STRIKA
USILIKOSE
Monday, June 25, 2012
Ngassa atamani kucheza Simba
ACHANA na Mrisho Ngassa. Mshambuliaji nyota wa timu ya Moro United iliyoshuka kwenye ligi kuu ya Bara, Benedict Ngassa, amesema anatamani kuichezea Simba.
Kama hatopata nafasi ya kucheza Simba, mabingwa wa mwaka jana, Ngassa amesema anatamani kusajiliwa Yanga.
Akizungumza na MICHARAZO, Ngassa, alisema kati ya ndoto anazoota kila siku ni ile ya kuja kuichezea ama Simba au Yanga, klabu anazozihusudu na anazoamini zitaweza kumfikisha mbali kisoka.
Ngassa, alisema yeye hatakuwa mchezaji wa kwanza nchini kuziota timu hizo kubwa, ingawa alisema ni vigumu kupata fursa hiyo kirahisi kama hufanyi vitu vya kuzivutia.
"Kwa kweli natamani kuichezea timu moja kati ya Simba au Yanga, ni klabu kubwa na zenye mafanikio makubwa nchini na zinazoweza kumfikisha mbali mchezaji kama ana malengo na kila kijana anatamani kuzichezea," alisema.
Ngassa, alisema mpaka sasa wakati usajili ukiendelea bado hajasaini kokote licha ya kufuatwa na timu kadhaa.
Ngassa ni mmoja wa nyota wa timu ya Moro iliyokuwa imerejea ligi kuu na kushuka msimu uliopita sambamba na Villa Squad na Polisi Dodoma.
Nafasi za timu hizo tatu, mbili zikiwa za uraiani, zimechukuliwa na Mgambo Shooting, Polisi Moro na Mbeya Prisons.
Niombeeni kwa Mungu, naumwa-Omar Kapera 'Mwamba'
Kapera (wa tatu kushoto waliochuchumaa) akiwa na wachezaji wenzake wa Yanga |
Hassani Kumbi: Kiungo mkabaji anayetesa na miondoko ya Mduara
AWALI ndoto zake tangu akiwa shuleni ilikuwa kuja kuwa nyota wa soka akimudu nafasi ya kiungo mkabaji na nafasi nyingine za mbele akitamba na timu kadhaa ikiwemo Ajax Mzamba ya Temeke alioshiriki nao Ligi ya Taifa.
Hata hivyo kitendo cha kupigwa bisibisi katika mechi ya 'mchangani' ya Ligi ya kuwania Ng'ombe, Kiwalani, lilisitisha ndoto za Hassani Kumbi ' H-Kumbi au 'H-Kilakitu' na kujikuta akihamia kwenye fani ya muziki.
Kumbi, alisema baba yake alimpiga marufuku kucheza soka baada ya tukio hilo lilomfanya alazwe hospitalini na alipopona aliamua kuingia katika muziki kwa vile alishawahi kuimba kaswida alipokuwa madrasa.
Msanii huyo anayetamba baada ya kuibuliwa na kituo cha Mkubwa na Wanae kinachoendeshwa na Said Fella, alisema alipigwa bisibisi hiyo mbavuni na mmoja wa mashabiki wa timu pinzani iliyocheza na timu yake ya Young Stars.
"Baba alinizuia kucheza soka baada ya kitendo cha kujeruhiwa uwanjani ndipo nikahamishia makali yangu kwenye muziki baada ya kupita usaili wa Mkubwa na Wanae," alisema.
Kumbi alisema baadhi ya nyota aliocheza nao shuleni na kwenye timu kadhaa ni Abuu Ubwa, Nizar Khalfan, Adam Kingwande, Ramadhani Chombo, Juma Jabu na Ally Mustafa 'Barthez'.
Mkali huyo anayetamba kwa sasa na kibao cha 'Vocha' alichoimba na Dogo Aslay waliopo naye kituo cha Mkubwa na Wanae, alisema licha ya kuimba kaswida, pia aliwapenda mno Banzastone na Zahiri Ally Zorro.
"Nilivutiwa na Banzastone na Zahir Ally ambao hata leo wanawafuatilia ndio maana nimeweza kuinuka haraka kisanii," alisema.
Msanii huyo, anayetarajia kuachia kazi mpya iitwayo 'Sindano' akiwa na video yake huku akikamilisha pia kibao cha Deni alichoimba na AT, alisema muziki kwa sasa nchini unalipa na una mafanikio makubwa.
Alisema zamani ilikuwa vigumu msanii wa muziki wa kizazi kipya kuandaa shoo ya kiingilio cha Sh 20,000 au 50,000 lakini sasa inawezekana akitolea mfano tukio la Diamond alipofanya onyesho lake la 'Diamond Are Forever'.
Kumbi, anayetamani kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa mara 'kijiwe' cha muziki kitakampomchanganyia, alisema licha ya muziki kulipa bado vipo vikwazo ikiwemo uharamia na unyonyaji unaofanywa dhidi ya kazi za wasanii.
Alisema ni vema serikali ikawasaidia wasanii kwa kutunga sheria kali ili kuwatia adabu wezi wa kazi za wasanii, sambamba na kuvuna mapato yaliyopo katika fani hiyo, akidai fedha nyingi zinapotea mikononi mwa 'wahuni'.
Msanii huyo anayependa kula wali kwa maharage au ugali kwa samaki wa kukangaa na mlenda pamoja na kunywa juisi ya Embe, alisema kama angekutana na Rais angemweleza jambo hilo sambamba na kumsihi aboreshe maisha ya watanzania hasa huduma za kijamii na kudhibiti mfumuko mkubwa wa bei za vyakula na bidhaa nyingine.
Kumbi anayeishabikia Simba na Manchester United na kuwazimia wachezaji nyota wa timu hizo, Haruna Moshi 'Boban' na Javier Hernandez 'Chicharito', alisema kati ya matukio ya furaha kwake ni kukubalika kwa kazi yake ya kwanza ya 'Vocha' na pia kukutana kwa mara ya kwanza na kuzungumza na Zahir Ally Zorro anayemhusudu na kumsifia uwezo alionao.
"Nilisisimka mno nilipokutana uso kwa uso na Zahir Ally na kujisikia faraja aliponieleza kwamba naweza, pia nilipoachia kazi yangu ya Vocha na kupokelewa vema na kwa huzuni ni msiba wa baba yangu Ally Kumbi na kuuguliwa na mama yangu hadi leo," alisema Kumbi.
Mkali huyo aliyeoana na Aisha Soud na kuzaa nae mtoto mmoja aitwae Hawa (2), alisema matarajio yake ni kuhakikisha anafika mbali katika muziki, pia akiweka wazi kwamba yeye ni H Kila Kitu akimaanisha anaimba miondoko yote ya muziki ikiwemo taarab na dansi.
Kumbi anayemshukuru Mungu na watu waliomsaidia katika muziki kama Said Fella, Yusuf Chambuso, Suleiman Daud 'Sulesh' na wasanii wenzake wa Mkubwa na Wanae, alisema kitu cha thamani anachokumbuka kununua kwa fedha zake za muziki ni kumuugizia mwanae.
"Nakumbuka nilienda kufanya shoo Iringa na kupata fedha nyingi kwa mara ya kwanza katika maisha yangu bya muziki na niliporejaea Dar nilikuwa mwanangu Hawa mgonjwa hivyo nikatumia kumtibia pamoja na kumnunulia nguo za bei mbaya," alisema.
Msanii mwenye ndoto za kuja kujitolea kuwasaidia wengine kama anavyofanya Mkubwa Fella, alitoa ushauri kwa watu matajiri kuwasaidia wasanii kuwaibua na kuwaendeleza badala ya kusubiri watu wengine wawaibue kisha kuwarubuni wasanii hao bila kujua walikotokea.
"Wapo watu wenye fedha zao wamekuwa wakifanya hila kuwarubuni wasanii chipukizi baada ya kuona wameanza kutoka kwa kuinuliwa na watu kama THT, Mkubwa na Wanae au Tip Top Connection, hii sio haki kwanini wasitumie fedha zao kufanya kama wenzao?" Alihoji.
Hassani Ally Kumbi, alizaliwa Juni 16, 1987 akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto wanne na kusoma Shule ya Msingi Mabatini -Tandika Dar es Salaam kabla ya kuendelea na masomo ya Sekondari alipohitimu kidato cha nne mwaka 2006 Shule ya Twaybat pia ya Temeke.
Alienda kusomea ufundi umeme wa magari mjini Morogoro kabla ya kuzama kwenye soka aliloanza kucheza tangu akisoma shule ya msingi, timu yake ya chandimu ikiwa ni Santiago Chile maarufu kama G Stiva akimudu namba 6 na nyingine zote za mbele.
Timu nyingine alizozichezea kabla ya kutua kwenye muziki ni Good Hope, TMK Kids, DYOC na Ajax Mzamba aliyoitoa daraja la tatu hadi Ligi ya Taifa ya TFF.
Mwisho
Kingwendu ajipanga kuachana na soka, kisa...!
MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya African Lyon aliyewahi kutamba na timu za Ashanti Utd na Simba, Adam Kingwande amesema anatarajiwa kupumzika kwa muda kucheza soka ili arejee darasani kusoma.
Kingwande, aliiambia MICHARAZO kama mipango yake ya kwenda darasani itatimia hivi karibuni, basi huenda asionekane tena dimbani hadi atakapomaliza masomo yake baada yaa miaka mitatu.
Mchezaji huyo aliyekuwa msaada mkubwa kwa Lyon kabla ya kuumia na kuwa nje ya dimba hadi aliporejea mwishoni mwa msimu uliopita, alisema ameona ni bora arejee darasani kusoma kisha ndipo aendelee kucheza soka.
Kingwande alisema anatarajia kwenda kusomea Sheria katika Chuo kimoja kilichopo hapa nchini na hivyo itamuwia vigumu kwake kuchanganya mambo mawili kwa wakati mmoja.
"Kaka huenda nisionekane tena dimbani kwa muda kidogo kwani natarajia kurudi darasani kusoma, si unajua soka la Bongo lilivyo kama mtu hujiwekei mipango mizuri unaweza kuumbuka mbeleni," alisema.
Mkali huyo, aliyeibuliwa na kituo cha kukuza soka la vijana cha DYOC, alisema masomo yake yatachukua muda wa miaka mitatu na hivyo kipindi chote cha masomo hayo hataweza kucheza timu yoyote labda ya chuoni tu.
Kingwande alisema mbali na chuo hicho, pia ameomba nafasi ya kusoma pia katika chuo kimoja kilichopo nje ya nchi hivyo anasikilizia kama akikubaliwa anaweza kuamua kujiunga na chuo kimojawapo kati ya hivyo.
"Nimeomba pia katika chuo kimoja nje ya nchi, lakini ningependa kusoma hapa nchini, mradi tu nitimize ndoto zangu za kuwa mwanasheria," alisema.
Mchezaji huyo anayemudu nafasi zote za mbele ikiwemo kiungo alisema anaamini kusoma kutamwezesha kulicheza soka lake kwa uhakika sambamba na kuwa na uhakika wa maisha baada ya kutundika daluga zake.
