|
Brandts wa pili kutoka kulia, akiwa na viongozi wa Yanga. Kulia ni Seif Magari. Kushoto kwake ni Bin Kleb na Majjid |
|
Anapakia mizigo kwenye gari la Bin Kleb |
|
Anazungumza na Waandishi wa Habari |
|
Akiwa na viongozi wa Yanga |
|
Kulia kwake Bin Klerb, kushoto Mwalusako |
|
Anatoka Uwanja wa Ndege |
KOCHA
mpya wa Yanga, Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts, anatarajiwa
kutambulishwa leo saa 3:00 asubuhi katika Mkutano maalum na Waandishi wa
Habari utakaofanyika makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga
na Jangwani, Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako ameiambia BIN ZUBEIRY jana
kwamba, katika Mkutano huo, pamoja na kuelezwa mkataba ambao klabu
imeingia na kocha huyo, lakini pia Waandishi watapata fursa ya kumuuliza
maswali mbalimbali kocha huyo.
Beki
huyo wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi na klabu ya PSV Eindhoven ya
Holanzi, aliwasili jana majira ya saa 3:45 usiku katika Uwanja wa ndege
wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na ndege ya KLM na kupokewa na
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako na viongozi wengine, Abdallah
Ahmad Bin Kleb, Seif Ahmad ‘Magari’ na Majjid Suleiman.
Yanga,
imetimiza malengo yake ya kuwa kocha mpya, kabla ya kucheza na wapinzani
wao wa jadi, Simba SC, Oktoba 3, mwaka huu baada ya kumfukuza Mbelgiji,
Tom Saintfiet, kutokana na kuwasili kwa Brandts, ambaye ataanza kazi
mara moja leo.
Kikosi
cha Yanga kipo kambini, hoteli ya Uplands, Changanyikeni, Dar es Salaam
na kabla ya kucheza na Simba Jumatano, kesho kitacheza na African Lyon,
Uwanja wa Taifa pia.
Mholanzi
huyo aliyefukuzwa APR ya Rwanda baada ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki
na Kati, Kombe la Kagame, Agosti mwaka huu amepewa ukocha wa Yanga,
baada ya Mbrazil Marcio Maximo kukataa nafasi hiyo kwa mara ya pili.
Mtaalamu
huyo, alizaliwa Februari 3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland,
mbali na PSV Eindhoven, alichezea pia Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht
na De Graafschap.
Brandts
aliichezea mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na kuifungia mabao matano
na pia alicheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.
Katika
fainali hizo, Raundi ya pili kwenye mechi na Italia, aliweka rekodi ya
kuwa mchezaji pekee aliyezifungia mabao timu zote katika mechi moja
kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Alianza
kujifunga dakika ya 18, kisha akaisawazishia Uholanzi dakika ya 50
katika mechi ambayo, mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye aliifungia timu
yake bao la ushindi na kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
Alipostaafu
soka akawa kocha na katikati ya msimu wa 2007–2008, Brandts aliambiwa
hataongezewa mkataba NAC-Breda, licha ya matokeo mazuri ya kushika
nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), ingawa uamuzi huo
haukuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo na nafasi yake akapewa Robert
Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
Akateuliwa
kuwa Kocha wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla ya kufukuzwa Desemba 2009 na
kuibukia APR ya Rwanda mwaka 2010, ambako ‘riziki’ yake imeisha miezi
miwili iliyopita na sasa amepata maisha mapya Yanga.
Akiwa
APR, Brandts alifungwa mechi zote mbili na Yanga iliyokuwa ikifundishwa
na Mbelgiji Tom Saintfiet katika Kombe la Kagame, moja ya makundi 2-0 na
nyingine ya Nusu Fainali 1-0. Yanga iliibuka bingwa, ikiifunga Azam FC
2-0 kwenye fainali.
Brandts
atakutana na wachezaji wake wa zamani wawili Yanga, beki Mbuyu Twite
anayeanza msimu wa kwanza katika klabu hiyo na kiungo Haruna Niyonzima
anayeingia katika msimu wa pili, ambao alifanya nao kazi APR.
CHANZO:BIN ZUBEIRY