STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, September 19, 2012

SIMBA, YANGA MAJARIBUNI TENA LEO


KINYANG'ANYIRO Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea leo kwa michezo ya raundi ya pili ambapo mabingwa watetezi, Simba na watani zao Yanga watakuwa kwenye viwanja viwili tofauti kujaribu tena bahati yao katika ligi hiyo.
Jumla ya mechi saba zinatarajiwa kuchezwa kwenye ambapo kwenye dimba la Taifa, jijini Dar 'Mnyama' Simba itaikaribisha JKT Ruvu ya Pwani, wakati Yanga iliyoanza ligi kwa suluhu na timu ilipoapanda daraja ya Prisons-Mbeya, itakuwa ugenini tena uwanja wa Jamhuri, Morogoro kuumana na  Mtibwa Sugar.
Simba itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kuanza vyema katika ligi hiyo kwa ushindi wa magoli 3-0 iliopata dhidi ya African Lyon wakati mabingwa wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) Yanga wana pointi moja iliyotokana na suluhu dhidi ya Prisons mkoani Mbeya.
Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic amenukuliwa akisema kuwa kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo na anachotaka kuona wanapata pointi tatu.
Cirkovic alisema kurejea kwa mshambuliaji wake Mzambia Felix Sunzu kumekifanya kikosi hicho kuwa na ushindani zaidi wa namba katika eneo la ushambuliaji kutokana na kila mmoja kuonyesha kiwango cha juu mazoezini.
"Hakuna mechi nyepesi, ninachohitaji ni kuona tunashinda na kupata pointi tatu katika mechi hizi za kwanza ili kuondoa wasiwasi katika mechi za mwishoni mwa ligi, kikosi changu kimekamilika," alisema kocha huyo raia wa Serbia.
Charles Kilinda, kocha wa JKT Ruvu, aliliambia gazeti hili kuwa timu yake imejiandaa vyema na mechi zote za ligi na si kwa ajili ya kuikabili Simba tu.
Kilinda alisema kwamba anafahamu mchezo huo utakuwa na ushindani huku akisikitika kumkosa mshambuliaji wake mpya, Mussa Hassan 'Mgosi' ambaye hajapata kibali chake cha Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kutoka katika timu ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo ameichezea msimu mmoja uliopita.
Akiondoka bila ya mshambuliaji, Jerry Tegete na Rashid Gumbo, kocha wa Yanga, Tom Saintfiet, alisema kwamba mchezo wa leo dhidi ya Mtibwa Sugar utakuwa na upinzani mkubwa.
Hata hivyo, Saintfiet aliahidi kupata matokeo mazuri katika mchezo huo na kurejesha furaha kwa mashabiki wa Yanga.
Kocha huyo amemjumuisha kiungo wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima licha ya kuwa mgonjwa.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime aliliambia gazeti hili kwamba wachezaji wake wamejiandaa vyema kushinda na hatimaye kutorudia makosa yaliyojitokea wakati wanaivaa Polisi Morogoro katika mechi ya kwanza ya ligi iliyoisha kwa sare ya 0-0 pia.
Michezo mingine ya leo ni pamoja na pambano la African Lyon dhidi ya Polisi Moro utakaochezwa  kwenye Uwanja wa Chamazi jijini, Ruvu Shooting itashuka kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi kuikabili Mgambo Shooting ya Tanga na  Prisons itaikaribisha Coastal Union ya Tanga kwenye dimba la Sokoine jijini Mbeya.
JKT Oljoro ya Arusha baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Toto Afrika katika mechi yake ya awali itakuwa Kaitaba, Kagera kuumana na wenyeji wao Kagera Sugar, huku Azam iliyochanua katika pambano la fungua dimba mbele ya Kagera itaalikwa na Toto Afrika katika uwanja wa CCM Kirumba.
Kocha wa Toto, John Tegete ameapa kupata ushindi leo ili kujiongezea hazina ya pointi katika ligi hiyo aliyokiri ni ngumu kwa namna timu zilizvyojiandaa.

No comments:

Post a Comment