Mwisho
Theresia Ojade, mshindi wa tuzo ya TASWA anaizimia Simba
MWENYEWE anakiri kuwa kiu aliyokuwa nayo tangu utotoni ya kutaka kuwa nyota wa michezo nchini, ndiyo iliyomfanya ajibidiishe, kujituma na kujifunza kwa wengine waliomtangulia na katika kipindi kifupi ameanza kuona matunda yake bila ya kutarajia.
Moja ya matunda yanayomfanya mchezaji huyo mkali wa timu ya mpira wa wavu ya Jeshi Stars, Theresia Ojade kujivunia ni Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike wa Wavu aliyotwaa iliyotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini, TASWA.
Theresia, alisema tuzo hiyo ambayo hakutarajia kuipata licha ya kuwa mmoja wa nyota watatu walioteuliwa kuiwania sambamba na mchezaji wenzake wa Jeshi Stars, Zuhura Hassani na Evelyne Albert wa Magereza, imempa faraja kubwa na kumtia nguvu ya kujibidiisha zaidi.
Mkali huyo aliyeanza kung'ara katika michezo tangu akisoma Shule ya Msingi
akicheza netiboli, wavu na kikapu, alisema hakutarajia kama ndoto zake za kung'ara katika michezo zingeanza kutimia mapema kiasi hicho.
"Kwa kweli namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuanza kutimiza ndoto zangu za utotoni za kutamba katika michezo baada ya kutwaa tuzo ya TASWA," alisema.
Aliongeza tuzo hiyo haimvimbishi kichwa badala yake imemuongezea morali wa kuongeza juhudi ili aje kutamba kimataifa ikiwezekana kucheza mpira wa wavu wa kulipwa kama nyota wa nchi jirani za Rwanda na Kenya.
"Natamani nifike mbali katika mchezo huu, hasa kucheza wavu wa kulipwa sambamba na kuisaidia timu yangu ya Jeshi Stars itambe kimataifa," alisema.
MAFANIKIO
Theresia, aliyeingia kwenye wavu kwa kuvutiwa na umahiri wa dada yake, Maria Daniel na Fausta Paul aliyestaafu kwa sasa, alisema mbali na heshima ya tuzo hiyo na kitita cha Sh. Mil. Moja, pia anashukuru wavu kumsaidia mengi.
Alisema, mchezo huo umemfanya hafahamike, kutembea sehemu mbalimbali na kumwezesha kumudu maisha yake na kuisaidia familia yake licha ya kupata mafunzo ya kijeshi kama askariu wa kujitolea wa JKT.
"Japo mchezo huu haulipi sana nchini kutokana na kutopewa kipaumbele na kudodora kwake, ukweli umenisaidia kwa mengi kiasi najivunia kuucheza," alisema.
Alidokeza kuzimika kwa mchezo huo nchini kumechangiwa na Chama chao cha TAVA kukosa ubunifu na kuandaa mashindano mara kwa mara kuuhamaisha mchezo huo na kuutaka uongozi wake kuzinduka usingizini.
Theresia alisema, pia 'ubaguzi' unaofanywa na serikali na wadhamini kwa kutupia macho soka tu, ni tatizo linalodidimiza wavu na michezo mingine na kudai angekutana na Rais angemlilia atupie macho michezo yote ili kuwasaidia wenye vipaji kunufaika nayo.
"Ningemuomba Rais aitupie na kuiwezesha michezo mingine ili tunayoicheza tunufaike nayo kama kwa wanasoka na kama ningekuwa Rais ningewekeza katika michezo sambamba na kuboresha huduma za kijamii hasa Afya na Elimu," alisema.
FURAHA
Nyota huyo anayependa kula ugali kwa samaki na kunywa juisi ya Embe, alisema hakuna kitu cha furaha kwake kama kutwaa tuzo hiyo ya TASWA na kuhuzunishwa na kifo cha mjomba wake kipenzi, Ojade aliyefariki mwaka jana.
Theresia aliyejaliwa umbo la kike na sura ya kuvutia, alisema licha ya kucheza mechi nyingi, hawezi kuisahau pambano kati ya Jeshi Stars dhidi ya Prisons ya Kenya katika fainali za michuano ya ubingwa wa nchi za Afrika Mashariki.
"Naikumbuka kwa namna wapinzani wetu walivyotuzidi maarifa na namna tulivyocheza na kuambulia kipigo cha aibu cha seti 3-0," alisema.
Theresia ambaye hajaolewa wala kuzaa mtoto, akitamani atakapoolewa awe na watoto watatu, ni shabiki mkubwa wa Simba na Manchester United akimzimia mchezaji mwenzake wa Jeshi Stars, Yasinta Remmy.
Mkali huyo anayechishwa na nguo za rangi nyeupe na nyeusi na kupenda kutumia muda wake wa mapumziko kusikiliza muziki na kufuatilia maambo ya urembo na mitindo, aliwashukuru familia yake hasa wazazi, dada yake Maria Daniel na marehemu mjomba wake Ojade.
ALIPOTOKA
Theresia Sylvanus Abwao Ojade, alizaliwa Januari 8, 1988 Shirati mkoani Mara akiwa ni mtoto wa kwanza kati ya wawili wa familia yao.
Alisoma Shule ya Msingi Mbagala Kuu jijini Dar kabla ya kujiunga na masomo ya Sekondari katika Shule ya Mwanga na kukwamia kidato cha pili kutokana na matatizo ya kifamilia na kujikita katika michezo aliyoicheza tangu kinda.
Klabu yake ya kwanza kujiunga kuichezea ni JKT Mgulani alipokuwa mmoja wa askari wa kujitolea wa Jeshi la Kujenga Taifa kwa mkataba wa miaka mitatu.
Baada ya kung'ara na timu hiyo na kumalizika kwa mkataba wake alijiunga na Jeshi Stars mwaka juzi na kufanikiwa kutwaa nao mataji mbalimbali ukiwemo ubingwa wa Ligi ya Muungano wa mwaka huu.
Theresia anayewazimia wasanii Lady Jaydee na Ally Kiba wanaotamba katika muziki nchini, alisema atakuwa mchoyo wa fadhila kama hatawashukuru wachezaji wenzake na makocha waliomnoa na kumfikisha hapo alipo.
Mwanadada huyo alikiri kwamba amekuwa akipata usumbufu mkubwa kwa wanaume wakware, lakini kwa kujithamini na kutambua kuwa Ukimwi upo na unaua huepuka vishawishi jambo alilotaka wachezaji wenzake na jamii kwa ujumla nao kuwa makini kwa kuepuka tamaa.
Pia aliwasihi wachezaji wenzake kupendana, kushirikiana na kujibidiisha na kujituma katika mazoezi na michuano mbalimbali ili wafike mbali.
Mwisho
Tuesday, June 19, 2012
Waislam wadai hawahitaji upendeleo serikali, ila...!
AMIRI wa Vijana wa Dini ya Kiislam Tanzania, Sheikh Shaaban Mapeyo, amesema malalamiko wanayotoa waumini wa dini hiyo dhidi ya serikali haina maana ya waislam kutaka upendeleo bali kutaka haki na uadilifu utendwe kwa raia wote nchini.
Aidha alisisitiza kuwa msimamo wa viongozi wa dini hiyo juu ya Sensa ya mwaka huu ni ule ule wa kuigomea mpaka kipengele cha dini kilichoondolewa kirejeshwe ili kuondoa utata uliopo na kusaidia kujua idadi ya wanadini nchini.
Akiwahutubia waumini wa msikiti wa Mwenge, jijini Dar es Salaam, Sheikh Mapeyo ambye pi ni Imamu Mkuu wa msikiti huo, alisema waislam hawahitaji upendeleo wa aina yoyote, isipokuwa wanapenda kuona haki na uadilifu unatendwa kwa raia wote.
Sheikh Mapeyo alisema madai wanayoyatoa kila mara dhidi ya dhuluma na hujuma wanaofanyiwa ni kama njia ya kuikumbusha serikali ifanye shughuli zake kwa uadilifu ikiwatendea haki raia wake wote badala ya kupendelea kundi fulani na kuwapuuza wengine.
"Waislam tunapolalamika na kupiga kelele kila mara hatuna maana ya kutaka upendeleo, tunachotaka ni kuona serikali inaendesha shughuli zake za usawa, haki na uadilifu kwa vile taifa hili ni la watanzania wote," alisema.
Aliongeza, waislam wamekuwa wavumilivu kwa muda mrefu nchini licha ya kutambua kuna baadhi ya mambo hawatendewi haki, lakini kwa kupuuzwa kwao imewafanya wafikie kikomo na kuitahadharisha serikali iwe makini.
"Kwa mfano kwa muda mrefu tumekuwa tukilalamika hujuma tunayofanyiwa katika elimu, ila majuzi imebainika hatulii ovyo baada ya kubainika madudu ya matokeo ya Baraza la Taifa la Mitihani, ambapo wenyewe wamekiri makosa."
Alisema ni vema serikali ikazinduka na kuliona tatizo lililopo nchini ni kubwa kuliko wanavyofikiria, huku akisisitiza kuwa bila kuyrejeshwa kwa kipengele cha dini kwenye zoezi la Sensa waislam hawatashiriki.
"Huu ni msimamo wetu na tumeanza kuwahimiza waumini wetu kuwa kama kipengele hicho hakirejeshwi basi wasishiriki Sensa na tumeshaiandikia barua serikali juu ya msimamo huo," alisema Sheikh Mapeyo.
Alisema serikali iliwaita viongozi wa kidini mjini Dodoma kuzungumzia jambo hilo na kusisitiza hawaterejesha kipengele hicho na wao kuieleza wazi kwamba kama ni hivyo basi wapo radhi wahesabiwe watu wengine na sio waislam.
Mwisho
Mcheza filamu wa Marekani kukimbia Mount Kilimanjaro
MCHEZA sinema maarufu duniani kutoka nchini Marekani Deidre Lorenz, anatarajiwa kushiriki mbio za kila mwaka za Mount Kilimanjaro Marathon zitakazofanyika Jumapili ijayo mjini Moshi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na waratibu wa mbio hizo zilizoanzishwa na Marie France wa mji wa Bethesda, Maryland nchini Marekani mwaka 1991 na zitakazojulikana kama 7 Continental Races, muigizaji huyo wa filamu naye atakimbia katika mbio hizo.
Taarifa hiyo iliyotumwa MICHARAZO na Afisa Habari Uhusiano wa mbio hizo, Grace Soka ni kwamba mcheza sinema huyu aliyecheza sinema kama Santorini Blue, Perfect Strangers, The Great Fight, ujio wake utaitangaza Tanzania katika macho ya dunia na kuwavutia watalii.
Lorenz aliyewahi kuteuliwa mara tatu kuwania tuzo za Grammy, ataambana na wamarekani wengine na anatarajiwa kutua nchini Juni 21.
Mbio hizo za Mount Kilimanajaro zitawashirikisha wakimbiaji wengine wa kimataifa pamoja na wa nyumbani na zitakuwa za umbali wa Kilomita 42 na washindi wake wakiwemo watoto watazawadiwa zawadi mbalimbali.
Pia mbizo zitahusisha mbio za umabli wa kilometa 21, kilometa 10 na kilometa 5 kwa watoto na kwamba washiriki wake hawahitaji ujuzi wa kukimbia bali mradi mtu anayeweza kufanya hivyo.
