MPIGAPICHA mkongwe nchini wa gazeti la Tanzania Daima, Joseph
Senga, ni kati ya walioshuhudia tukio la kuzingirwa, kuteswa hadi kuuawa
kinyama na askari wa Jeshi la Polisi kwa mwandishi wa habari wa Kituo
cha Televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi hapo
Septemba 2, katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa.
Senga, kati ya wapiga picha maarufu na wakongwe nchini waliopita
katika magazeti mbalimbali, anayefanya kazi hiyo kwa takribani miaka 28
sasa, anasimulia aliyoyashuhudia siku hiyo wakati akitimiza wajibu wake.
Kubwa zaidi, Senga anasema ameweza kupata picha nyingi za ukatili huo
uliofanywa na askari polisi dhidi ya Mwangosi, kuanzia kukamatwa kwake,
kupigwa na kuteswa kabla ya kuelekezewa bunduki ya mdomo mpana katika
tumbo na kuukatisha uhai wake.
Katika mahojiano maalumu, Senga anasema tangu kutokee mauaji yale ya
kinyama ambayo yangeweza kumtisha yeyote yule kutokana na kufanywa na
askari polisi wenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao,
mengi yamezungumzwa.
Anasema kinachomsikitisha zaidi, ni kitendo cha baadhi ya waandishi
kuibuka na kudai kuwa sio tu walikuwepo karibu ya tukio hilo, pia ndio
waliopiga picha zikionesha mauaji hayo ikiwemo ile ya askari
aliyeelekeza mtutu tumboni kwa Mwangosi.
Senga anasema kwake haoni fahari yoyote kujitwika jukumu hilo la
kuueleza umma kuwa alikuwa hatua chache tu wakati Mwangosi anafanyiwa
unyama ule na askari polisi, bali ameamua kuweka sawa ili kuepuka
upotoshwaji wa tukio hilo la kikatili lililogharimu uhai wa Mwangosi.
Anasema ameamua kufanya hivyo baada ya kubaini kuwa kupitia tukio hilo
lililogusa wengi, baadhi ya watu ambao hawakuwepo kwenye eneo
alilosulubiwa Mwangosi hadi kuuawa, wamejitwisha ushuhuda wa tukio hilo
na kusema ni hatari kuleta maigizo kwenye tukio nyeti kama hilo.
Senga anasisitiza kuwa amekuwa kimya kuhusu jambo hilo, lakini baada
ya kushauriwa na watu wenye busara wakiwamo wakuu wake wa kazi, akaona
aeleze kilichotokea kuweka mambo sawa, japo hakutaka kwani hakuona ni
tukio la kujipatia sifa isipokuwa simanzi isiyofutika haraka machoni.
Anasema licha ya kuifanya kazi hiyo kwa miaka yote hiyo na kuwahi
kukumbana na kadhia nyingi, lakini mazingira ya kuuawa kwa Mwangosi,
hatayasahau kamwe katika maisha yake yote atakayojaaliwa na Mwenyezi
Mungu.
“Jamani tukio la kuuawa kwa Mwangosi linatisha. Wakati anaburutwa,
kupigwa, kuteswa na kundi la askari, usingeweza kusema ni mwandishi wa
habari, pengine ungeweza kusema ni kibaka au jambazi, hakuwa na muda wa
kujihami zaidi ya kusema ‘mnaniua mimi ni mwandishi’,” anasema Senga.
Anasema alishangazwa namna askari polisi walivyokuwa wamempania
Mwangosi kwani alikumbana na mateso hayo akiwa na kamera mkononi na
mkoba mdogo begani kwake, kuashiria hakuna kilichompeleka Nyololo,
isipokuwa kutimiza wajibu wake.
Senga anasema cha kushangaza zaidi ni kuona askari wale walivyokuwa
wamejawa na jazba iliyowafanya wampuuze hata bosi wao (aliyemkumbatia
Mwangosi), ambaye licha ya kuwaeleza wamwache, wasiendelee kumtesa kwani
anamjua, wakazidi kumshambulia wakati huo Mwangosi akijitetea na
kuwasihi wamwache bila mafanikio.
Katika mazingira hayo, Mwangosi akiwa amezingirwa na askari kama nane
hivi akiwemo mtetezi wa mwandishi huyo, na askari ambaye alikuja
kujulikana jina lake baadaye kuwa ni Pacificus Cleophace Simon (G2372),
akiwa karibu mno akaelekeza mdomo wa bunduki tumboni mwa mwandishi huyo
na kumlipua.
Mbali ya kuusambaratisha mwili wa Mwangosi, alimjeruhi pia eneo la
mapaja askari yule aliyekuwa akimtetea Mwangosi (OCS Mwampamba).
Kinachosikitisha zaidi, ni kwamba wakati wote huo askari wakimtesa
Mwangosi, Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Iringa, Michael Kamuhanda,
alikuwepo mita chache tu kutoka kwenye tukio, akiwa kwenye gari yake
(angalia picha namba 7).
Kabla ya Mwangosi kupigwa bomu, mwandishi wa Tanzania Daima, Abdallah
Hamis alimfuata Kamuhanda aliyekuwa ndani ya gari yake iliyofungwa vioo
(pengine kuogopa moshi wa mabomu) na kuhoji vipi askari wanamsulubu
Mwangosi?
Alichofanya Kamuhanda, ni kumpuuza Abdallah na alipoona anazidi
kusumbuliwa, akashusha kioo kumsikiliza, lakini hakujibu kitu zaidi ya
kufunga kioo na kutoa picha kuwa, alichokuwa akifanyiwa Mwangosi ni
agizo lake au ni malipo aliyostahili kwa siku ile.
Senga anasema kwa kulishuhudia kwa macho yake tukio hilo la kinyama
lililokatisha uhai wa Mwangosi, kamwe hataweza kulisahau kutokana na
kufanywa katika mazingira ya kutisha na kuogofya huku yeye akipiga picha
za kuteswa hadi kuuawa kwa bomu kikatili.
Mwanahabari huyo mkongwe amebainisha kuwa, katika tukio hilo aliweza
kupiga picha karibia zote zilizotumika kwenye vyombo mbalimbali vya
habari vya ndani na nje, yakiwemo magazeti na hata televisheni, kubwa
zaidi zikipingana na hila za Jeshi la Polisi kutaka kupindisha ukweli wa
mambo.
Ikumbukwe, jioni ya siku ya tukio, Kamanda Mkuu wa Operesheni na
Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, bila hata hofu ya Mungu ndani
yake, akaanza kudai eti kabla ya kutokea mlipuko wa bomu, Mwangosi
alitokea upande wa wafuasi wa CHADEMA. Ni aibu na hatari kubwa kwa
taifa.
Mazingira kabla ya kifo
Senga anasema asubuhi ya siku ya tukio, waandishi wa habari
walialikwa katika mkutano na Kamanda Kamuhanda ambao ulifanyika ofisini
kwake, mjini Iringa, yeye akiwa mmoja wao.
Anasema ulikuwa ni mkutano wa kutoa tamko la kuzuia mikutano ya
kisiasa, lakini hususan iliyokuwa imepangwa kufanywa na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kilikuwa kinaendelea na
mikutano yake mkoani humo baada ya kutoka Morogoro.
Polisi walitaka kusitishwa kwa mikutano hiyo kutokana na kile
kilichoelezwa kuongezwa kwa muda wa zoezi la sensa kwa siku saba zaidi,
baada ya zile siku saba za kwanza kumalizika huku lengo lililokuwa
limekusudiwa kutotimia.
Senga anasema baada ya mkutano huo, waandishi walitaka kujua upande wa
pili yaani CHADEMA, hivyo walielekea walikokuwa ambako nako kulifanyika
mkutano na waandishi wa habari ukiongozwa na Katibu Mkuu wa chama
hicho, Dk. Willibrod Slaa.
