MSHAMBULIAJI mpya wa timu ya Coastal Union ya Tanga, Ben Mwalala 'amerejeshwa' kwa nchini Kenya, baada ya timu yake iliyorejea Ligi Kuu Tanzania Bara, kuamua kupiga kambi ya kudumu nchini humo.
Coastal iliyowahi kuwa mabingwa wa soka nchini mwaka 1988, imeamua kuweka kambi ya kudumu mjini Mombasa, kujiandaa na msimu mpya wa ligi utakaoanza mwezi ujao hali inayowafanya nyota wao wapya Mwalala na mkenya mwenzie Abubakar Husseni kurejea kwao.
Afisa Habari wa timu hiyo, Eddo Kumwembe, alisema uongozi wao umeamua kuweka kambi ya kudumu Kenya, ikicheza mechi kadhaa za kirafiki za kujipima nguvu kujiweka fiti kabla ya kuanza kwa mikikimikiki ya ligi iliyokuwa ianze rasmi Agosti 20.
Kumwembe, alisema awali walikuwa wamepanga kurejea kwa muda Tanzania kwa ajili ya kuja kucheza pambano la kirafiki na Yanga lililokuwa lichezwe jana, lakini kutokana na uongozi wa Jangwani 'kuchomoa' kucheza nao wameamua kusalia Kenya hadi msimu utakapoanza.
"Kutokana na Yanga kuchomoa kucheza na sisi, tumeamua kubaki Kenya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kwa kujipima nguvu na timu za huko," alisema.
Coastal inayonolewa na kocha Hafidh Badru, imefanya usajili unaoonekena wa kutisha kwa kuwajaza nyota wa kigeni kama Mwalala, Husseni na wanigeria wawili, Felix Amechi na Samuel Temi huku ikiwa na nyota wengine wa Tanzania akiwemo Aziz Salum Gilla aliyetoka Simba.
Mwisho
No comments:
Post a Comment