Deidre Lorenz alizaliwa katika jiji la Oregon nchini Marekani lakini alihamia katika jiji la New York City linalijulikana kama "The Big Apple" nchini Marekani akiwa na kampuni yake ya kutengeneza sinema inayoitwa Thira Films LLS.
Lorenz alipatikana kushiriki mbio hizo katika bahati nasibu iliyochezwa wakati wa mbio za New York Marathon za mwaka jana.
Coastal Union yanasa vifaa vipya yumo Atupele
KLABU ya soka ya Coastal Union ya Tanga, imetangaza kuwanyakua wachezaji kadhaa wapya akiwemo kipa wa zamani wa Yanga na Azam, Jackson Chove.
Afisa Habari wa Coastal, Eddo Kumwembe, aliiambia MICHARAZO,
Chove ni miongoni mwa makipa wawili wapya iliyowasajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kumwembe alimtaja kipa mwingine iliyomnyakua ni Juma Mpongo aliyekuwa akiidakia Kiyovu Sports ya Rwanda.
Afisa Habari huyo aliwataja wachezaji wengine iliyowanasa mpaka sasa kuwa ni mshambuliaji Nsa Job toka Villa Squad, mlinzi wa kushoto wa JKT Oljoro, Othman Omary, Atupele Green aliyekuwa Yanga na nyota wa timu ya taifa ya U20.
Kumwembe aliwatraja wachezaji wengine kuwa ni Soud Mohamed kutoka Toto Afrika, Seleman Kassim 'Selembi' na Raraq Khalfan waliokuwa African Lyon.
"Hao ni baadhi ya wachezaji tuliowanyakua na tunaendelea na usajili wetu kwa ajili ya kuziba nafasi za wachezaji tisa tuliowatema katika kikosi cha msimu uliopita," alisema Kumwembe.
Aliongeza kuwa, mbali na wachezaji hao pia timu yao imeshamalizana na kocha wao wa zamani Rashid Shedu kutoka Kenya ambaye amechukua nafasi ya Jamhuri Kihwelu 'Julio' waliyeachana nae mara baada ya kuiwesha Coastal kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tano.
"Pia tumeimarisha benchi letu la ufundi kwa kumnyakua Rashid Shedu kuziba nafasi ya Julio tuliyeachana nae," alisema.
Kumwembe alisema pia kwa sasa wanafanya mazungumzo na kiungo wa zamani wa Simba, Jerry Santo ili zweze kuichezea timu yao kwa msimu ujao.
Mwisho
Friday, June 8, 2012
Zuri Chuchu: Muimbaji wa zamani Double M anayeishi na VVU
HUENDA mashabiki wa muziki wa dansi na ule wa kizazi kipya, bado wanalikumbuka jina Zuri Chuchu, mmoja wa waimbaji mahiri wa kike waliowahi kutamba nchini na bendi mbalimbali pamoja na kazi zake binafsi.
Moja ya kazi binafsi zilizomtambulisha muimbaji huyo wa zamani wa Bambino Sound na Double M Sound ni kibao kilichokimbiza kwenye vituo vya runinga kiitwacho 'Channel ya Mapenzi' alichokitoa mwaka 2005 kuelekea 2006 kikiwa katika miondoko ya zouk.
Ila wakati mashabiki walipokuwa wakisubiri vitu zaidi kutoka kwake, ghafla alitoweka kitambo kirefu na kuja kuibuka akijitangaza kwamba ni muathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.
Wapo baadhi ya wanamuziki wenzake, mashabiki wa muziki na hata ndugu, jamaa na rafiki zake walishindwa kumuamini wakidhani labda 'amedata' au alikuwa akitafuta mbinu za kurejea upya kwenye game kwa njia hiyo.
Hata hivyo, mwenyewe alikuwa akisisitiza hajitangazi kutafuta sifa au 'promo' bali ni kweli yeye anaishi na VVU kabla ya kuanza kuendesha kampeni za kuelimisha watu wengi kujikinga na maambukizo ya VVU na Ukimwi.
Baada ya kuendelea na msimamo wake, jamii ilikubali ukweli hasa alipomuona akiendesha kampeni zake shuleni na ndani ya jamii bila ya hofu yoyote, huku mwenyewe akitoa ushuhuda jinsi anavyoendelea kutumia vidonge vya ARV.
Msanii huyo anayejishughulisha kwa sasa na muziki wa Injili akijiandaa kutoa albamu yake ya kwanza iitwayo 'Napenda Kuishi' yenye nyimbo 12, alisema hata yeye awali alipopewa taarifa kuwa ameathirika hakuamini kirahisi.
"Hata mimi jambo hili awali lilinitesa kabla ya kukubali ukweli na kujitangaza hadharani nikibeba jukumu la kuwaelimisha wengine juu ya ugonjwa huo."
Zuri Chuchu ambaye majina yake kamili ni Esther Charles Mugabo, alisema kumtumainia Mungu na ushauri aliopewa na wataalamu wa afya umemfanya leo ajione mtu wa kawaida akiendelea na shughuli zake kuelimisha wengine.
ALIPOTOKEA
Zuri Chuchu alizaliwa Septemba 8, 1974 mkoani Mara akiwa mtoto wa tano kati ya saba wa familia yao na alisoma Shule ya Msingi Nyamboto na kuishia kidato cha pili kwa masomo katika Shule ya Sekondari Tarime.
Alisema tatizo la kifedha la kifamilia ndilo yaliyomkwaza na kukimbilia kusaka maisha katika machimbo ya Dhahabu ya Nyamongo kabla ya mwaka 1994 kwenda Kenya kufanya shughuli zake binafsi na kutamani kuingia kwenye muziki.
Zuri alisema ingawa kipaji cha sanaa hasa uimbaji alizaliwa nacho na kuimba shuleni na kanisani, kupenda uimbaji wa Ally Choki aliyekutana nae Kenya akiwa bendi ya Extra Kimwa, ndiko kulikomfanya atamani nae kuingia katika fani hiyo.
Ndipo alipoanza kujifunza taratibu fani hiyo na aliporejea nchini mwaka 2000 alienda kunolewa na Nyoshi El Saadat kabla ya baadae kutua Bambino Sound.
Baadae alitoka Bambino kwenda Stono Musica alioenda nao umangani mwaka 2004 na aliporejea alitua Tango Stars na kusafiri na Patcheko kwenda Oman chini ya kundi la Kampiosa Sonare.
Alirejea nchini na kujiunga Double M Sound akiwa miongoni mwa walioshiriki kupika albamu ya 'Titanic' kabla ya kujiunga African Beats na kusafiri nao 2006 kwenda Arabuni ambapo alirejeshwa nchini kwa madai hati yake ina tatizo.
"Sikujua chochote niliporudishwa, ila nikiwa nchini nilitumiwa ujumbe wa simu na mwanamuziki mwenzangu mmoja aliyenieleza kwamba nijiandae kufa kwani nimerudishwa kwa vile nilikuwa muathirika, nilistuka mno," alisema.
Katika wiki kadhaa za mateso ya moyo akijifungia ndani, Zuri alisema alijiwa na nguvu za kiroho na kwenda kupima Muhimbili alikothibitishwa kuwa ni kweli alikuwa na VVU, jambo lililozidi kumchanganya na akakata tamaa.
"Nilikuwa najifungia ndani tu nikiwakimbia watu kwa jinsi nilivyoshtushwa na hali hiyo, ila nikajiuliza rohoni nitaendelea kujifungia ndani hadi lini, ndipo nikajitokeza hadharani, ingawa nilipokewa tofauti," alisema.
Zuri alikiri alipokuwa kwenye muziki wa kidunia alijirusha na kujiachia kwa raha zake, pia akiwahi kuishi na wanaume watatu bila ya ndoa, lakini hana hakika alivipatia wapi virusi hivyo na hataki kumnyooshea mtu kidole.
"Siwezi kumlaumu mtu kwani sikuishi kwa utulivu enzi za nyuma, ila najua kila limpatalo mtu ni mipango ya Mungu, nimejikubali na nasonga mbele kuwasaidia wengine waweze kubadili maisha yao," alisema.
MLOKOLE
Zuri ambaye sasa ameolewa na Dennis Ignas Mhala ambaye naye ni muathirika, alisema kabla ya kujigundua ni muathirika na kuingia kwenye muziki wa injili, alishaokoka kitambo.
Alisema aliokoka mwaka 2005 kutokana na kusumbuliwa na mizimu ya upande wa mama yao iliyomtaka awe Mganga wa Kienyeji.
"Nilikuwa nalazimishwa kuwa mganga, sikutaka, nikasumbuliwa sana. Ndipo nilipopata uponyaji na kuokoka hata kabla ya kugundulika kwa tatizo langu," alisema.
Alisema anashukuru tangu alipokabidhi maisha yake kwa Mungu na kujitolea kuendesha kampeni dhidi ya Ukimwi amefarijika akiishi kwa amani na utulivu kuliko ilivyokuwa zamani.
Zuri anashukuru muziki kumsaidia kwa mengi ikiwemo kujenga nyumba kwao Mara, kuanzisha miradi yake ya biashara ya vyakula akitengeza na kuuza maandazi, kazi anayoifanya kwa sasa.
"Sio siri muziki wa kidunia ulinisaidia mengi tofauti na muziki wa Injili kwa vile muziki ninaoufanya sasa siufanyi kibiashara zaidi ya kujitolea kueneza neno la Mungu ila nashukuru sapoti ninayopata kwa watu mbalimbali."
Zuri anayependa kula ugali kwa mbogamboga na matunda na kunywa maji na juisi, alisema hakuna tukio la furaha kwake kama kuvishinda VVU kwa kujikubali, amesema mambo yanayomsikitisha ni kusikia waathirika wenzake wanasambaza virusi kwa makusudi.
Pia alisema tabia ya unyanyapaa ni tatizo kubwa linalofanya jamii kushindwa kuwa wazi katika ugonjwa huo na kufanya walioathirika kujificha na kuendelea kuwaumiza wengine.
HARAKATI
Msanii huyo anayewashukuru wakuu wa shule kwa namna wanavyomuunga mkono katika harakati zake, alikiri amekuwa na wakati mgumu kuendesha kampeni zake kwa kutokuwa na fedha na kutopigwa tafu na serikali.
"Nilidhani kwa nilivyokuwa muwazi na kipaji cha sanaa nilichokuwa nacho ningetumiwa na serikali kuendesha kampeni za kutokomeza Ukimwi kwa ufanisi zaidi, lakini ukweli sina sapoti yoyote najitolea mwenyewe tu," alisema.
Alisema anachoshukuru ni kwamba juhudi zake zimesaidia kuwaokoa wengi na wale walioathirika kujikubali akishirikiana nao kuendesha maisha yao kupitia mashamba ya kilimo cha mboga waliyoyaanzisha ili kujikimu.
Alidai mashamba hayo yapo Gongolamboto na Kisarawe, ambayo yamekuwa wakiwawezesha waathirika kumudu maisha bila ya kuwa ombaomba.
Zuri aliitaka jamii ibadilike na kukubali kuwa Ukimwi ni tatizo linalohitaji vita ya kila mmoja anakawataka wanandoa kuheshimu ndoa zao na wale wasio na ndoa kuwa waaminifu.
"Wengi wameumizwa na Ukimwi, hivyo jukumu letu kila mmoja kuchukua jukumu la kuwa makini nao ili kuepusha au kupunguza maambukizo mapya, kubwa watu wawe waaminifu katika ndoa zao, tusirukeruke ovyo," alisema.
Alisema yeyote anayetaka kumuunga mkono katika harakati zake awasiliane nae kwa 0656-756356 au kumtupia mchango wa kuendesha shughuli zake katika akaunti ya Benki ya Posta 01000294431 kwa jina la Esther A. Mugabo.
Thursday, June 7, 2012
Mchumiatumbo atamba hana mpinzani Bongo
BONDIA wa ngumi za kulipwa wa uzito wa juu, Alphonce Joseph 'Mchumiatumbo' ametamba kuwa, haoni bondia wa kupigana nae nchini kutokana na karibu mabondia wote wa uzito wake kuwachapa na wengine kuingia mitini kukacha kupigana nae.
Aidha, amewaomba mapromota na wafadhili wa ngumi nchini kumsaidia kumtafutia mapambano ya kimataifa na mabondia wa nje ili awe kutimiza ndoto za kutwaa na kulitangaza jina lake katika anga hizo.
Akizungumza na MICHARAZO
kwenye mahojiano maalum, Mchumiatumbo alisema kutokana na kuwapiga karibu mabondia wote wa uzani wake na wengine kumkacha ulingoni anahisi hana bondia wa kupigana nchini hivyo kuwataka mabondia wa nje.
Bondia huyo aliyepigana mapambano sita na kushinda matano, manne kati ya haayo kwa KO na kupata sare moja dhidi ya Ashraf Suleiman, alisema bondia aliyekuwa akidhani angeweza kumpa upinzani Amur Zungu alishaawahi kumkacha ulingoni.
"Kwa kweli kama kila bondia ninayepigana nae naamshinda na wengine kunikacha ulingoni, sidhani kama kuna wa kupigana nami kwa sasa, hivyo nilikuwa naomba nitafutiwe michezo ya kimataifa kujitangaza zaidi na kuwania mikanda," alisema.
Bingwa huyo wa zamani wa Mkoa wa Dar es Salaam wa ngumi za ridhaa, alisema mabondia wengi wa Tanzania wanaishia kutamba nchini tu kwa vile mapromota na waandaaji wa michezo ya ngumi hawawatafutii michezo ya kimataifa kama nchi nyingine.
Mara ya mwisho Mchumiatumbo kupata ushindi ni wiki mbili zilizopita alipomtwanga kwa KO Bahati Mwafyale katika pambano lililofanyika kwenye ukumbi wa DDC Keko.
Madega awaonya Yanga kuhusu uchaguzi
WANACHAMA wa klabu ya soka ya Yanga wameonywa na kutakiwa kuwa makini katika uchaguzi wao mdogo utakaofanyika Julai 15, kwa kuhakikisha wanachagua viongozi wenye uchungu na nia ya dhati ya kuipeleka mbele klabu hiyo.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Imani Madega ambapo alisema uchaguzi huo unapaswa kutumiwa vema na wanachama wa Yanga kuhakikisha wanachagua viongozi wenye sifa na wataoikwamua klabu yao.
Madega, alisema pupa yoyote watakayofanya wanachama hao kwa kuchagua viongozi wasiokuwa makini maana yake ni kuiweka pabaya Yanga na huenda watu wakaanza kunyoosheana vidole kama ilivyotokea katika uongozi uliopita.
Mwenyekiti huyo wa zamani aliyeondoka madarakani kwa heshima kubwa ikiwemo kuiachia klabu hiyo akaunti iliyokuwa na fedha za kutosha, alisema ingawa katika kipindi kama hiki wanachama hunufaika, lakini waikumbuke klabu yao.
"Ni vema wanayanga wakawa makini katika uchaguzi huu kwa kuhakikisha wanachangua watu wa mpira, wenye upeo na uwezo wa kuiongoza Yanga ili itoke mahali ilipo na kuweza kuwa klabu yenye hadhi kimtaifa," alisema.
Kauli ya Madega imekuja wakati mchakato wa uchaguzi huo wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na waliokuwa viongozi wa Yanga, ambapo wagombea 28 kati ya 33 walirudisha fomu za kuwania uongozi katika kinyang'anyiro hicho.
Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi wa Yanga, Francis Kaswahili waliojitokeza kuwania nafasi ya Uenyekiti ni wagombea wanne ambao ni pamoja na Sarah Ramadhan, Edger Chibura na John Jambele.
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti pia ina wagombea wanne ambao ni meneja wa zamani wa klabu hiyo, Ayoub Nyenzi, Ali Mayay, Yono Kevela na Clement Sanga huku kwenye Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ina wagombea 20.
Wagombea hao ni nyota wa zamani wa timu hiyo akiwemo aliyekuwa nahodha Shaaban Katwila, Aaron Nyanda, Edger Fongo na Ramadhan Kampira.
Wengine wanaowania nafasi nne za ujumbe huo wa kamati ya utendaji ni Lameck Nyambaya, Mohammed Mbaraka, Ramadhani Saidi, Beda Tindwa, Ahmed Gao, Mussa Katabalo, George Manyama, Omary Ndula na Jumanne Mwamwenya.
Wagombea wengine ni Abdallah 'Binkleb' Mbaraka, Peter Haule, Justine Baruti, Abdallah Sheria, Jamal Kisongo, Gaudecius Ishengoma na Yona Kevela.
Bingwa wa karate aililia serikali
BINGWA wa mchezo wa Karate kwa nchi za Afrika Mashariki ngazi ya klabu, Sensei Mikidadi Kilindo, ameiomba serikali iutupie macho mchezo huo na kuupa sapoti kama ilivyo kwa michezo mingine ili kuuhamasisha nchini.
Aidha, Kilindo amedai kuwa kutopewa kipaumbele kwa mchezo huo ndio kilichomfanya mara zote awe anaenda na kurudi na medali bila hata kutangazwa au kufahamika kwa wananchi kitu kinachomsikitisha.
Akizungumza na MICHARAZO
, Sensei Kilindo alisema licha ya mchezo huo kuwa na manufaa makubwa kwa taifa na jamii kwa ujumla umekuwa haupewi kipaumbele kama michezo mingine.
Alisema kutokana na hali hiyo ni vema serikali na wadau wa michezo kuutupia macho na kuusaidia ili utangazike na kutumiwa kuiletea sifa Tanzania baada ya michezo mingine kushindwa kufanya hivyo.
Bingwa huyo wa miaka minne mfululizo wa Afrika Mashariki tangu 2008 alisema, kutopewa kipaumbele kwa karate ndiko kunakofanya hata wachezaji wanaoenda kuitangaza nchi wasifahamike warudipo na ushindi.
"Mimi nimerudi hivi karibuni na medali ya dhahabu baada ya kuwa mshindi wa kwanza Afrika Mashariki, hii ni mara ya nne mfululizo, ila hakuna anayejua wala kiongozi aliyewahi kunipokea na kunipongeza inauma sana," alisema.
Pia Kilindo alisema ukimya unaofanywa na viongozi wa Chama cha Karate nchini, TASHOKA katika kuutangaza mchezo huo ni tatizo linalofanya usisikike licha ya mafanikio yake kwa ngazi ya klabu.
Alisema ni vema TASHOKA ikafanya utaratibu wa kuandaa michuano ya taifa angalau mara mbili kwa mwaka itakayoshirikisha klabu mbalimbali nchini kwa lengo la kuuhamasisha na kuutangaza mchezo huo.
Zuri Chuchu Anapenda Kuishi bwana!
MUIMBAJI wa zamani wa bendi za Bambino Sound na Double M Sound, Zuri Chuchu ambaye kwa sasa anaimba muziki wa Injili, yupo mbioni kuingiza sokoni albamu yake ya kwanza iitwayo 'Napenda Kuishi', huku akianza kuipika nyingine mpya.
Zuri, ambaye majina yake kamili ni Esther Charles Mugabo, alisema albamu hiyo yenye nyimbo 12 ilishakamilika mujda mrefu kiasi baadhi ya nyimbo zake kuchezwa redioni, ila aliichelewa kuingiza sokoni kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake.
Alisema hata hivyo anashukuru kwa sasa mipango yake ya kuitoa hadharani albamu hiyo inaelekea vema na wakati wowote ataingiza sokoni.
Zuri, ambaye alitangaza kuishi na VVU akiendesha kampeni mbalimbali kwa sasa kutoa elimu dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, alisema wakati albamu hiyo ya kwanza ikiandaliwa kutoka, tayari ameanza maandalizi ya albamu yake nyingine ya pili.
Alisema mpaka sasa amesharekodi nyimbo sita katika studio za Katra Production iliyompa ofa ya kufyatua albamu hiyo bure kama kuunga mkono juhudi zake za kuendesha neno la Mungu na kutoa elimu ya Ukimwi kwa jamii.
"Nashukuru kwa nafasi niliyopewa na Katra Studio kutoa albamu yangu ya pili ambapo mpaka sasa nimesharekodi nyimbo sita, wakati nikitaka kuingiza sokoni kwanza albamu yangu ya kwanza iitwayo Napenda Kuishi yenye nyimnbo 12," alisema.
Muimbaji huyo, alisema ameamua kutumia muziki kuhubiri na kutoa elimu ya Ukimwi kutokana na ukweli wanaoathirika na ugonjwa huo ni wengi, licha ya kwamba mambo hayawekwi hadharani hivyo anataka maambukizi mapya yasiendelee kuwepo kwa jamii.
Yanga, Simba 'jino kwa jino' kisa Kelvin Yondani
KLABU za soka za Simba na Yanga zimeingia katika vita mpya kufuatia beki wa kati wa kimataifa nchini, Kelvin Yondani kudaiwa kusaini kwa mpigo ndani ya klabu hizo kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Wakati Simba ikiendelea kushikilia msimamo kwamba Yondani ni mali yao baada ya kusaini mkataba mpya, Yanga wenyewe wamesisitiza kuwa beki huyo wameshamilazana nao na kuinyoa Simba iache kutupia vitisho katika suala la mchezaji huyo.
Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu amesema wameshamalizana na Yondani kwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili na kwamba kinachofanywa na watani zao kutaka kuwayumbisha mashabiki na kusisitiza watakula nao sahani moja hadi kieleweke ili kubaini nani mkweli katika hilo.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Simba Ismail Rage, amesema Yanga inajidanganywa kwa Yondani na huenda ikala kwao kwa hasara waliyoingia juu ya beki huyo wa kimataifa ambaye pia anaichezea timu ya taifa, Taifa Stars.
Wednesday, June 6, 2012
Mwenyekiti Villa Squad ajiuzulu, kisa...!
MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Villa Sqaud aliyekuwa pia akikaimu nafasi ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhani Uledi ametangaza kujiuzulu kuiongoza klabu hiyo kwa kile alichodai kutaka kulinda heshima yake.
Habari za kuaminika toka katika klabu hiyo iliyoshuka daraja toka Ligi Kuu na yenye maskani yake eneo la Magomeni Mapipa, jijini Dar na kuthibitishwa na Uledi mwenyewe zinasema mwenyekiti huyo ameamua kubwaga manyanga tangu jana.
Sababu zilizomfanya Uledi ajiondoe uongozini ni kutokana na kusakamwa na wanachama na kutengwa na viongozi wenzake baada ya kushindwa kushindwa kuinusuru Villa Squad isishuke daraja.
Chanzo cha habari cha awali kilisema kutokana na shinikizo kubwa la wanachama hao, Uledi aliamua kubwaga manyanga akiandika barua ya kujitoa madarakani.
Hata hivyo MICHARAZO lilipowasiliana na Uledi kutaka kuthibitisha taarifa hizo, alikiri juu ya kujiuzulu kwake, akidai amefanya hivyo ili kulinda heshima yake kutokana na kuona hali si shwari ndani ya klabu yao.
Uledi, alisema tangu alipochaguliwa hakuwahi kupata ushirikiano wa kutosha kwa viongozi na wanachama, ila aliichukulia hali hiyo kama changamoto wake, lakini kwa hali inavyozidi kwenda mrama klabu kwao ameona bora ajiengue ili Villa itulie.
"Ni kweli nimejiuzulu kutokana na hali ya mambo iliyopo klabuni, pia nahofia kuvunjiwa heshima, hivyo nimewaachia wanachama klabu yao, ingawa bado nitaendelea kuwa ndani ya timu hiyo kwa hali na mali kama mwanachama hai," alisema.
Uledi, aliongeza anadhani chokochoko zote zilizopo Villa Squad kwa sasa zimetokana na timu hiyo kushindwa kubaki ligi kuu, japo alidai yapo mambo mengi yaliyochangia timu hiyo kutohimili ushindani hasa kutokana na hali mbaya ya kifedha iliyokuwa nayo.
Mwenyekiti huyo na wenzake walichaguliwa kwenye uchaguzi mkuu uliokuwa umejaa mizengwe Juni 25 mwaka jana, huku nafasi ya Mwenyekiti na wajumbe watatu zikiwa wazi baada ya Kamati ya Uchaguzi wa TFF, kuwaengua waliokuwa wagombea wake kwa kukosa sifa za kuwania nafasi hizo ikiwemo suala la elimu zao.
Muziki wa Dansi walilia nafasi redioni, runingani
BAADHI ya wamiliki wa bendi za muziki wa dansi wameomba nyimbo za muziki huo zipewe nafasi ya kutosha katika vipindi vya televisheni na redio ili zisikike kama ilivyo sasa kwa taarab na bongofleva.
Walitoa ombi hilo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wao na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari huku wakibainisha kuwa nyimbo za muziki huo kwa sasa hazina nafasi kubwa kama zamani.
Mratibu kamati ya muda wa wamiliki wa bendi, Khaleed Chuma 'Chokoraa' alisema kuwa wamefikia kutoa ombi hilo baada ya kuona hali inavyokwenda sivyo ndivyo na hivyo kuwa na hofu muziki huo ukapotea kama hautapewa nafasi ya kutosha kwenye vyombo hivyo vya habari.
"Tunachofanya sasa ni kujaribu kuwaunganisha wamiliki wote wa bendi za muziki wa dansi wa ndani na nje ya Dar es Salaam kwa lengo ya kufanya mkutano wa pamoja ili kuzungumzia hali hii," alisema Chokoraa.
Alisema kuwa tayari baadhi ya wamiliki hao wameshakubaliana katika hilo na kwamba huenda mkutano huo ukafanyika wiki chache zijazo kama watakuwa wamewasiliana kikamilifu na wamiliki wote.
"Lengo letu ni kuwaomba wahusika angalau kuangalia uwezekano wa kuufanya muziki wa dansi uwe na nafasi ya kutosha kwenye redio na televisheni ili kuwaibua wanamuziki wachanga nao wajulikane, p[ia muziki wa dansi uwe na vipindi maalum kama ilivyo kwa Bongofleva na Taarab ambao karibu kila redio na televisheni una vipindi," alisema.
Naye Msemaji wa kamati hiyo ya muda, Ally Choki, alisema muziki wa dansi ni muziki wa zama na zama, na umekuwa ukisaidia vijana wengine kupata ajira, kwa wamiliki kama wao kuwaajiri, lakini kama hawapewi nafasi ya kutangazika ni vigumu wamiliki kuendelea kutoa ajira hizo.
Choki, alisema kama walivyoweza kupewa nafasi na kutangazika wao wakati wakiibuka ndivyo vijana walioingia katika muziki huo nao wanapaswa kutangazwa kama ilivyo kwa wenzao wa miondoko mingine.
"Siombi hili labda kwa kutaka nitangazwe, ila kuna vijana ambao wapo kwenye muziki huo hawapati nafasi na hivyo kuwatia unyonge na kusababisha dansi kufa tukiondoka kizazi chetu," alisema.
Aliongeza kuwa, kama bendi wamekuwa wakilipa matangazo katika redio na televisheni kwa gharama, lakini fadhila ya matangazo hayo hawayaoni kwa muziki wao kutopewa nafssi katika vituo hivyo.
Pia alidai kwamba muziki wa dansi ni mrefu kwa wimbo mmoja sio ukweli kwani wimbo mmoja wa dansi hauzidi dakika 8, lakini taarab wimbo mmoja huchukua hadi robo saa, lakini wanapewa nafasi, kadhaalika nyimbo za kikongo huwa na muda zaidi lakini nazo pia zinapigwa na vituo hivyo, jambo analohisi kinachofanyika ni kama hujuma kwa dansi.
Aidha, alisema kwa uchunguzi wao wamebaini watangazaji wengi wa redio na televisheni wamekuwa na mzuka na miondoko mingine zaidi ya dansi kwa vile baadhi yao ni mameneja wa wasanii wa bongofleva na wengine hutumia vikundi vya taarab kuandaa maonyesho kama waratibu hivyo hutoa upendeleo kwa ajili ya masilahi yao binafsi.
Choki alisisitiza kilio chaao sio kama kuvilaumu vituo hivyo, ila wanaombwa nao wapewe nafasi kama miondoko mingine kwa sababu muziki wa dani una historia kubwa ya nchi hii pi ni ajira za watu hivyo kama bendi zinazopiga muziki huo zitasahaulika, basi hata ajira za wanamuziki zitakuwa shakani pia.
Mratibu huyo alikiri kwamba muziki wa dansi unachezwa na vituo hivyo vya runinga na redio lakini akadai kuwa si kama ilivyo kwa taarab na bongofleva ambao umekuwa ukipewa nafasi kubwa.
Uchaguzi Mkuu Yanga kumekucha, wanawake waitwa Jangwani
WAKATI zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa klabu ya Yanga ukitarajiwa kufungwa rasmi leo saa 10:00 jioni, wanachama vibopa wa klabu hiyo wamejitokeza kuwania uongozi na kuonyesha namna gani Jangwani walivyopania kufanya mabadiliko ya kuondokana na viongozi 'ombaomba'.
Miongoni mwa waliojitokeza kwa jana kuchukua fomu za kuwania madarakani katika uchaguzi huo utakaofanyika Julai 15 ni pamoja na Yono Kevella wa Yono Auction Mart, Muzzammil Katunzi na Mussa Katabalo wanaowania nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.
Wanachama wengine waliochukua fomu jana kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Eliakim Mmaswi, Lameck Nyambaya, Ahmed Gao na wachezaji nyota wa zamani wa klabu hiyo ambao ni Edgar Fongo, Ramadhani Kampira, Ally Mayai na Aaron Nyanda.
Uchaguzi mdogo wa Yanga unatarajiwa kufanyika Julai 15, hatua inayotokana na idadi kubwa ya viongozi waliokuwa madarakani hapo awali kutangaza kujizulu hivi karibuni, akiwemo Lloyd Nchunga aliyekuwa akishikilia nafasi ya uenyekiti.
Tofauti na wagombea wengine, Katunzi na Katabalo wao walichukuliwa fomu na wazee wa klabu hiyo ambao wako chini ya mwenyekiti wao Jabir Katundu na katibu, Ibrahim Akilimali.
Akimkabidhi fomu Katunzi, Akilimali alisema kuwa lengo la kumtaka mwanachama huyo wa Yanga kugombea ni kuimarisha safu yao ya uongozi ambayo itakuja na jukumu moja tu la kuiendeleza Yanga na kuokoa jahazi lao ambalo anaamini kwamba lilikuwa likizama.
Akilimali alisema kuwa Yanga inahitaji wanachama wenye uwezo wa kuisaidia timu wakati wowote ili ifanye vizuri na kurejesha furaha kwa wanachama wao.
"Hatuhitaji waomba dagaa, tunataka kiongozi mwenye uwezo ambapo inapohitajika Sh. 300,000, yeye atatoa Sh. 600,000," alisema Akilimali.
Hadi kufikia jana, waliochukua fomu kuwania kutwaa mikoba ya Nchunga ni pamoja na John Lambele, huku Ayuob Nyenzi ambaye katika uchaguzi uliopita alijitoa kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, akichukua fomu ya kuomba kuchaguliwa kwenye cheo hicho.
Wengine waliochukua fomu wakiwania nafasi za ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ni Jumanne Mwamwenya, Peter Haule, Gaudecius Ishengoma, Abdallah Sheria, Saleh Abdallah, Abdallah Binkleb na Muhingo Rweyemamu.
Isack Chanzi amejitokeza kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti ambayo Davis Mosha alijiuzulu mapema mwaka jana baada ya kudai kwamba ameshindwa kutimiza malengo yake kwa kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wenzake.
Uchaguzi huo unasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo iliyoko chini ya Jaji Mstaafu John Mkwawa.
Hata hivyo mpaka sasa hakuna mwanachama yeyote wa kike wa klabu hiyo aliyejitokeza kuwania uongozi, hali iliyofanya kamati hiyo kutoa wito kwa wanachama hao kujitokeza kwani milango i wazi kwa wote.
John Kitime ajitosa kwenye utunzi wa vitabu, aja na 'vunja mbavu'
MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi nchini, John Kitime, amejitosa kwenye utunzi wa vitabu, ambapo kwa sasa yuko hatua za mwisho kukamilisha kitabu chake cha kwanza cha 'vunja mbavu' kiitwacho 'Kucheka ni Muhimu'.
Akizungumza na MICHARAZO
jana, Kitime ambaye ni mwanamuziki wa bendi ya Kilimanjaro 'Wana Njenje na pia ni mmoja wa wanakamati ya kutetea muziki wa dansi nchini, alisema amepata wazo la kuandika kitabu hicho kutokana na kipaji cha uchekeshaji alichonacho.
Kitime ambaye wakati mwingine huwa jaji wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Bongo Star Search, alisema kitabu hicho kwa sasa kipo katika hatua ya uhariri kabla ya kuanza mipango ya kukichapisha na kukisambaza ili kuwapa burudani wapenzi wa vunja mbavu.
"Nipo katika hatua ya mwisho ya kumalizia kitabu changu cha kwanza kiitwacho 'Kucheka ni Muhimu', nadhani muda si mrefu mhakato wake wa kukitoa utafanyika na kuwapa burudani Watanzania," alisema.
Aliongeza mbali na kitabu hicho pia ameshaandika vitabu vingine viwili kimoja kiitwacho 'Kilimanjaro Band' ambacho kitakuwa maalum kwa ajili ya kuzungumzia historia ya bendi hiyo ilitoka, ilipo na inapoenda pamoja na wasifu wa wanamuziki wake.
"Kitabu kingine cha tatu ni cha 'Haki Miliki'. Nimeamua kuandika hiki kwa nia ya kuwazindua wasanii kufahamu haki zao katika miliki ya kazi zao," alisema mkongwe huo.
Kitime anakuwa mwanamuziki wa pili mkongwe kujitosa kwenye fani ya uandishi vitabu, baada ya Tshimanga Kalala Assosa, aliyetunga kitabu cha 'Jifunze Lingala' ambacho kinaendelea kutamba sokoni kwa sasa huku akiandaa kingine cha wasifu wake.
Nassib, Majia kuwania ubingwa wa TPBO
MABONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Nassib Ramadhani na Fadhili Majia wanatarajiwa kupanda ulingoni Juni 9 kuwania taji la taifa la Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO).
Pambano hilo la uzani wa Super Fly (kilo 52) litafanyika kwenye ukumbi wa Friend's Corner, Manzese na litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Rais wa TPBO, Yasin Abdallah 'Ustaadh', aliiambia MICHARAZO jana kuwa pambano hilo limeandaliwa na promota Kaike Siraju na kwamba maandalizi yanaendelea vema.
Ustaadh alisema tayari mabondia wote wanaendelea kujifua tayari kwa pambano hilo litakalokuwa la raundi 10 ambapo siku moja ya kupanda ulingoni watapimwa afya na uzito wao.
"Mabondia wetu mahiri kabisa nchini, Nassib Ramadhani na Fadhili Majia wanatarajiwa kupigana kuwania ubingwa wa TPBO uzani wa Super Fly, litakalofanyika siku ya Jumamosi kwenye ukumbi wa Friend's Corner," alisema.
Katika kuzuia vitendo vyovyote vya kihuni, Ustaadh alisema TPBO imejipanga kuhakikisha ulinzi madhubuti katika pambano hilo kwa kuanza kuwasiliana na mkuu wa polisi kituo cha urafiki ili kuwasaidia siku hiyo.
"Tayari tumeshamuandikia barua mkuu wa kituo cha Polisi cha Urafiki, Afande Paparika, ili kutupa ulinzi wa kutosha siku ya pambano," alisema.
Ustaadh alisema imani yake pambano hilo litawasisimua wengi kutokana na upinzani mkali uliopo baina ya mabondia hao na wale watakapambana katika michezo ya utangulizi siku hiyo na kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi.
Bibi Cheka, Dogo Aslay kutambulishwa Kanda ya Ziwa
WASANII wanaokuja juu katika muziki wa kizazi kipya nchini, Asilahi Is'haka 'Dogo Aslay' na Cheka Hija a.k.a 'Bibi Cheka' wanatarajiwa kwenda kutambulishwa rasmi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa wakisindikizwa na wasanii kibao nyota.
Meneja wa wasanii hao, Said Hassani 'Mkubwa Fella' aliiambia MICHARAZO
kwamba wasanii hao wataenda kutambuliwa katika mikoa ya Mwanza na Mara katika maonyesho yatakayofanyika mwishoni mwa wiki hii.
Fella alisema wasanii watakaoenda kuwasindikiza Bibi Cheka anayetamba na wimbo wake wa 'Ni Wewe' alioimba na Mheshimiwa Temba, na Dogo Aslay aliyeachia ngoma mpya ya 'Umbea', ni pamoja na Ferooz, Easy Man, kundi la TMK Wanaume Family na wengine.
"Mkubwa tunatarajia kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya maonyesho maalum ya kuwatambulisha Dogo Aslay na Bibi Cheka, shoo hizo zitakuwa tatu mfululizo zikianza Juni 8 mpaka 10 na watasindikizwa na 'vichwa' kibao," alisema Fella.
Aliongeza kuwa maonyesho yao mawili ya awali yatafanyika jijini Mwanza kabla ya kumalizia burudani yao mkoani Mara na iwapo watapata fursa zaidi wanaweza kuhamishia utambulisho huo mkoani Shinyanga kabla ya kurejea Dar es Salaam.
Alisema mbali na 'Ni Wewe', Bibi Cheka msanii wa muziki wa kizazi kipya mwenye umri mkubwa kuliko wote nchini, atatambulisha wimbo wake mwingine mpya aliouimba kwa kushirikiana tena na Mheshimiwa Temba uitwao 'Mario'.
Warembo Miss Bagamoyo kusaka vipaji J'pili Dar
WAREMBO tisa wanaojiandaa na shindano la urembo la 'Redd's Miss Bagamoyo 2012' wanatarajiwa kuonyeshana kazi katika mchuano wa kusaka kipaji 'Miss Talent' Jumapili ijayo.
Mratibu wa shindano hilo, Awetu Salim, alisema shindano hilo la vipaji litafanyika kwenye ukumbi wa Club Masai, Kinondoni kabla ya warembo hao kuelekea mjini Bagamoyo kuwania taji la urembo la mji huo litakalofanyika Juni 15.
Alisema warembo hao wanaoendelea na mazoezi kwenye ukumbi wa Club Masai chini ya mkufunzi wao, Sadah Salim wameanza kutambiana kila mmoja akidai ana kipaji kitakachompa ushindi kabla ya kwenda kutwaa taji la urembo.
"Warembo wetu wanaendelea vizuri na mazoezi yetu na Jumapili wanatarajia kuchuana kwenye shindano la vipaji, litakalofanyikia kwenye ukumbi wa Club Masai na siku chache baadae wataelekea Bagamoyo kuwania taji la urembo litakalofanyika Juni 15 kwenye ukumbi wa TaSUBA," alisema.
Awetu aliwataja warembo hao kuwa ni Zuhura Abdallah, Veronica James, Rose Lucas, Beatrice Bahaya, Diana Exavery, Nancy, Flora, Yvonne Steven na Celline Wangusu.
Aidha, Awetu alishukuru kuongezeka kwa wadhamini zaidi katika shindano lao ambapo aliitaja kiwanda cha mvinyo cha Dodoma Wines kuwa ni miongoni mwa wadhamini wapya waliojitosa kuwapiga tafu.
Mratibu huyo aliongeza kuwa upande wa burudani katika shindano lao watapambwa na bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' na mshehereshaji wa shughuli hiyo anatarajiwa kuwa Khadija Shaibu 'Dida wa G'.
Aurora afariki, azikwa Dar atakumbukwa kwa mengi
MDAU wa michezo na burudani hapa nchini, Ally Suleiman 'Aurora' amefariki usiku wa kuamkia juzi na kuzikwa jana kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana ilieleza kwamba Aurora alifikwa na mauti baada ya kuugua kwa muda mrefu na kulazwa kwenye hospital ya Muhimbili.
Enzi za uhai wake Aurora aliweza kufadhili mashindano ya urembo, sambamba na michezo mbalimbali ikiwamo ngumi.
Miongoni mwa mabondia waliofanikiwa kwa msaada wa Aurora ni bingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Awadh Tamim ambaye alisaidiwa na Aurora kutimiza ndoto hizo.
Mbali na Tamim, Aurora aliweza kuisadia timu ya waandishi wa Habari za Michezo nchini 'Taswa FC' katika kufanikisha kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ikiwamo yale ya Media Bonanza yanayofanyika kila mwaka mkoani Arusha.
Pia alikuwa akitajwa kama mmoja wa wafadhili wakubwa wa Coastal Union, hivyo kifo chake ni pigo kwa wadau wengi wa michezo na burudani.
Mungu Ailaze Roho ya Marehemu Mahali Pema PEPONI Amiin
Monday, June 4, 2012
Kitale: 'Teja' la kwenye runinga lisiloujua 'unga'
KWA jinsi anavyoigiza na muonekano wake kama 'teja' katika baadhi ya kazi zake za filamu za kawaida na vichekesho, ni vigumu kuamini kuwa msanii Mussa Yusuph 'Kitale Rais wa Mateja' sio mtumiaji wa dawa za kulevya.
Mwenyewe anadai hatumii kilevi cha aina yoyote zaidi ya kuigiza tu kama muathirika wa dawa hizo haramu za kulevya.
Msanii huyo aliyewahi kutamba na makundi ya Kaole Sanaa na Fukuro Arts Professional, alisema watu wachache wanaoamini kama kweli hatumii kilevi.
"Situmii kilevi chochote, sio pombe wala bangi, naigiza tu we mwenyewe unaniona bonge la HB au vipi?" Kitale alisema kwa utani alipohojiawa.
Kitale alidokeza chanzo cha yeye kupenda kuigiza kama 'teja' aliyeathiriwa na 'unga' kiasi cha kuwa kibaka ni uzoefu alioupata kwa kuishi karibu na 'mateja'.
Kitale, alisema jirani na kwao na sehemu kubwa ya Mwananyamala wapo vijana walioathiriwa na dawa hizo za kulevya, hivyo alikuwa akiwachunguza jinsi wanavyoongea, kutembea na maisha yao kwa ujumla na kujifunza mengi.
"We unajua Mwananyamala na maeneo mengi ya uswazi kuna mateja wengi na bahati nzuri karibu na home kuna maskani yao ndio walionisaidia kunifanya niigize kama teja la kutupwa," alisema.
Alisema mbali na uigizaji huo kuwa kama 'nembo' yake, lengo lake ni kuishtua jamii jinsi ya kuthibiti tatizo la dawa za kulevya, linaloteketeza kizazi na nguvu kazi ya taifa.
"Naigiza hivyo, ili kuizindua jamii na kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, dawa hizi zimekuwa zikiharibu na kupoteza nguvu kazi kwa jinsi zinavyoathiri na kuwa na madhara makubwa kwa taifa letu," alisema.
Alisema japo wanaibuka wasanii wanaoigiza kama yeye (Kitale), msanii huyo alidai hana hofu kwa kutambua ataendelea kubaki kuwa Kitale na kamwe hajishughulishi na wasanii hao wanaoiga 'nembo' yake.
"Kwa kweli wapo baadhi ya wasanii wameanza kuiga uigizaji wangu, ila sina hofu na wala muda wa kuwajadili, mie naendelea kupiga kazi kwani naamini nitaendelea kubaki kuwa Kitale aliye mmoja tu yaani Rais wa Mateja," alisema.
Kitale, aliyeanzia sanaa tangu akiwa kinda wakati akisoma Shule ya Msingi, alisema licha ya umaarufu mkubwa alioupata kwa namna ya uigizaji huo wa kama 'teja' hasa alipong'ara katika tamthilia ya 'Jumba la Dhahabu', alidai wakati mwingine hupata usumbufu.
"Ukiacha watu kunishangaa, wapo wengine hudhani uigizaji wangu ni uhalisia wa maisha yangu hivyo huniogopa wakidhani ni teja na kibaka, ingawa huwa naamini ujumbe nilioukusidia umefika kwa jamii," alisema.
VIPAJI KIBAO
Kitale, mchumba wa Fatuma Salum na baba wa mtoto mwenye umri wa miaka karibu miwili aitwae Ahmed, licha ya kuigiza pia ni mahiri kwa utunzi na utayarishaji wa filamu sambamba na akiimba muziki wa kizazi kipya.
