STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, July 31, 2011

Pondamali awachanganya Villa Squad

UONGOZI wa klabu ya soka ya Villa Squad, umedai kuchanganywa na kitendo cha aliyekuwa kocha wao, Juma Pondamali kujiondoa kikosi, huku wakikanusha kumteua Rachel Mwiligwa kuwa msemaji mpya wa klabu yao.
Makamu Mwenyekiti wa Villa, Ramadhani Uledi, aliambia MICHARAZO juzi kuwa, kujiondoa kwa Pondamali kumewapa wakati mgumu kutokana na ukweli alikuwa sehemu ya mipango yao ya kuisaidia timu hiyo kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Uledi alisema kinachowachanganya zaidi ni hatua ya kocha huyo aliyekuwa pia Mkurugenzi wa Ufundi, kuondoka kimyakimya bila kuwaambia zaidi ya kusoma taarifa zake kwenye vyombo vya habari.
"Tumeshtushwa na kuchanganywa na Pondamali kujiondoa tukielekea kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara tuliyoirejea msimu huu, hatujui kitu gani kilichomkimbiza, ila kutakutana kujadili tuone tunafanyaje," alisema.
Uledi anayekaimu pia nafasi ya Mwenyekiti, ambayo ipo wazi baada ya TFF kusitisha kuwaniwa kwenye uchaguzi mkuu wa klabu hiyo uliofanyika Juni, mwaka huu, alisema pia sio kweli kama klabu yao imemteua Mwandishi Rachel Mwiligwa kuwa Msemaji wao, akisisitiza nafasi hiyo bado inashikiliwa na Idd Godigodi aliyetangaza kujiuzulu.
"Hatutateua msemaji mpya kwa kuwa nafasi hiyo na zile zinazotakiwa zitolewe kwa ajira rasmi, zitatangazwa baada ya kikao chetu, kwa maana hiyo Godigodi aliyetangaza kujiondoa baada ya kusoma taarifa za uteuzi wa Mwiligwa ataendelea na nafasi yake," alisema Uledi.
Mwenyekiti huyo aliongeza katika kikao chao watajadili suala la ushiriki wa timu yao katika msimu mpya wa ligi waliorejea baada ya kushuka msimu wa 2008-2009.
Villa Squad ni miongoni mwa timu nne 'mpya' zitakazocheza ligi ya msimu ujao iliyopangwa kuanza Agosti 20, zingine zikiwa ni JKT Oljoro, Coastal Union na Moro United.

Mwisho

No comments:

Post a Comment