STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, September 19, 2012

Kivumbi za Mabingwa Ulaya kuendelea tena leo

Kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson

KOCHA wa Manchester United, Alex Ferguson amesema hapatakuwa na marudio ya kutolewa mapema kama mwaka jana katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya wakati wakijiandaa kucheza mechi yao ya ufunguzi wa Kundi H nyumbani dhidi ya Galatasaray leo.
Mabingwa hao mara tatu wa Ulaya walishindwa kusonga mbele kutoka katika hatua ya makundi msimu uliopita baada ya kipigo cha kustusha cha 2-1 kutokakwa klabu ya Uswisi ya FC Basel katika mechi yao ya mwisho.
"Tumefungwa katika fainali mbili dhidi ya Barcelona na tumeshinda fainali nyingine mbili katika miaka 10 iliyopita lakini tunataka kufanya vizuri zaidi," Ferguson aliiambia tovuti ya klabu hiyo (www.manutd.com). "Hakika tutafanya vyema kuliko msimu uliopita, hakuna maswali kuhusu hilo.
"Kombe la Ulaya ni bab'kubwa. Kuna hisia kali kuelekea katika fainali ya Ulaya.
"Pia, bila ya maswali, kombe linainua heshima yako mchezoni kama ilivyo kwa Real Madrid na AC Milan. Tunataka kufikia kule kwa idadi ya makombe katika soka la Ulaya."
Kuanzia kwenye kipigo kutoka kwa Barcelona katika fainali ya mwaka 2011, Man U imeshinda mechi tatu tu za Ulaya kati ya 11 na imefungwa nne kati ya tano zao za mwisho.
Kikosi cha Ferguson, kinachoshiriki michuano hiyo kwa mara ya 18, ambayo ni rekodi, kitakuwa bila ya majeruhi wa muda mrefu Wayne Rooney leo lakini timu inalo "jembe" Robin van Persie lililotayari kuanza kwa mara ya kwanza kuichezea timu yake mpya katika michuano hiyo ya Ulaya.
Van Persie amekuwa katika kiwango cha juu tangu alipowahama mahasimu Arsenal mwisho wa msimu na tayari anaongoza katika ufungaji wa Ligi Kuu ya England akiwa na magoli manne, sawa na Michu wa Swansea City.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi aliachwa nje ya kikosi kilichoanza Jumamosi kabla ya kuingia kipindi cha pili na kuisaidia Man U kuifunga Wigan Athletic 4-0 katika ligi.
Mtokea benchi mwenzake Nick Powell alicheza mechi yake ya kwanza Man U na kufunga goli kali la shuti la mbali dhidi ya Wigan na mchezaji huyo wa zamani wa Crewe Alexandra alisema alikuwa na presha kubwa wakati alipoingia mbele ya mashabiki 75,142 kwenye Uwanja wa Old Trafford.
"Nilipoingia kwa mara ya kwanza ilinitisha kidogo kwa sababu nilizoea kucheza mbele ya mashabiki 5,000 tu," alisema kiungo huyo mwenye umri wa miaka 18. "Lakini ni mazingira mazuri na mashabiki walikuwa bab'kubwa.
"Najifunza kila siku kutoka kwa viungo Paul Scholes, Michael Carrick, Ryan Giggs. Wameshapitia hayo na kutwaa mataji na nataka kushinda mataji pia."
Galatasaray wanacheza mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika miaka sita.
Klabu hiyo ya Uturuki haijashinda mechi yoyote kati ya saba walizocheza dhidi ya timu za England lakini ilipata sare za kukumbukwa dhidi ya Manchester United, Liverpool na Leeds United katika rekodi zao.
Umut Bulut, ambaye amefunga magoli matano katika mechi nne za ligi msimu huu, anajiandaa kuwa patna wa mshambuliaji wa zamani wa Bolton Wanderers, Johan Elmander katika mashambulizi. Beki wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Eboue, anatarajiwa kuanza katika ulinzi.

Ratiba ya mechi za leo Ligi ya Mabingwa Ulaya:

Kundi E
Shakhtar          v Nordsjaelland
Chelsea           v Juventus
  
Kundi F
Lille                  v BATE Borisov
Bayern Munich v Valencia
  
Kundi G
Barcelona        v Spartak Moscow
Celtic               v Benfica
  
Kundi H
Man U             v Galatasaray
Braga              v CFR Cluj

No comments:

Post a Comment