuba Gregory wote kutoka Kaizirege, Razack Hassan wa St Matthew’s (Pwani) na Hamis Msangi kutoka Eangles (Pwani).
Wengine ni Joshua Zumba wa Uwata (Mbeya), Brian Laurent na Mohamed Ally wa Marian Boys (Pwani), Shahzill Msuya wa St Amedeus (Kilimanjaro) na Shabani Hamisi Maatu wa Mivumon Islamic Seminary (Dar es Salaam).

Simba, Azam kuvuna nini kesho Dar?

Simba itavuna nini kwa JKT Ruvu?
JKT Ruvu itaendelea kuwa urojo kesho katika ligi kuu mbele ya Simba?
Azam watahimili vishindo vya Prisons baada ya kung'oka Kombe la Shirikisho Afrika?
Prisons wataendeleza ubabe wao walioonyesha kwenye mechi za duru la pili kesho kwa Azam au...?!
BAADA ya kupata ushindi wa mechi tatu mfululizo na sare moja katika duru la pili, Prisons ya Mbeya kesho itavaana na timu ambayo haijapoteza mechi yoyote katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam huku Simba wakivaana na maafande wa JKT Ruvu waliochabangwa mabao 6-0 katika mechi yao iliyopita.
Mechi hizo mbili zitachezwa kesho jijini Dar es Salaam zikiwa ndiyo pekee katika mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania bara kukamilisha mzunguko wa 19.
Azam wanaorejea kwenye ligi baada ya kung'olewa kwenye Kombe la Shirikisho la Ferroviario de Beira wataivaa Prisons kwenye uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya jiji, huku Simba itaikaribisha Ruvu inayonolewa kwa sasa na kocha Fred Minziro kwenye uwanja wa Taifa.
JKT walikuwa wahanga wa Prisons kwa kukubali kipigo cha 6-0 na kuweka rekodi ya kufungwa mabao nande katika mechi mbili zilizopita, kipigo kingine walipewa na ndugu zao Ruvu Shooting ambayo leo imekumbana na dhahama kwa kulazwa mabao 7-0 na watetezi Yanga.
Mechi hizo zinasubiriwa kwa hamu kwa sababu ndizo zinazoweza kubadilisha msimamo wa ligi hiyo kwa timu zilizopo kwenye Nne Bora, kwani Azam ikishinda itarejea kwenye nafasi yake ya kwanza ambayo imechukuliwa na Yanga jioni ya leo baada ya ushindi wake dhidi ya Ruvu.
Simba nayo ikishinda itaiengua Mbeya City na kukalia nafasi ya tatu baada ya vijana hao wa Juma Mwambusi kuchezea kipigo toka kwa Coastal Union jijini Tanga jioni ya leo.
Simba ina pointi 32, tatu nyuma ya Mbeya City, lakini ikiwa na uwiano mzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Azam wenyewe wana pointi 36, mbili zaidi ya Yanga wanaoongoza sasa kwa pointi 38, hali inayofanya mechi za kesho kuwa na msisimko mkubwa mashabiki wakitaka kuona Prisons itaendeleza rekodi yake ya kukusanya pointi 10 katika mechi zake nne za duru la pili na kuvunja mwiko wa Azam kupoteza mchezo!
Wana Lambalamba ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mechi yoyote katika ligi ya msimu huu na katika mechi zake za duru la pili imekuwa ikigawa dozi nene hali inayoifanya Prisons kuwavaa wapinzani wao hao kwa tahadhari kubwa.
Tayari timu zote nne zimekuwa zikitambiana kila moja ikidai imejiandaa kushinda, lakini matokeo ya mwisho yatategemea baada ya dakika 90 kwa namna timu hizo zilivyopigana katika kuwakabili wapinzani wao.
Simba ambayo imekuwa na mwenendo mbovu tangu duru la pili lianze itataka ushindi ili kutuliza munkari wa mashabiki na wanachama wao baada ya kujikuta wakipoteza pointi saba kati ya tisa katika mechi zao tatu zilizopita ikiambulia sare mbili dhidi ya Mtibwa Sugar na Mbeya City na kulazwa na Mgambo JKT.
Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2013-2014     
                                      P    W     D     L     F    A   GD  PTS
01.Yanga                        17   11    05   01   41   12   29  38
02.Azam                         16  10    06   00   29   10   19   36
03.Mbeya City                19   09    08   02   24   16   08  35
04.Simba                        18   08    08   02   33   16   17  32
05.Kagera Sugar             19   06    08   05   16  15   01  26
06.Coastal Union            19   05    10    04  14  09   05  25
07.Mtibwa Sugar            19   06    07    06   23  23   00  25
08.Ruvu Shooting            19   06   07   06    20  26  -06  25
09.Mgambo                    19   05    05    09   12  27  -15  20
10.Prisons                       17   04    07    05   15  16  -01  19
11. JKT Ruvu                  18   06    01    11   13  27  -14  19
12.Oljoro                        20   02    09    09   15  30  -15  15
13.Ashanti                       18   03    05    10   15  30  -15  14
14.Rhino Rangers            19   02    07    10   12  23 -11  13

Real Madrid yapanda kileleni Hispania


Real Madrid's Gareth Bale
MABAO matatu yaliyofungwa na Illaramendi katika dakika ya 34, Gareth Bale la dakika ya 72 na lile la Isco la dakika ya 81 yalitosha kuipaisha Real Madrid hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) walipoifumua Elche mabao 3-0.
Madrid wakiwa uwanja wa nyumbani wa Santiago Bernabeu ilionyesha dhamira ya kupata ushindi kwa Illarramendi kufunga bao kwa pasi ya Pepe, bao lililodumu hadi mapumziko.
Bale mchezaji ghali kuliko wote katika usajili, alitupia bao la pili akimalizia kasi ya Xabi Alonso kabla ya Karim Benzema kumtengea Isco kufunga bao la tatu.
Kwa ushindi huo, Madrid imefikisha pointi 63 na kuziengua kileleni Barcelona na Atletico Madrid zenye pointi 60 kila moja ambazo zina mchezo mmoja mkononi, Barca wakitarajia kushuka dimbani muda mchache baadae ugenini dhidi ya Real Sociedad, huku wenzao wakitarajiwa kucheza kesho.




Arsenal, Man City, West Ham 'zaua' England


Olivier Giroud
Wachezaji wa Arsenal wakishangilia moja ya mabao yao leo
Carlton Cole
Wachezaji wa West Ham United wakishangilia mabao yao

Yaya Toure scores for Man City against Stoke
Yaya Toure akifunga bao lililoipa ushindi Manchester City
ARSENAL imeendelea kuifukuzia Chelsea kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England baada ya muda mfupi uliopita kuichabanga Sunderland mabao 4-1, huku Manchester City nayo ikiibuka na ushindi.
Vijana wa Gunners wakiwa uwanja wa nyumbani wa Emirates ilipatra ushindi huo ikitoka kulala mabao 2-0 dhidi ya Bayern Munich katika Ligi ya mabingwa wa Ulaya.
Mabao ya Oliver Giroud aliyefunga mawili katika dakika ya tano na 31 kabla ya Tomas Rosicky kufunga la tatu dakika ya 42 na kwenda mapumziko wakiongoza kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Arsenal kuongeza bao la nne likifungwa Laurent Koscielny katika dakika ya 57 na bao pekee la Sunderland likifungwa na Giaccherini'  katika dakika ya 81.
Ushindi huo umeifanya Arsenal kubaki nafasi ya pili nyuma ya Chelsea kwa tofauti ya pointi moja, Arsenal ikiwa na 59 na Chelsea 60 huku wakifuatiwa na Manchester City ilipata ushindi wa 1-0 nyumbani dhidi ya Stoke City.
Bao hilo pekee katika mchezo huo uliochezwa uwanja wa Etihad lilifungwa na Yaya Toure katika dakika yua 70.
Katika mechi nyingine Hull City imepata ushindi mnono ugenini kwa kuilaza Cardiff City mabao 4-0, huku West Bromwich ikilazimishwa sare ya 1-1 na Fulham waliotangulia kupata bao mapema.
Nayo West Ham United ikiwa nyumbani iliishindilia Southampton kwa mabao 3-1.
Mechi inayotarajiwa kuchezwa muda mfupi ujao ni kati ya mabingwa watetezi, Manchester United iliyopo ugenini dhidi ya Crystal Palace.

KILELE CHA MIAKA 10 YA ‘LADY IN RED’ KUFANYIKA NYUMBANI LOUNGE

* Kutolewa vyeti maalum
* Wadau kukata keki ya pamoja
* Slim kutumbuiza
https://thumbp4-ne1.mail.yahoo.com/tn?sid=2126005954&mid=AMJ2imIAABG1UwdzPAAAAA91Vj0&midoffset=2_0_0_1_1606779&partid=2&f=1214&fid=Inbox&w=3000&h=3000
 
Na Andrew Chale
KILELE cha Miaka 10  na ‘After Party’ ya onesho la mavazi la ‘Lady in Red Super Brand’  kinatarajia kufikia tamati usiku wa Jumamosi, Februari 22, ndani ya Ukumbi ulio na mgahawa wa kisasa na hadhi ya juu wa kwa jiji la Dar es Salaam, wa Nyumbani Lounge, huku kukitarajiwa kuwa na surprise mbali mbali kwa wadau watakaojitokeza.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Fabak Fashions,  Asia Idarous Khamsin, wandaaji wa Lady in red, kila mwaka hapa nchini, alisema, ‘after party’  hiyo ni maalum kwa ajili ya kutoa  shukrani na  vyeti maalum kwa wadau wanaoliunga  mkono jukwaa la Lady in red kwa kipindi chote hadi kufikia hapo ambapo pia watapata wasaha wa kukata keki  ya ukumbusho.
“After party ya miaka 10 ya Lady in red, kwa mwaka huu itakuwa ya aina yake sambamba na surprise, hivyo nyote munakaribishwa na hakuna kiingilio na kwa watakaokuwa tayari kujiunga siku maalum pale  Nyumbani Lounge, wafike  katika duka la Fabak Fashion, lililopo  jirani na kituo cha Msasani, Kwa Mwalimu Nyerere au kwa kupiga simu namba 0713263363  ama 0784263363” alisema Asia Idarous.
Na kuongeza kuwa, pia tiketi maalum za bure zitatolewa mlangoni Nyumbani Lounge, kwa wadau watakaofika. Aidha, alisema msanii wa muziki wa kizazi kipya, Slim Guapo Sosa anayetamba na kibao cha ‘ LOVE YOU ’ na vingine vingi anatarajiwa kuwakonga nyoyo watakaojitokeza kwenye ‘after party’ hiyo.
 Party hiyo imedhaminiwa na  wadhamini mbali mbali wakiwemo Times fm, Michuzi media group, mo blog, Nyumbani Lounge, Darling air, G one Media na wengine wengi.
Mwisho

Mtibwa Sugar yaona mwezi yainyuka Ashanti, Mgambo haikamatiki

Ashanti United waliyolazwa na Mtibwa Sugar
Mtibwa Sugar iliyoona mwezi
Oljoro JKT waliogeuzwa asusa na Mgambo mjini Arusha
Mgambo inayoendelea kugawa dozi kwa wapinzani wao katika Ligi Kuu
MABINGWA wa zamani wa kandanda nchini, Mtibwa Sugar leo imeona mwezi baada ya kupata ushindi wake wa kwanza katika mechi za duru la pili kwa kuinyoa Ashanti Utd wa mabao 2-1.
Mabao ya Mohammed Mkopi na Abdallah Juma ya kila kipindi yalitosha kuipa Mtibwa iliyokuwa uwanja wa nyumbani wa Manungu Complex pointi tatu muhimu vijana hao wa Mecky Mexime katika ligi hiyo inayozidi kuchanja mbuga.
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mussa hassan Mgosi, alilimwa kadi nyekundu katika mchezo huo kabla ya timu yake kupata bao la ushindi lililofungwa na Abdallah Juma.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Rhino Rangers ikisafiri ugenini kuumana na wenyeji wa Kagera Sugar walishindiliwa bao 1-0 lililoifungwa na Suleiman Kibuta katika dakika ya nne na kuzidi kujiweka pabaya kwenye janga la kushuka daraja.
Nao Mgambo JKT ambao kwenye duru la pili wameonekana kuamka waliendeleza ubabe wao kwa kuichapa Oljoro JKT nyumbani kwao kwa mabao 2-1, mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Chelsea yazidi kujikita kileleni yailaza Everton