Baada ya zuio la mkutano
Senga anasema CHADEMA walitoa tamko wakilaumu utendaji wa Jeshi la
Polisi kwa madai kuwa, lilikuwa likifanya kazi zake kwa kuongozwa na
matakwa ya wanasiasa hususan wa chama tawala (CCM), lakini walisitisha
mikutano yao japo kwa shingo upande.
“Katika mkutano wa waandishi wa habari na Kamanda Kamuhanda,
yalijitokeza maswali mengi likiwemo la mikutano ya ndani iliyokuwa
ikifanywa na CHADEMA, wakati wa zoezi la sensa likiendelea kabla ya
kuongezwa zile siku saba, ambalo lilijibiwa na kamanda huyo, kwamba
mikutano hiyo inaruhusiwa,” anasema Senga na kuongeza:
“Uongozi wa CHADEMA uliamua kuendelea na mikutano ya ndani ikiwa ni
pamoja na kufungua matawi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa
katika kila jimbo, wakati wakisuburi kumalizika kwa sensa ya awamu ya
pili.”
Ufunguzi wa matawi
Senga anasema baada ya hapo ndipo Chadena wakajipanga kwenda kufanya
zoezi hilo mchana wa siku hiyo kufungua matawi katika kijiji cha Nyololo
kwa kuteua viongozi wawili kuongoza zoezi hilo bila kumshirikisha
Katibu Mkuu, Dk. Slaa.
“Nakumbuka walipangwa viongozi wa kuendesha zoezi hilo akiwemo Naibu
Katibu (Zanzibar), Hamad Yusuf na Kamanda wa Operesheni hiyo, Benson
Kigaira. Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa hakushiriki kabisa siku hiyo,
alibaki hotelini,” anaongeza Senga.
Mwangosi anasita kwenda katika ufunguzi
Wakati wa maandalizi ya kwenda katika ufunguzi wa matawi, Senga
anasema Mwangosi alimwambia asingekwenda katika hafla hiyo kwa kuwa
hakuona tena kama kungekuwa na habari kwani ilikuwa ni mikutano ya ndani
tu.
Anasema kama ilivyo kawaida kwa wanahabari, kunusa na kutafuta habari
zilipo, zilizagaa taarifa kuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia
(FFU), walikuwa wamemwagwa katika eneo ambalo CHADEMA wangefungua matawi
katika kijiji hicho.
Kwa taarifa hizo, wanahabari wengi wakatamani kwenda kushuhudia
ufunguaji huo wa matawi (akiwemo Mwangosi), pasipo kujua kuwa kumbe yeye
ndiye anakwenda kuwa habari iliyotikisa nchi.
“Ni kweli ndivyo ilivyokuwa, baada ya kufika katika Kijiji cha
Nyololo, tulikuta maandalizi yamekamilika, askari hao wakiwa na silaha
za kila aina. Nilijua ni kazi yao pengine walipewa maelekezo ya
kuwalinda viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA wakati wakifungua
matawi yao ili kuwahakikishia usalama wao,” anasema Senga.
Hata hivyo, anasema fikra zake hizo zilianza kupotea baada ya kuanza
kutolewa amri na viongozi wa Jeshi la Polisi wa mkoa huo, wakiongozwa na
RPC Kamuhanda na RCO ambao kwa nyakati tofauti walionekana
kutofautiana, mwingine akikubali kufanyika kwa zoezi hilo kwa vile
halikuwa na madhara na mwingine akitaka kusitishwa.
Kwa mujibu wa Senga, CHADEMA walifanikiwa kufungua tawi la kwanza
wakiwa wamezingirwa na askari, lakini hali ilibadilika wakati wakifungua
tawi la pili ambako polisi walianzisha mapambano dhidi ya viongozi,
wanachama na wafuasi wa chama hicho.
