STRIKA
USILIKOSE
Sunday, July 31, 2011
Tamasha la Simba Day usipime!
BURUDANI mbalimbali za muziki na pambano la kirafiki la kimataifa litakaloihusisha wawakilishi wa Uganda kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika zinatarajiwa kupamba tamasha la soka la klabu ya Simba, 'Simba Day' litakalofanyika Agosti 8 jijini Dar es Salaam.
Wawakilishi hao wa Uganda, Simba Fc inayomilikiwa na Jeshi la nchi hiyo ndiyo watakaokuja kupamba tamasha hilo, ambalo pia litashuhudia timu ya Simba U23, ikikwaruzana na Azam katika kunogesha shamrashamra hizo.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliiambia MICHARAZO kuwa, tamasha lao litapambwa na burudani za muziki toka kwa bendi mbalimbali za muziki wa dansi na wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao hata hivyo hakuwataja.
Kamwaga alisema shamrashamra hizo za burudani ya muziki zitafuatiwa siku hiyo na utoaji wa tuzo za heshima kwa wadau wa Simba wakiwemo wachezaji, makocha na viongozi wa zamani walioisaidia klabu yao tangu ilipoanzishwa pamoja na wale wanaoisaidia sasa klabu hiyo.
"Karibu kila kitu kimekaa vema kwa sasa ikiwemo kuthibitishwa kwa Simba ya Uganda kuja nchini kucheza nasi katika tamasha hilo, ambalo kabla ya pambano hilo kutakuwa na burudani za muziki na pambano la timu za vijana za Simba na Azam," alisema Kamwaga.
"Mbali na burudani hizo pia tutatoa tuzo za heshima kwa wadau wetu katika namna ya kukumbuka na kushukuru mchango wao," alisema Kamwaga.
Kuhusu maandalizi yao ya mechi yao ya Ngao ya Hisani iliyoapngwa kucheza Agosti 17, Kamwaga alisema yanaendelea vema ikiwemo kikosi chao kuendelea kujifua kwa mazoezi pamoja na kucheza kadhaa za kirafiki visiwani Zanzibar.
Alisema wana imani kubwa ya kufanya vema kwenye pambano hilo dhidi ya Yanga pamoja na kwenye msimu mpya wa ligi kuu utakaoanza wiki moja baada ya pambano hilo la Ngao ya Hisani.
Simba ina deni la kulipa kisasi kwa Yanga iliyowafunga kwenye mechi kama hiyo msimu uliopita kwa mikwaju ya penati na kipigo ilichopata kwenye fainali za Kombe la Kagame lililochezwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam ambapo Mghana Kenneth Asamoah waliwaliza.
"Hatuna shaka na mechi zetu zijazo kutokana na maandalizi tuliyofanya huko Zanzibar," alisema Kamwaga aliyechukua nafasi hiyo hivi karibuni akimrithi, Clifford Ndimbo.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment