STRIKA
USILIKOSE
Sunday, July 31, 2011
Uongozi wakana kumpa Nyagawa umeneja Simba
UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba umekanusha taarifa kwamba umempa cheo cha umeneja kiungo wake iliyomtema kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania, Nico Nyagawa.
Nyagawa, aliyekuwa nahodha wa klabu hiyo ametemwa kwenye usajili wa kikosi kipya kitakachoitumikia timu hiyo msimu ujao, huku kukiwepo na taarifa kwamba kiungo huyo amekula shavu la kuteuliwa kuwa meneja wa timu hiyo.
Klabu ya Simba kupitria Afisa Habari wake, Ezekiel Kamwaga, alikanusha madai hayo ya kumpa Nyagawa umeneja, akisema cheo hicho bado kipo kwa King Abdallah Kibadeni, licha ya kukiri ni kweli wamemuacha mchezaji huyo kwa msimu ujao.
"Nyagawa hajapewa umeneja, ingawa ni kweli ametemwa kwenye orodha mpya ya kikosi cha Simba kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara," alisema Kamwaga.
Alisema kwa sasa uongozi wao unaangalia namna ya kumpa kazi nahodha wao huyo, kwa vile bado anaye mkataba na klabu hiyo hadi mwakani.
Alipoulizwa madai kwamba mchezaji huyo amekuwa akitaka kulipwa haki zake ili atimke zake kimoja Msimbazi, Kamwaga alisema hizo ni taarifa za uzushi kwa vile Nyagawa mwenyewe hajawahi kuueleza chochote uongozi juu ya jambo hilo hadi alipoongea na Sema Usikike.
"Hizo ni taarifa za uzushi tu, tulishazungumza na Nyagawa na ndio maana tunasema tupo katika mipango ya kumpa majukumu ndani ya Simba, " alisema.
Nyagawa aliyesajiliwa na Simba msimu wa 2005-2006 akitokea Mtibwa Sugar anatajwa kama mmoja wa wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu wa soka nchini, ingawa amekuwa na bahati mbaya ya kutoitwa mara kwa mara katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment