STRIKA
USILIKOSE
Saturday, August 11, 2012
Yanga kutafuta kocha mwingine iwapo...!
UONGOZI wa mabingwa wa soka Afrika mashariki na Kati, Yanga, umesema utatafuta kocha mwingine kama mwalimu wao Tom Saintfiet atapata kazi ya kufundisha timu ya taifa ya Kenya.
Hata hivyo, Yanga imesema mpaka sasa haina taarifa rasmi juu ya kocha wake huyo kutakiwa na Shirikisho la soka Kenya kwa ajili ya kuifundisha timu yake ya taifa hivyo inasubiri barua kutoka KFF.
Akizungumza na Nipashe jana, Afisa habari wa Yanga, Luis Sendeu, alisema endapo KFF itaonyesha dhamira ya kumtaka Saintfiet hawatomzuia.
"Hatutaweza kumzuia," alisema Sendeu.
"Tutakaa naye na kujua nini cha kufanya, lakini napenda kuwaambia kuwa sisi kama Yanga hatuna taarifa za kocha wetu kutakiwa Kenya.
"Ila kama tutapata taarifa rasmi uongozi utajua nini cha kufanya," alisema Sendeu.
Itabidi klabu itafute kocha mwingine endapo itaridhia kusitisha mkataba wa miaka miwili wa mwalimu huyo Mbelgiji aliyeanza kuifundisha mwezi uliopita.
Sendeu alisema kuwa kwa sasa kocha huyo anaendelea na programu zake za kuiandaa timu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Bara ambao utaanza mwezi ujao.
"Kocha Tom yupo na kikosi akikiandaa kwa ajili ya ligi kuu ya Bara... na yeye ana programu zake ambazo anazifanyia kazi kuhakikisha timu inakuwa katika kiwango cha juu zaidi ya sasa pindi ligi kuu itakapoanza," alisema.
Alisema viongozi wa Yanga wanaamini uwezo ambao timu hiyo ilionyesha kwenye mashindano ya Kagame ndiyo ambao utahamishiwa kwenye ligi na kufuta makosa waliyoyafanya msimu uliopita ambapo ilivuliwa ubingwa na mahasimu wao Simba.
Yanga ilionyesha soka la hali juu kwenye michuano hiyo licha ya kuanza kwa kipigo, ikishinda michezo yake sita iliyofuatia hadi kutetea Kombe la Kagame.
CHANZO:NIPASHE JUMAMOSI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment