STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, July 31, 2011

Waumini Answar Sunna wacharuka, watulizwa na RITA

WAUMINI wa Jumuiya ya Answar Sunna Tanzania wanaoshinikiza uongozi wa juu ya jumuiya hiyo hung'oke madarakani kwa kukiuka katiba, wametulizwa wakitakiwa kuwa na subira wakati ofisi wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini, RITA ukisubiri kutoa maamuzi juu ya mgogoro huo.
Wito huo umetolewa jana kwenye maazimio ya mkutano wa pamoja kati ya waumini hao na kamati yao maalum inayofuatilia mgogoro huo, uliofanyika kwenye msikiti uliopo makao makuu ya Answar Sunna, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kadhalika wito kama huo umetolewa na Meneja wa Ufilisi na Udhamini wa Rita, Linna Msanga Katema, alipozungumza na MICHARAZO akithibitisha ofisi yao imeomba ipewe muda wa mwezi mmoja kutoa majibu juu ya sakata linaloendelea kwenye jumuiya hiyo.
Meneja huyo alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kueleza tofauti na awali walipokuwa wakikosa ushirikiano toka kwa viongozi wanaolalamikiwa wakiwemo Baraza la Wadhamini na Amiri wa Jumuiya hiyo, Sheikh Juma Poli, sasa mambo ni shwari.
"Tumeshawaandikia barua kuomba watupe muda wa mwezi mmoja toka Julai 26 tuliowaandikia barua ili RITA tutoe maamuzi juu ya kinachoendelea baina ya pande hizo mbili, hivyo tunaomba waumini watulie haki itatendeka," alisema Katema.
Katika mkutano wao wa jana, waumini hao walionyesha kuwa na hasira ya kutaka viongozi wang'oke kwa kukiuka katika na kushindwa kuipeleka mbele jumuiya yao, kabla ya Mwenyekiti wa Kamati yao, Hamis Buguza kuwasihi wavute subira.
"Vuteni subira tusubiri maamuzi ya RITA ili kuona nini kitaamuliwa, ila lolote litakalotolewa tunawaahidi kuyaleta kwenu mjue kitu cha kufanya, ila kwa sasa ni mapema mno na Uislam unatufundisha kuwa na subira," alisema mwenyekiti huyo.
Kutokana na kauli ya Mwenyekiti pamoja na Katibu wao, Abdulhafidh Nahoda, waumini hao katika kutoa maazimio waliafiki kuvuta subira hadi maamuzi ya RITA yanayotarajiwa kutolewa Agosti 26, ili wajue la kufanya.
Hata hivyo walitoa angalizo kwa kudai kama kutakuwa na aina fulani ya upendeleo basi, watakachoamua wasije wakaamuliwa kwa madai wamechoka kuvumilia.
Mzozo wa waumini wa jumuiya hiyo na uongozi wao umeanza tangu mwaka juzi kutokana na madai viongozi wamekiuka katiba kwa kutoitisha mikutano kwa muda wa miaka 10, huku wakifanya maamuzi bila kuwashirikisha kama wanavyoelekezwa kwenye katika mama ya mwaka 1992.

Mwisho

No comments:

Post a Comment