Kwa sasa mkali huyo anatamba na wimbo uitwao 'Hili Dude Noma' alioimba na kaka yake Mide Zo na Corner, kikiwa ni kibao cha pili kwake baada ya 'Chuma cha Reli' alichokitoa mwaka jana akiimba na mchekeshaji wenzake, Gondo Msambaa.
Msanii huyo alisema kwa sasa anaendelea kumalizia kazi yake ya mwisho kabla ya kuhitimisha albamu itakayokuwa na nyimbo nane akizitaja zilizokamilisha kuwa ni 'Anajifanya Msela' alioimba na Juma Nature, 'Hili Toto' ft. Sharo Milionea na Mide Zo, 'Tulianzishe' na 'Kinaunau'.
"Nimebakisha wimbo mmoja tu ambao nimeshautunga na kuufanyia mazoezi ila nasubiri kuafikiana na mmoja wa wasanii nyota nchini ili niurekodi," alisema.
Hata hivyo Kitale alikiri kuwa, licha ya umaarufu mkubwa aliopata katika uigizaji, bado haridhiki na masilhai anayopata katika fani hiyo akidai hailipi kama ilivyo kwa muziki.
Alisema, uigizaji haulipi kama muziki, lakini bado hana mpango wa kuachana na fani hiyo.
"Kwenye uigizaji tunaambulia sifa tu, ila masilahi ni madogo mno tofauti na muziki, hata hivyo siwezi kuachana na fani hii kwani nimeshaizoea, na kwa sasa najiandaa kutoa kazi mpya nikishirikiana na Sharo Milionea," alisema.
Alizitaja kazi hizo mpya ni; 'Sharo Madimpoz', 'Sharo Crazy', 'Sharo Taxi Driver' na 'Drug Dealer' wanazoziandaa na msanii mwenzake.
Kitale alisema hizo ni baadhi ya filamu walizopanga kuzitoa ndani ya mwaka huu, sambamba na kuendelea na masuala ya muziki akidai kila mmoja imekuwa ikimpa mafanikio makubwa.
FILAMU
Kitale aliyezaliwa miaka kadhaa iliyopita mjini Morogoro ni shabiki mkubwa wa soka, mchezo aliowahi kucheza utotoni kabla ya kutumbukia kwenye uigizaji, akizitaka timu anazoshabikia kuwa ni Yanga na Manchester City.
"Aisee katika soka huniambii kitu, licha ya kulicheza pia ni mnazi mkubwa wa Yanga na naipenda mno Manchester City," alisema.
Kitale anayependa kula ugali kwa dagaa na kunywa vinywaji laini, alisema mbali na kucheza 'Jumba la Dhahabu' iliyompa umaarufu mkubwa, ameigiza pia filamu kama 30 na kushiriki kipindi cha vichekesho cha 'Vituko Show'.
Alizitaja baadhi ya kazi hizo kuwa ni 'Back from Prisons', 'Mtoto wa Mama', 'Alosto', Mbwembwe', 'More than Lion' aliomshirikisha msanii wa muziki wa kizazi kipya wa kundi la Tip Top Connection, Abdulaziz Chende 'Dogo Janja'.
Kitale, anayemzimia King Majuto aliyeigiza naye baadhi ya kazi, alisema fani ya sanaa nchini imepiga hatua kubwa, isipokuwa inakwamishwa na wajanja wachache wanaowanyonya wasanii na kuwafanya wasinufaike na fani hiyo.
Alisema ni vema juhudi za kupambana na maharamia ikaongezwa, ili wasanii wa Bongo wanufaike na jasho lao na kuishi kama wasanii wa mataifa mengine ambao ni matajiri kuliko hata watu wa kada zingine.
Kitale, anayefurahishwa na tukio la kuzaliwa kwa mwanae, akihuzunishwa na kifo cha mjomba wake aliyekufa kwa ajali ya gari, alisema matarajio yake ni kumuomba Mungu ampe umri mrefu na afya njema afike mbali kisanii.
Alisema angependa kujikita zaidi katika muziki na kutoa kazi zake binafsi za filamu ili kunufaika na jasho lake baada ya kutumikia watu wengine bila kunufaika zaidi ya kuambulia sifa tu.
Drogba aimwagia sifa Taifa Stars, achekelea kuwatungua
NAHODHA wa timu ya taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba, ameisifu timu ya Tanzania kwamba iliwapa wakati mgumu sana katika mechi yao ya raundi ya awali ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2014 kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny mjini Abidjan Jumamosi.
"Ilikuwa ni mechi ngumu sana, lakini jambo la muhimu ni kwamba tumepata pointi tatu," alisema Drogba baada ya mechi hiyo ambayo wenyeji walishinda 2-0.
"Kocha alikuwa na siku tatu za kuwa pamoja nasi, lakini tumeshinda mechi hivyo ni kazi nzuri kwake. Sasa tuna muda wa kufanya kazi pamoja naye na kujaribu kuboresha tulichofanya. Tutajiandaa na mechi ijayo dhidi ya Morocco kisha tuone nini kitatokea."
Ivory Coast ilimfukuza kocha wake, Francois Zahoui na kumpa nafasi hiyo nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Sabri Lamouchi, siku tatu kabla ya mechi dhidi ya Stars.
Ushindi unaifanya Ivory Coast kuongoza Kundi C la kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za Brazil 2014 ikiwa na pointi tatu baada ya Gambia na Morocco kutoka sare ya 1-1 katika mechi nyingine ya kundi hilo na kuzifanya kuwa na pointi moja kila moja baada ya mechi hiyo moja. Tanzania imeanza kwa kushika mkia ikiwa haina pointi.
Baada ya kuanza vibaya, Stars imedhamiria kumalizia hasira zao kwa ushindi katika mechi yao ya pili dhidi ya Gambia Jumapili 10 jijini Dar es Salaam.
Stars haijaonekana kurudishwa nyuma na kipigo kutoka kwa miamba hao wa Afrika na badala yake kikosi kilianza mazoezi jana asubuhi kwenye uwanja wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ivory Coast (FIF) ambao uko pembezoni mwa jiji la Abidjan.
Timu hiyo ilitarajia pia kutafanya tena mazoezi leo asubuhi asubuhi kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani saa 1:30 usiku kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo itawasili Dar es Salaam kesho saa 1:40 asubuhi.
Kocha Kim ambaye amekuja na wachezaji wote hapa ukiondoa wanne ambao ni majeruhi (Thomas Ulimwengu, Nurdin Bakari, Haruna Moshi na Nassoro Masoud Cholo) amesema hivi sasa wameelekeza akili yao kwenye mechi ijayo dhidi ya Gambia.
“Safari ya kujenga timu ndiyo imeanza. Mechi dhidi ya Ivory Coast imepita na ninawashukuru wachezaji kwa kucheza kwa mujibu wa maelekezo na kujituma. Mpira ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa yaliyosababisha tuwape Ivory Coast mabao mepesi," alisema kocha wa Stars, Kim Poulsen.
“Lakini kama nilivyosema mechi hiyo imepita, hivi sasa tunaangalia mechi ijayo dhidi ya Gambia. Hatuna muda mwingine wa kujipanga na ndio maana niliamua kuja na wachezaji wote Abidjan,” amesema Kim.
Mechi dhidi ya Gambia itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Gambia ilitoka sare ya bao 1-1 na Morocco katika mechi iliyochezwa juzi jijini Banjul.
Stars itamkosa nahodha msaidizi Aggrey Morris ambaye alitolewa kwa kadi ya pili ya njano dakika ya 65 baada ya baada ya kumkwatua mchezaji wa Ivory Coast, Gosso Gosso. Morris alipewa njano ya kwanza katika dakika ya 12 baada ya kumkwatua Didier Drogba.
Vikosi katika mechi hiyo vilikuwa; Ivory Coast: Boubacary Barry, Kolo Toure, Siaka Tiene, I. Lolo, Emmanuel Eboue, Cheik Tiote/Ya Konan, K. Coulibaly, Jean Gosso Gosso, Didier Drogba, Salomon Kalou/Max Gardel na Gervinho/Kader Keita.
Tanzania; Juma Kaseja, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Mrisho Ngassa, Shaban Nditi, Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar/ John Bocco, Mbwana Samatta na Frank Domayo.
CHANZO:NIPASHE
Wazee wa Ngwasuma kutumbuiza Miss Kigamboni
BENDI ya muziki wa dansi ya FM Academia maarufu kama 'Wazee wa Ngwasuma' na msanii wa vichekesho, Mpoki, wataburudisha wakati wa shindano la kumsaka mrembo kitongoji cha Kigamboni City 2012 litakalofanyika Juni 15 katika ukumbi wa Navy Beach, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu alisema kutakuwa na ushindani mkubwa katika shindano hilo kutokana na vimwana wakali waliopo kambini na bendi ya FM inafahamika kwa kutoa burudani nzuri kwa mashabiki wa muziki wa dansi nchini.
Somoe alisema kuwa burudani nyingine kali itatoka kwa Mpoki ambaye mbali ya kuwa ni mkazi wa Kigamboni, lakini ukubwa wa kazi yake unafahamika na kwamba mashabiki watapaswa kuandaa mbavu za ziada kutokana na vichekesho vyake.
Mratibu huyo kutoka kampuni ya K& L, alisema kuwa jumla ya warembo 15 wanaendelea kujifua katika kambi ya mazoezi chini ya mwalimu wao Miss Temeke, Hawa Ismail, ambaye anashirikiana na mshiriki wa Miss Tanzania mwaka jana Blessing Ngowi.
Aliwataja warembo hao kuwa ni pamoja na Carolyne Dandu, Fatina Francis, Edda Slyvester, Aisha Mussa, Rosemary Peter, Doreen Kweka, Caroline Peter, Agnes Goodluck, Sophia Martine, Rosemary Deogratius, Beatrice Boniface, Julieth Philip na Khadija Kombo.
"Kigamboni ni zaidi ya kitongoji, tunaamini shindano letu litakuwa na mvuto na hadhi ya kipekee kama eneo lake lilivyo," aliongeza.
Somoe alisema kuwa warembo watakaofanya vizuri watapata nafasi ya kuwakilisha kitongoji hicho katika mashindano ya kanda ambayo yatafanyika baadaye mwaka huu.
Aliwataja wadhamini ambao tayari wamethibitisha kuwezesha shindano hilo kuwa ni pamoja na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd's, Dodoma Wine na NSSF, Hope Country Motel, Norbro’s Collections, Screen Masters, Global Publishers.
Salha Israel kutoka Kanda ya Ilala ndiye mrembo anayeshikilia taji la taifa ambapo mwaka huu ratiba ya mashindano hayo imebadilika.
CHANZO:NIPASHE
Warembo watakaochuana kwenye shindano la Miss Kigamboni 2012
Masai Nyota Mbofu aachia Rungu na Mukuki
MCHEKESHAJI maarufu nchini, Gilliad Severine 'Masai Nyota Mbofu', ameachia wimbo mpya uitwao 'Rungu na Mukuki' sambamba na video yake akishirikiana na wasanii wa kundi la Vichwa la Zambia, Simple K na G4.
Tayari wimbo na video hiyo imeshaanza kurushwa hewani wakati mwenyewe akijiandaa kupakua kazi nyingine mpya.
Akizungumza na MICHARAZO, Masai Nyota Mbofu, alisema wimbo huo ameurekodia nchini Zambia katika studio za Hez Sound chini ya Prodyuza, Acknex na video yake amefyatulia nchini humo na kuja kuimalizia Tanzania.
Msanii huyo, alisema kazi hiyo mpya ni salamu kwa mashabiki wake waliomzoea kumuona katika filamu na komedi tu, kwamba kwenye muziki naye yumo.
Masai Nyota Mbofu, alisema wakati wimbo na video hiyo ikiendelea kutamba ameanza kuandaa wimbo mipango ya kutoa kazi nyingine kwa lengo la kuja kufyatua albamu hapo baadae.
"Wakati Rungu na Mukuki, ikiendelea kukimbiza kwa fideo na radio, tayari nimenza kuandaa kazi nyingine nataka onyesha mashabiki angu kwamba mi nawesa," alisema Masai kwa kiswahili kibovu cha kikomedi.
Mkali huyo aliyeanza kutamba kwenye michezo ya runinga akiwa na kikundi cha Jakaya Theatre kabla ya kuibukia kwenye filamu chini ya kampuni ya Al Riyamy Production.
Baadhi ya kazi zilizowahi kumpa ujiko msanii huyo ni Iny'e Plus, 'Iny'e Gwedegwede', 'Vumba Vimejaa', 'Pedeshee' na sasa anatamba na kipindi cha Vituko Show.
Mosha awachomolea wazee Yanga, fomu zachangamkiwa
HUKU zoezi la uchukuaji fomu za kuwania uongozi kwa ajili ya Uchaguzi wa klabu ya Yanga ukizidi kupambamoto, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Davis Mosha amewachomolea wazee wa Yanga waliomtaka awanie tena uongozi akidai hana mpango huo.
Aidha, kamati ya uchaguzi imekanusha taarifa kwamba Mfadhili Mkuu wa klabu huyo, Yusuf Manji amejityosa kuchukua fomu za kuwania Uenyekiti, ingawa kamati hiyo imesema milango i wazi kwake kama ana dhamira hiyo ya kuwania uongozi Yanga katika uchaguzi utakaofanyika Julai 15.
Mosha, aliyefuatwa na wazee hadi nyumbani kwake Mikocheni juzi jijini Dar es Salaam, akijibu maombi ya baraza wazee lililomuomba kugombea moja ya nafasi katika uchaguzi huo na kusema hana mpango wa kuwania uongozi.
Alisema kwa sasa hayuko tayari kugombea uongozi katika klabu lakini yupo tayari kusaidia kitu chochote kinachohitajika kwa maendeleo ya klabu.
“NAwashukuru wazee kwa kuja kuniaona na kunipa pole, pia nashukuru kwa kuona umuhimu wa mimi kuwepo Yanga, ila napenda niwaeleze sintoweza kuwania uongozi kwa sasa, bali nipo tayari kuisaidia Yanga kwa lolote litakalokuwa ndani ya uwezo wangu,”alisema.
“Mimi ni mpiganaji kweli, naiopenda Yanga na napenda iwe na maendeleo…nitashirikiana na viongozi watakaochaguliwa lakini mimi siwezi kuongoza Yanga kwa sasa nina mambo mengi ya kufganya,”alisema
Mosha ambaye alijitoa madarakani miezi michache kabla iongeza kuwa wanachama wa Yanga hawana budi kuchagua viongozi ambao wapo tayari kuisaidia klabu hiyo na si kupata chochote.
“Napenda kuwahadharisha wanachama wenzangu nkwamba tusikurupuke, tutafute watu wenye mapenzi ya kweli na si maslahi kwani Yanga ni kwa ajili ya kutumika si kuvuna,”alisema.
Awali Katibu wa baraza hilo Ibrahim Akilimali ‘Abramovich’ kwa niaba ya wazee wengine wa Yanga ambao walikwenda nyumbani kwa Mosha kwa ajili ya kumpa pole kutokana na kufiwa na Mkwewe, aliwasilisha ombi la kumtaka Mosha kurejea kundini.
Mzee Akilimali alisema kuwa wameamua kumuomba Mosha arejee kuongoza Yanga kutokana na umahiri mkubwa aliouonesha kipindi alichoongoza ambapo alikuwa mstari wa mbele kuisaidia timu hiyo na hatimaye kwa kipindi kifupi iliweza kupata mafanikio.
“Mwanetu sisi wazee wako tumekuja kukupa pole lakini pamoja na hilo tunakuomba urejee kuongoza kwani bado tunakumbuka ushupavu wako katika kuongoza…kuna kombe la Kagame linakuja ambalo wewe ulichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana, sasa uje ulibakize tena kombe hilo,”alisema Mzee Akilimali.
Aidha , Mzee Akilimali aliongeza kuwa wanataka Yanga iingie kwenye mashindano na kushiriki hivyo mchango wa Mosha katika hilo ni muhimu sana.
Uuchaguzi huo utajaza nafasi za viongozi waliojiuzulu na ile ya mjumbe mmoja aliyefariki dunia, ambapo viongozi watakaochaguliwa watakaa madarakani kwa muda uliosalia kama katiba inavyoelekeza na kwa mantiki hiyo viongozi hao watamaliza muda wao wa miaka minne mwaka 2014.
Uchaguzi huo unafuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti Lloyd Nchunga baada ya kushinikizwa na baadhi ya wanachama wakiongozwa na baraza la wazee wa klabu hiyo kutokana na kushindwa kuiletea mafanikio klabu hiyo chini ya uongozi wake.
Pia nafasi ya Makamu mwenyekiti iliyokuwa inashikiliwa na Davis Mosha ambaye alijitoa miezi michache baada ya kuchaguliwa kutokana na kutoelewana na Nchunga, huku mjumbe Theonest Rutashoborwa akitangulia mbele ya haki.
Uchaguzi huo pia utajaza nafasi za Wajumbe walioachia ngazi ambao ni pamoja na Mzee Yusuf, Charles Mgondo na Ally Mayay.
Kwa sasa Yanga imebaki na wajumbe wanne, Mohammed Bhinda, Sarah Ramadhan, Tito Osoro na Salum Rupia ambao baada ya uchaguzi wataungana na viongozi wapya na kuteua wajumbe wengine watatu kwa mujibu wa katiba, hiyo inatokana na wajumbe hao wa kuteuliwa Seif Ahmed, Mbaraka Igangula na Pascal Kihanga kujiuzulu.
Katika hatua nyingine, wagombea watatu walijitokeza kuchukua fomu za kuwanmia nafasi ya ujumbe katika, wanachama hao ni pamoja na Jumanne Mwamamwenye na Salehe Hassan na Ayoub Nyenzi anayewania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Huku kamati ya uchaguzi ikikanusha taarifa kwamba Manji naye amejitosa kuchukua fomu kuwania Uenyekiti wa klabu hiyo, ingawa umesema milango i wazi kwake na kwa yeyote mwenye sifa kabla ya zoezi la kuchukua na kurudisha fomu kufungwa rasmi Jumatano jioni.
Simba noma, yabebe mzigo wa matibabu ya akina Boban
UONGOZI wa klabu ya Simba umesema kuwa umechukua jukumu la kuwatibu wachezaji wake Haruna Moshi 'Boban' na Nasoro Masoud 'Cholo' walioumia wakiwa na kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' baada ya kukatishwa tamaa na kusuasua kwa shirikisho la soka (TFF) kubeba gharama hizo.
Akizungumza jijini Dar, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alisema kuwa klabu yake haina muda wa kusubiri matibabu ya TFF kwa wachezaji hao kwasababu ya kuzongwa na kalenda ya mashindano.
Simba imeanza maandalizi kwa ajili ya mashindano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati hivyo haiwezi kusubiri mpaka TFF liwatibie 'Boban' na 'Cholo'.
Kauli hiyo ya Mtawala imekuja siku moja baada ya katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah, kusema bila kutaja tareeh rasmi kuwa shirikisho litafanya jitihada za kuwatibu wachezaji hao walioumia wakiwa ndani ya kikosi cha Stars.
"Sisi ndio tunawalipa mshahara wachezaji hawa, na mtu akigundulika ameumia anatakiwa kutibiwa haraka na hakuna kusubiri," alisema.
"Tumeanza kuwatibu ili kocha wetu atakaporudi awakute wachezaji katika hali nzuri na kuendelea na programu zake za mazoezi."
Kocha wa timu hiyo Mserbia Milovan Cirkovic atarejea nchini Juni 15, alisema.
Kocha huyo ametuma programu ya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Kagame ambayo kwa sasa yanasimamiwa na kocha wa makipa wa timu hiyo James Kisaka.
"Timu imeanza maandalizi chini ya Kisaka (James) kwa sababu kocha msaidizi naye ameenda mapumzikoni nchini kwao," alisema zaidi Mtawala.
Alisema kocha msaidizi Richard Amatre ataungana na timu Alhamisi baada ya kuwasili nchini Jumatano.
Mtawala alisema klabu hiyo imeweka malengo ya kutwaa ubingwa wa Kagame ambao unashikiliwa na watani zao Yanga walioutwaa kwenye mashindano ya mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Simba goli 1-0.
Noela ndiye Miss Tabata 2012
MREMBO Noela Michael, 19, usiku wa kuamkia juzi alifanikiwa kutwaa taji la Tabata 'Miss Tabata 2012' katika shindano lililofanyika kwenye ukumbi wa Da’ West Park jijini Dar es Salaam.
Noela ambaye awali alibwagwa katika kuwania taji la talent aliweza kuwafunika warembo wengine 18 waliokuwa wanawania taji hilo lililokuwa linashikiwa na Faiza Ally.
Noela alizawadiwa shilingi 500,000 na king’amuzi iliyolipiwa miezi sita iliyotolewa na Multichoice.
Nafasi ya pili katika shindano hilo ilishikwa na Diana Simon, 20, aliyeshinda Sh 500,000 watatu ni Wilhemina Mvungi, 21, (Sh 350,000), wanne ni Phillos Lemi, 19, na Suzzane Deodatus, 20, alishika nafasi ya tano. Wote wawili walizawadiwa Sh 200,000 kila moja.
Warembo hao watano watakiwakilisha Tabata katika mashindano ya Kanda ya Ilala yatakayofanyika baadaye mwaka huu.
Warembo wengine waliofanikiwa kuingia hatua ya 10 walikuwa ni Angel Kisanga, Khadija Nurdin, Haika Joseph, Queen Issa na Neema Saleh. Wote walizawadiwa Sh 100,000 kila moja.
Queen Issa alifanikiwa kutwaa taji la mrembo mwenye kipaji cha kucheza huku Mercy Mlay akiteuliwa kuwa mrembo aliyekuwa na nidhamu ya juu tangu kuanza kwa shindano hilo. Queen na Mercy kila moja alizawadiwa Sh 100,000.
Warembo waliosalia walipata kifuta jasho cha Sh 50,000 kila moja.
Shindano hilo lilipambwa na burudani kutoka kwa bendi ya Mashujaa, Mashauzi Classic iliyoko chini ya Isha Ramadhani Mfalme na Costa Sibuka.
PICHA Tofauti za matukio ya Miss Tabata 2012, ambapo Noela Michael aliibuka kidedea.
Subscribe to:
Posts (Atom)