Quick off the mark: John Terry reacts first as Slyvain Distin, Leighton Baines and Phil Jagielka can only watch
BAO la dakika ya lala salama lililofungwa na nahodha, John Terry limeiwezesha Chelsea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England, EPL, baada ya kupata ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Everton.
Terry alifunga bao hilo katika dakika ya tatu ya nyongeza ya mchezo huo uliochezwa 'darajani' ambao ulionekana kama ungeisha kwa sare na kuweka reheni nafasi ya timu hiyo kuendelea kuongoza msimamo.
Ushindi huo umeifanya Chelsea kufikisha jumla ya pointi  60 baada ya mechi 27, na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ambapo michezo mingine inaendelea jioni hii huku Arsenal ikiwa nyumbani inaongoza 3-0 mpaka sasa.

Yanga yaua Taifa, Mbeya City yafa Mkwakwani

Emmanuel Okwi akimtoka kipa wa Ruvu Abdallah Ramadhani na kuifungia Yanga bao la tatu (Picha: Francic Dande)


Coastal walioifanyizia Mbeya City Mkwakwani Tanga

Mbeya City waliopoteza mechi yao ya pili katika ligi msimu huu baada ya kuwa wagumua duru la kwanza
MABINGWA watetezi Yanga wametuma salamu na kujibu mapigo ya wapinzani wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri baada ya jioni hii kuinyuka Ruvu Shooting kwa mabao 7-0 jijini Dar es Salaam.
Yanga na Al Ahly zitavaana Jumamosi kwenye uwanja wa Taifa katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya kwanza huku Wamisri hao wakitoka kutwaa taji la Super Cup kwa kuilaza CS Sfexien ya Tunisia.
Al Ahly ilitoa kipigo cha mabao 3-2 kwa Watunisia wakishuhudiwa na kocha msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa aliyetumwa kwenda kuifanyia ushushushu ambaye alitua Taifa Yanga ikiua Ruvu.
Yanga iliyopiga kambi yake Bagamoyo iliisambaratisha Ruvu iliyo chini ya Mkenya, Tom Olaba kwa mabao ya haraka haraka ya kipindi cha kwanza kupitia kwa Didier Kavumbangu na Simon Msuva.
Wachezaji hao waliofunga mabao mawili kila mmoja katika mechi hiyo walifunga mabao hayo ndani ya dakika mbili tu za kuanza kwa mchezo huo kabla ya Mrisho Ngassa na Emmanuel Okwi kuongeza mengine mawili na kufanya waende mapumziko wakiongoza 4-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Yanga kuongeza bao la tano kupitia tena kwa Didier kabla ya Hamis Kiiza 'Diego' kuongeza jingine la sita dakika ya 69 na Msuva akamalizia kazi.
Kwa ushindi huo Yanga imerejea kileleni ikiing'oa Azam ambayo itashuka dimbani kesho dhidi ya Prisons kwa kufikisha pointi 38 na mabao 41 ya kufunga, huku Didier na Kiiza wakifikisha mabao 9.
Pia ushindi huo umeifanya Yanga kuweka rekodi ya kipigo kikubwa kutolewa msimu huu ikipiku vile vya Simba na Mgambo JKT na Prisons dhidi ya JKT Ruvu zilizoisha kwa mabao 6-0 kila moja.
Katika mechi nyingine iliyochezwa mjini Tanga, Mbeya City imekuwa urojo kwa Coastal Union kwa kulazwa mabao 2-0 kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Mabao ya washindi yamefungwa na Mohammed Miraji dakika nane za mwisho kabla ya kumalizika kwa pambano hilo na kuifanya Coastal kuwa timu ya pili kuidungua Mbeya City baada ya Yanga na kufikisha pointi 25.

Friday, February 21, 2014

Matokeo ya Kidato cha Nne 2013 yatangazwa

Kaimu Katibu Mkuu wa baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde akisoma matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2013 Dar es Salaam jana. 


Idadi ya ufaulu mtihani kidato cha nne mwaka jana  imeongezeka kutoka 185,940  hadi kufikia 235, 225, ikilinganishwa na mwaka 2012.
Vile vile watahiniwa 151,187 kati ya 404,083 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana wamepata ‘divisheni’ ziro.

Hata hivyo,  idadi ya waliopata daraja sifuri imepungua ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo wanafunzi 240,903 kati ya 397,132 waliambulia daraja hilo na kusababisha hamaki iliyoshinikiza viongozi wa sekta ya elimu kuwajibishwa.

Matokeo hayo yalitangazwa jana jijini Dar- es- Salaam na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la  Mitihani (Necta), Dk. Charles Msonde, aliyeongeza kuwa idadi ya ufaulu kwa mwaka jana ilipanda ikilinganishwa na mwaka 2012.

Ongezeko hilo la watahiniwa 49,285 waliofaulu zaidi mwaka huo, limefanya kiwango cha ufaulu kupanda kwa asilimia 58.25 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa  mwaka 2012.

“Jumla ya watahiniwa  404,083 sawa na asilimia 94. 48 waliofanya mtihani huo, wanafunzi 151,187 ambao ni  asilimia 42.91 walishindwa mtihani.” Alisema Dk. Msonde na kuongeza kuwa wasichana waliofaulu ni 106,792 sawa na asilimia 56.73,  wavulana ni 128,435 sawa na asilimia 59.58.

Watahiniwa  waliofaulu  moja kwa moja kutoka shuleni ni 201,152 sawa na asilimia 57.09, wasichana wakiwa 90,064 sawa na asilimia 55.49 na wavulana ni 111,088 sawa na asilimia 58.45.

Alisema idadi ya wanafunzi  wa kujitegemea ilikuwa   34,075 sawa na asilimia 66.23 ikilinganishwa na  ya mwaka 2012 ambao idadi yao ilikuwa 2,619.

Watahiniwa wa mtihani wa Maarifa(QT), waliofaulu ni 6,529 sawa na asilimia ikilinganisha na watahiniwa 5,984  wa  mwaka 2012.

Akitangaza matokeo hayo mbele ya wanahabari alisema watahiniwa  walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka jana walikuwa 427,679, kati yao wasichana ni  199,123 sawa na asilimia 46.56.

Wavulana walikuwa ni 228,556 sawa na asilimia 53.44, huku watahiniwa wa shule wakiwa 367,163 na watahiniwa wa kujitegemea wakiwa 60,516.

Alisema kati ya watahiniwa 427,679 waliosajiliwa kufanya mtihani huo, 404,083 sawa na asilimia 94.48 walifanya mtihani huo na watahiniwa 23,596 sawa na asilimia 5.52 hawakufanya mtihani huo.

Kwa watahiniwa wa shule 367,163 waliosajiliwa , 352,614 sawa na asilimia 96.04 walifanya mtihani, wasichana wakiwa 162,412 sawa na asilimia 96.07 na wavulana ni 190,202 sawa na asilimia 96.0.

Pia alisema watahiniwa 14,549 sawa na asilimia 3.96 hawakufanya mtihani.

Aidha aliongeza kuwa kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea 60,516 waliosajiliwa  kufanya mtihani huo, 51,469 sawa na asilimia 85.05 walifanya mtihani huo, na watahiniwa  9,047 sawa na asilimia 14.95 hawakufanya mtihani.

Alisema  kwa  watahiniwa  18,217 wa mtihani wa maarifa (QT),  waliosajiliwa, 15,061 sawa na asilimia 82.68 walifanya mtihani huo na 3,156 sawa na asilimia 17.32 hawakufanya mtihani.

Kwa upande wa ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja , alisema kwa watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 74,324 sawa na asilimia 21.09 wamefaulu katika daraja la I hadi la III wakiwamo wasichana 27,223 sawa na asilimia 16.77 na wavulana 47.101 sawa na asilimia 24.

Dk. Msonde alisema takwimu za matokeo zinaonyesha kuwa ufaulu katika masomo yote umepanda kwa asilimia kati ya 0.61 na 16.72 ikilinganishwa na mwaka 2012.

Alisema watahiniwa wamefaulu zaidi masomo ya Kiswahili kwa asilimia 67.77 na somo ambalo wamefaulu kwa kiwango cha chini ni Hesabu kwa asilimia 17.78.

Kwa mujibu wa Necta wanafunzi waliong’ara ni Robina Nicholaus, Sarafina Mariki, Abby Sembuche   na  Janeth Urassa  wa Sekondari ya Wasichana ya Marian.

Wengine ni  Magreth Kakoko na Angel Ngulumbi wa   St. Francis, Joyceline Marealle wa Sekondari ya  Canossa,   Sunday Mrutu  wa Sekondari ya Anne Marie,  Nelson Rugola na Emmanuel Mihuba Sekondari ya  Kaizirege .

Kadhalika, shule zilizofanya vizuri zaidi  na kuingia katika kumi bora  katika kundi la shule zenye watahiniwa 40 ni  shule ya wasichana ya St. Francis, Shule ya wavulana na Marian, shule ya wasichana ya Feza, shule ya Precious Blood, Canossa, Shule ya wasichana ya Marian, shule ya wasichana ya Anwarite, Abbey, Rosminini na Shule ya Seminari ya Don Bosco.

KUANGALIA MATOKEO YA MITIHANI


Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) uliofanyika Novemba 2013 unaweza kuyaona kwa  kubofya hapa MATOKEO

Golden Bush, Pugu Veterani kuonyeshana kazi kesho

Wazee wa 'dozi' Golden Bush Veterani
BAADA ya kimya cha muda mrefu, wakali wa soka la maveterani, Golden Bush kesho inatarajiwa kushuka dimba la Kines majira ya asubuhi kuvaana na wazee wenzao, Pugu Veterani katika mchezo wa kirafiki.
Golden Bush ambayo imekuwa ikiwasasambua wapinzani wao kwa vipigo kikubwa, mechi hiyo ya kesho dhidi ya Pugu ni kama marudiano kwani walishakutana mwishoni mwa mwaka jana na mchezo kushindwa kumalizika kutokana na kugotokea fujo, huku Pugu wakiwa wamepigwa kimoja.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Golden Bush, Onesmo Waziri 'Ticotico' katika pambano hilo wanatarajia kuwashikisha adabu wapinzani wao.
Ebu soma tambo wa wakali hao hapo chini mwenyewe;
Hi Wadau
 
Kwa muda mrefu kidogo nimekuwa kimya kwasababu ya majukumu ya kila siku ambayo kwa namna moja ama nyingine ilikuwa taabu kupata nafasi ya kuto matokeo huku ukizingatia kwamba timu yetu sasa hivi imekuwa ikitoa vipigo vya goli kuanzia 5 kwenda mbele. Ukipona sana 4.
 
Kesho vijana watukutu kutoka Pugu wakiongozwa machezaji mwenye maneno mengi Sele Thomas watakuwa wageni wetu katika uwanja wa St James Park, ikumbukwe game ya mwisho tuliwafunga goli moja lakini mpira uliisha dakika ya 88 pale walipoanzisha vurugu na kutuharibia game yetu. Kesho tumejipanga umpya ili kuhakikisha tunawakoma kwa kuwapa goli nyingi kama wenzao wa Stakishari walipigwa 6, Kigogo fresh 5, Mtongani 9, Mwanyamala 5 na wengine ambao siwakumbuki lakini wek kwenye akili yako kuwa walifungwa sichini ya goli 4 au 5.
 
Baada ya game hiyo huenda tukawapata ndugu zetu ambao tumewatafuta kwa muda mrefu sana, Survey Veterans siku ya jumapili inayofuata. Game hii itakuwa na umuhimi wa pekee kabisa kwasababu tunataka tuwapige goli za mwaka mzima ili wakikataa kucheza tunakuwa na hakiba ya ushindi kibindoni, hawa jamaa nina hamu nao Survey! We acha tu.
Njooni wewe, mjomba wako na shangazi yako uone football ya kesho kuanzia saa mbili kamili asubuhi

Twiga Stars, Zambia sasa kukipiga mapema

MECHI ya pili ya Raundi ya Kwanza kuwania Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Zambia (Shepolopolo) sasa itachezwa Februari 28 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam. Twiga Stars tayari ipo kambini kujiandaa kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni. Twiga Stars chini ya Kocha Rogasian Kaijage inafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Karume ambao ni wa nyasi za bandia kama ulivyo ule wa Azam Complex.
Shepolopolo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka.
Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuiondoa Shepolopolo itacheza na mshindi wa mechi kati ya Botswana na Zimbabwe. Zimbabwe ilishinda mechi ya kwanza ugenini.
Wachezaji wa Twiga Stars waliopo kambini ni Amina Ali, Anastazia Katunzi, Asha Rashid, Donisia Minja, Esther Chabruma, Etoe Mlenzi, Everine Sekikubo, Fatuma Issa, Fatuma Makusanya, Fatuma Mustafa, Fatuma Mwisendi, Fatuma Omari, Flora Kayanda, Happiness Mwaipaja, Maimuna Mkane, Mwajuma Abdallah, Mwapewa Mtumwa, Pulkeria Charaji, Sherida Boniface, Sophia Mwasikili, Therese Yona, Vumilia Maarifa na Zena Said.

Michuano ya kusaka vipaji kuanza kesho

MICHUANO ya mikoa katika mpango maalumu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuboresha Taifa Stars inaanza kutimua vumbi kesho (Februari 22 mwaka huu) kwa mechi nne.
Mechi rasmi ya ufunguzi wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa kati ya Ilala na Temeke. Mechi hiyo ya kundi G itachezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kuanzia saa 9.30 alasiri.
Kundi A kutakuwa na mechi kati ya Pwani na Morogoro kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi wakati Kusini Unguja na Kaskazini Unguja zitacheza kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung mjini Unguja katika kundi H.
Kusini Pemba na Kaskazini Pemba zitacheza mechi ya Kundi I katika Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.
Mechi za keshokutwa (Februari 23 mwaka huu) ni Simiyu itacheza na Shinyanga mjini Bariadi katika kundi E. Nayo Ruvuma itacheza na Njombe kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea katika kundi D.
Kundi C ni Tanga na Kilimanjaro kwenye Uwanja wa Mkwakwani wakati Kagera itacheza na Geita kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba katika kundi B. Mtwara itacheza na Lindi kwenye Uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara katika kundi F.
Wang’amuzi 40 wa vipaji tayari wamesharipoti kwenye vituo vya mechi hizo kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Yanga, Ruvu Shooting kesho kiama, mtanange wa Azam wapelekwa mbele

Yanga watakaovaana na Ruvu Shooting kesho
Azam baada ya kung'oka Kombe la Shirikisho wenyewe watashuka dimbani Jumapili badala ya kesho kama ratiba ilivyokuwa inaonyesha
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaingia Raundi ya 19 kesho (Februari 22 mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa katika miji ya Dar es Salaam, Bukoba, Morogoro, Tanga na Arusha.
Yanga itakuwa mgeni wa Ruvu Shooting ya mkoani Pwani katika mechi itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Nayo Kagera Sugar inaikaribisha Rhino Rangers ya Tabora katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Uwanja wa Manungu uliopo Turiani mkoani Morogoro ndiyo utakaotumika kwa mechi kati ya Mtibwa Sugar na Ashanti United, wakati Coastal Union itaumana na Mbeya City katika mechi itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv kutoka Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Maafande wa Oljoro JKT watakuwa nyumbani kupambana na Mgambo Shooting katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
Jumapili (Februari 23 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa ni Simba dhidi ya JKT Ruvu, mechi ambayo pia itaoneshwa moja kwa moja na Azam Tv.
Mechi kati ya Azam na Tanzania Prisons iliyokuwa ichezwe kesho (Februari 22 mwaka huu) Uwanja wa Chamazi sasa itachezwa Jumapili (Februari 23 mwaka huu) ambapo na itakuwa ‘live’.
Ligi hiyo itaendelea Jumatano (Februari 26 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Ashanti United na Azam itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex (Chamazi).