“Nasema leo hatutapiga mabomu, tutakamata viongozi, wakamateni
viongozi wote wa CHADEMA,” anasimulia Senga alivyosikia amri kutoka
kinywani mwa RPC alipokuwa akiwaamuru askari wake kutekeleza amri hiyo.
Senga anasema kabla amri hiyo haijatekelezwa, ghafla yakaanza
kulipuliwa mabomu ya machozi kutoka kwa askari polisi kwa lengo la
kuwatawanya wana-CHADEMA waliokuwa nje ya ofisi hizo.
Wakati mgumu kwa wanahabari
Anasema viongozi hao walitawanyika huku hata wasio viongozi
wakakimbia kusikojulikana. Hapo ndipo wakati mgumu ulipoanzia kwa
wanahabari, kwa kubwia moshi mzito wa mabomu yaliyolipuliwa katika kila
kona ya eneo hilo.
Kama vile hapakuwa na tukio la kulipuliwa kwa mabomu, Senga anasema
baadaye utulivu ulirejea, lakini wakati huo hakukuwa na mwananchi hata
mmoja akipita katika maeneo hayo, isipokuwa askari tu na baadhi ya
waandishi wa habari.
Senga anasema aliendelea kutekeleza majukumu yake akiamini kuwa kwake
mbele ya askari wale ni hakikisho la usalama ingawa baadhi yao
walishaanza kuondoka baada ya kukamilisha kazi yao, wakitembea na mbele
yao kukiwa na magari matatu yakielekea barabara kuu ya Dar es Salaam -
Mbeya.
Mwangosi anaanza kusulubiwa
Anasema wakiwa katika msafara huo, ghafla aliona mtu akishambuliwa
kwa kipigo na askari hao waliokuwa mbele yake, akashtuka na kujiuliza ni
nani na kwa sababu gani kwani hali ya mambo tayari ilikuwa tulivu.
“Mmoja wa askari hao aliingilia kati na kumkumbatia, akiwazuia askari
wenzake wasiendele kumpiga akisema: “mwacheni namfahamu ni mwandishi,
acheni jamani,” akijaribu kuokoa uhai wa mtu huyo ambaye wakati huo
miguu yake ilikuwa katikati ya miguu ya askari yule msamaria. Wakati huo
akionekana kuishiwa nguvu kwa kipigo kikali,” anasema Senga.
Anasema licha ya jitihada kubwa za askari yule msamaria mwenye nyota
tatu mabegani mwake kuwazuia wenzake wasiendelee kumpiga, bado kundi la
askari wale waliendelea kumpa kipigo. Baadaye alimtambua kwa ukaribu
kuwa alikuwa ni Daudi Mwangosi.
Wakati hayo yakiendelea, Senga anaeleza kuwa, akili yake ilimkumbusha
kuwa alikuwa kazini, hivyo pamoja na huruma ya kuguswa na unyama ule,
pia akapaswa kuchukua picha za tukio hilo bila kujali kitu gani
kingempata kutoka kwa askari wale wenye hasira iliyopitiliza.
Anaongeza kuwa, ghafla mmoja wa askari hao alimkaribia na kumshika
mkono kabla ya wengine wawili kuongezeka, wakamzonga sana, wakati huo
Mwangosi akiendelea kusulubiwa.
“Tukupeleke pale na wewe?” lilikuwa swali kutoka kwa askari hao kwa
Senga, akimaanisha pale alipokuwa akisulubiwa Mwangosi. Senga anasema
wakati huo hakuwa na jibu la haraka.
Mwangosi alipuliwa
Senga anasema wakati askari hao wakiwa bado wanamsulubu Mwangosi,
ghalfa akasikia mlipuko mkubwa na kwa macho yake, akashuhudia wale
askari waliokuwa wamemzingira wakatawanyika kwa taharuki.
Anasema baadhi yao walionekana wakielekea kwenye magari yaliyokuwa
mbele, wakati huo Kamanda Kamuhanda akiwa umbali kama wa mita tano hivi
ndani ya gari yake iliyokuwa imefungwa vioo vyote.
Senga anasema baada ya mlipuko ule alichoweza kushuhudia ni nyama
zilizosambaa huku kando yake akiwepo askari (yule aliyekuwa akimtetea
kabla ya kulipuliwa kwake), akiwa amejiinamia kando ya mabaki hayo ya
mwili wa Mwangosi, naye akiwa amejeruhiwa sehemu ya paja la kushoto.
Anasema tukio hilo lilimfanya abaki ameduwaa kwa dakika chache asijue
la kufanya, kwani ni mara yake ya kwanza kuona unyama na ukatili wa
kiwango hicho, tena ukifanywa na askari polisi kwa mtu asiye na silaha
yoyote zaidi ya begi na kamera mkononi mwake.
“Swali kubwa ambalo nilijiuliza moyoni mwangu, ni kama kweli
nilichokuwa nikishuhudia mbele yangu ulikuwa mwili wa Mwangosi,” anasema
Senga.
Katikati ya swali hilo, Senga anasema akakumbuka kuwa yu kazini, hivyo
akaendelea kupiga picha za mabaki ya mwili wa Mwangosi, wakati huo
kando yake akiwepo yule askari aliyekuwa akilia kwa uchungu akisema,
“Afande wameniua.” Pengine akimweleza Kamuhanda aliyekuwepo karibu.
Anasema baadaye Kamuhanda akiwa ndani ya gari lake karibu na eneo la
tukio, aliwaamuru askari warudi kumchukua askari yule majeruhi, hivyo
wakarejea na kumbeba wakimweka kwenye gari.
Senga anasema dakika hizo chache kilikuwa ni kipindi kigumu sana
kwake, akibaki eneo hilo ameduwaa, akiangaza macho mbele na nyuma kwani
wakati huo hakuona raia wa kawaida zaidi ya askari.
Anasema katikati ya butwaa hiyo, ufahamu ukaanza kumrejea kuwa
kilichokatisha uhai wa Mwangosi kwa kuusambaratisha mwili wake, si
risasi ya kawaida pengine ni mlipuko wa bomu kutokana na ukubwa wa
kishindo chake.
Senga anasema baada ya tafakuri hiyo, hofu ya kibinadamu ikaanza
kumpata, akijiona kuwa kumbe hata yeye hakuwa eneo salama kwake,
akatamani kujificha kutokana na hofu kubwa aliyokuwa nayo.
Anasema alichofanikiwa kufanya baada ya kurudi katika hali ya kawaida,
alirejea nyuma kama mita hamsini na kuuona ua uliojengwa kwa magome ya
miti, akajibanza hapo huku machozi yakimtiririka akimlilia Mwangosi na
kuongeza kuwa, hakuwa tena na hamu wala nguvu ya kushika kamera.
“Bado sikuamini na kuridhika na nilichokishudia kwa macho yangu
mawili, niliendelea kuchungulia kujua nini kitaendelea. Ilichukua
takribani dakika 15, askari hao wakikusanya mabaki ya mwili wa Mwangosi
kwa kutumia ngao zao na kupakiza katika moja ya magari yao,” anaongeza.
Anasema baada ya zoezi hilo askari hao waliondoka, wakiwa ndani ya
magari pamoja na baadhi ya viongozi, pia baadhi ya wafuasi waliokuwa
wamewakamata kabla ya kuuawa kwa Mwangosi, wakielekea kusikojulikana.
“Mwenyezi Mungu ailaze pema roho ya marehemu Mwangosi. Amina,” anamaliza Senga.
|
Moja ya picha iliyopigwa na Senga ikionyesha askari Polisi (FFU) wakiwa kamili na zana zao |
CHANZO:GAZETI LA TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment