STRIKA
USILIKOSE
Saturday, August 11, 2012
Wanamasumbwi chipukizi Bongo kuvuna nini Idd Pili?
MASHABIKI wa ngumi za kulipwa nchini wanatarajia kupata burudani ya aina yake siku ya Idd Pili, wakati mabondia wawili chipukizi Ramadhani Shauri na Nassib Ramadhani watakapoanda ulingoni kuzipiga.
Mabondia hao walio chini ya kocha Christopher Mzazi watazipiga na mabondia kutoka Kenya na Uganda katika michez itakayofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam kuwania mataji ya IBF.
Shauri yeye atapanda ulingoni kuzichapa katika pambano la kuwania ubingwa wa IBF-Afrika uzani wa vinyoya (Featherweight) la raundi 10 dhidi ya Mganda, Sunday Kizito.
Bondia Nassib anayeshikilia taji la chama cha World Boxing Forum (WBF), atatangulia kuzipiga na Twalib Mubiru kutoka Kenya katika pambano la uzani wa Bantam kuwania ubingwa wa IBF-Afrika Mashariki na Kati.
Michezo hiyo yote inaratibiwa na promota Lucas Rutainurwa ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Kitwe General Traders na kusimamiwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini, TPBC.
Kwa mujibu wa Rais wa TPBC ambaye pia ni Rais wa IBF Afrika/USBA, Onesmo Ngowi, pambano la Shauri na Kizito ndilo pigano kuu (main bout) na limepewa jina la 'The Rumble in the City of Heaven's Peace'.
Ngowi, amemtaja Shauri kama 'mfalme' mpya aliyeanza kutishia hadhi za mabondia wengine nchini kutokana na kipaji kikubwa alichonacho katika mchezo huo wa ngumi za kulipwa.
Rais huyo alisema rekodi aliyonayo na namna ya uchezaji wake akiwa ulingoni imemfanya awe anamfananisa na nyota wa zamani wa ngumi za kulipwa kutoka Marekani Sugar Ray Leonard.
Katika umri alionao usiozidi miaka 25, Shauri tayari amekuwa na kivutio cha aina yake kutokana na haiba yake ya uchezaji na rekodi aliyonao tangu aanze kucheza mchezo huo chini ya kocha Mzazi wa gym iliyopo Mabibo jijini Dar es Salaam.
Bondia huyo amecheza mapambano 15, akishinda michezo 12, kupoteza miwili na kuambulia sare moja, huku akishikilia nafasi ya pili kati ya 40 katika orodha wa mabondia wa uzito wake akitangliwa na Roger Mtagwa.
Kwa upande wa mpinzani wake yeye ana rekodi ya kucheza mapambano 22 akishinda 12, kupoteza tisa na kupata sare moja.
Ngowi anaamini pambano hilo litasisimua mashabiki wengi wa ngumi ambao kwa mua mrefu hawajapata kushuhudia mabondia vijana wakiwania mataji ya kimataifa.
'Ni zamu ya kuwapa nafasi mabondia chipukizi kuonyesha vipaji vyao na kuwania mataji ya kimataifa kuitangaza Tanzania," alisema Ngowi.
Kuhusu pambano la Nassib Ramadhani, Ngowi alisema nalo linatarajiwa kuwa gumzo kutoka na rekodi alizonazo bondia huyo aliyecheza mapambano 11 na kushinda tisa akipoteza mawili.
Nassib pia ndiye anayeongoza orodha wa mabondia 21 wa Tanzania wa uzani wake huku katika orodha ya dunia akishika nafasi ya 88 kati ya mabondia 636.
Mpinzani anayecheza nae rekodi yake inaonyesha amecheza michezo 20 akishinda 11 na kupoteza saba huku akitoka sare miwili, hali inayofanya pambano lao litakuwa na msisimko na mvuto wa aina yake.
Mbali na michezo hiyo siku hiyo kwa mujibu wa Ngowi kutakuwa na michezo mingine kadhaa ya utangulizi ambayo itatoa burudani kwa mashabiki wa ngumi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.
Ngowi alisema lengo la Kamisheni la Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBC ni kuhakikisha kila miezi miwili kunakuwa na mapambano ya kimataifa kwa mabondia wa Tanzania baada ya kushuhudiwa 'ukame' wa mataji kwa muda mrefu.
"Pia lengo letu ni kutoa nafasi kwa mabondia chipukizi kuonyesha vipaji vyao sambamba na kuendeleza mpango maalum ulianzishwa na IBF-Afrika/USBA kutangaza utalii kupitia mchezo huo wa ngumi," alisema.
Tayari mabondia hao watakaoonyeshana kazi siku hiyo ya Idd Pili, wamejichimbia kambini wakijiandaa na mapambano hayo, huku mratibu Lucas Rutainurwa, akisisitiza kila kitu kinaendelea vema akiwataka mashabiki wa ngumi kujitokeza siku ya siku.
Kama alivyonukuliwa Rais wa TPBO ambaye pia ni msemaji wa TPBC, Yassin 'Ustaadh' Abdallah, huenda hiyo ikawa ni nafasi nzuri kwa mabondia hao chipukizi wa Tanzania kuanza safari ndefu ya kufikia mafanikio yaliyowahi kufikiwa na wakongwe kama Rashid Matumla aliyewahi kunyakua ubingwa wa dunia wa WBU.
Tusubiri tuone kipi kitakachovunwa na mabondia hao katika michezo
yao hiyo, ambayo itafanyika wiki chache kabla ya kumshuhudia Mtanzania mwingine, Thomas Mashale hajapanda ulingoni nchini Ujerumani kuwania taji la UBO Vijana uzani wa Kati kwa kupigana na mwenyeji wake Arthur Hermann.
Awali pambano hilo linaloratibiwa na Becker BoxPromotion lilipangwa kufanyika wiki iliyopita nchini humo, lakini limeahirishwa hadi Septemba 5 mjini Berlin, Ujerumani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment