Sharo Milionea enzi za uhai wake |
Kwa mujibu mjomba wa marehemu, Omar Fundikira, Sharo atazikwa nyumbani kwao katika kijiji cha Lusanga wilayani Muheza mkoani Tanga.
Sharo alifariki dunia alifariki kufuatia ajali ya gari iliyotokea eneo la Maguzoni, Songa, Muheza.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa mkoa wa Tanga, Constatine Masawe, Sharo alikuwa peke yake garini wakati ajali hiyo ikitokea na mwili wake uko katika hospitali ya Teule, Muheza.
Kamanda Masawe alisema Sharo akiwa anaendesha gari namba T478 BVR Toyota Harrier akitokea Dar es Salaam kwenda Muheza na alipofika eneo hilo gari lake liliacha njia na kupinduka mara kadhaa na kusababisha kifo chake.
Taarifa za kifo chake kilianza kuzagaa kwa watu kutumiana ujumbe wa simu kabla ya kuthibitishwa na Kamanda Constantine.
Umati wa watu ulikusanyika katika hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza kujaribu kuushuhudia mwili wa muigizaji huyo aliyepata umaarufu mkubwa kutokana na vibwagizo vyake vya "Umebugi meen!", "kamata mwizi meen!" na "Ooh mamma!"
Mwandishi wetu ambaye alifika katika chumba cha maiti katika hospitali hiyo alishuhudia umati wa watu ukisubiri kuingia ndani ya chumba hicho kuuona mwili wa msanii huyo aliyeumia vibaya kichwani na kifuani.
Kutokana na hali hiyo mhudumu wa chumba cha maiti aliyejitaja kwa jina la Mhusa na daktari wa hospitali hiyo aliyejitaja kwa Kibaja walipata wakati mgumu kuwazuia watu waliofurika wakiwamo wanafunzi wanaosomea udaktari katika hospitali hiyo.
Baadaye mwandishi wetu alifika nyumbani kwa marehemu katika kijiji cha Lusanga ambapo alikuta vilio kutoka kwa ndugu na jamaa huku umati wa watu ukiwa umefurika nyumbani hapo pia.
Miongoni mwa wasanii waliokuwapo nyumbani hapo akiwamo mkongwe aliyekuwa akifanya naye kazi nyingi, Amri Athuman maarufu King Majuto, alisema kuwa amesikitishwa mno na msiba huo.
Majuto alisema anakosa maneno ya kusema kutokana na ukubwa wa msiba huo kwake kwa kumpoteza kijana aliyemsifu kuwa ni mchapakazi aliyekuwa na usongo wa mafanikio.
Mkogwe huyo huyo alisema kifo cha Sharo ni pigo kwa wasanii wote hususan yeye mwenyewe ambaye alikuwa ni meneja wake katika kazi zao za kila siku.
“Kusema kweli sioni wa kuziba pengo hili… ni mtu ambaye nilimzoea sana na sijui ni kipi cha kusema ila Mwenyezi Mungu anajua zaidi yetu,” alisema Majuto.
Rambirambi pia zilitoka katika serikali wilayani Muheza ambapo ilisema imeshtushwa mno na kifo cha Sharo kutokana na umahiri wake na kuifanya kazi ya usanii kuwa ajira kama zilivyo ajira nyingine.
Mkuu wa wilaya ya Muheza, Subira Mgalu alisema kuwa kimsingi msanii huyo amekuwa mfano wa kuigwa na wasanii wengine nchini kutokana na kuithamini na kuipenda kazi yake na hivyo kuwa mbunifu siku hadi siku.
"Kwa kweli marehemu Sharo alikuwa ni mbunifu katika kazi yake na aliifanya sanaa kuwa ni ajira kama zilivyo ajira nyingine, kweli huu ni mfano wa kuigwa na vijana na kupitia yeye wengi wameweza na wanaweza kujitambua kuwa wana vipaji ambavyo wakivitumia vitawaondoa katika umasikini. Inasikitisha kwamba ametutoka mapema sana kipindi ambacho wapenzi wa sanaa na watoto walishamzoea kumwona na kumsikia," alisema Mgalu.
Naye mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, alisema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa msanii huyo.
Katika taarifa yake iliyotolewa na afisa habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, Rage alisema kwa niaba ya klabu ya Simba na kwa niaba yake binafsi, anapenda kutuma salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote wa marehemu kwa kuwa na msiba huu ni mkubwa sana si kwao pekee bali kwa taifa zima la Tanzania.
Taarifa hiyo ilisema: "Sharo Milionea hakuwa msanii wa kawaida. Yeye ni miongoni mwa kizazi kipya cha vijana wa Kitanzania walioamua kutafuta maisha kwa kutumia vipaji walivyopewa na Mungu. Yeye alijitumbukiza zaidi katika uchekeshaji na baadaye akaonyesha uwezo mkubwa katika fani ya muziki.
"Sharo alikuwa maarufu kiasi kwamba makampuni makubwa yalikuwa yameanza kumtumia kwenye matangazo yao ya kibiashara. Hii ilionyesha kwamba makampuni yalibaini faida itakayopatikana kwao kwa kumtumia msanii huyu ambaye bado alikuwa na heshima kubwa kwenye jamii kutokana na haiba yake na uwezo wake kwenye kazi alizokuwa akifanya.
"Msiba huu umekuwa pigo kubwa kwa tasnia ya filamu ambayo bado inaomboleza vifo vya wasanii kama Steven Kanumba, Mlopelo na John Steven Maganga, waliofariki dunia mwaka huu pia.
"Ifahamike kwamba Sharomilionea alikuwa miongoni mwa wasanii wa Kitanzania waliotuma maombi Simba ya kutaka kushiriki kwenye mchakato wa kutengeneza wimbo rasmi wa klabu ya Simba. Yeye alikuwa miongoni mwa wasanii waliokuwa wakiumizwa na ukweli kwamba klabu kama Simba inashindwa kufanya biashara ya kuuza nyimbo zake ilhali wanunuaji wapo."
Taarifa hiyo iliendelea: "Kwa klabu ya Simba, namna pekee ya kumuenzi marehemu ni kufanyia kazi mambo ambayo alikuwa akitushauri kwenye eneo la biashara. Ni matumaini yetu kwamba iwapo tutafanya lile alilokuwa akitushauri, atakuwa mwenye amani huko alikotangulia mbele ya haki."
Aidha, Rage amewaomba wasanii wa tasnia ya filamu na muziki kuwa watulivu na wenye subra kwenye kipindi hiki kigumu kwao akisema kila kitu katika maisha ya wanadamu kinapangwa na Mwenyezi Mungu na ndiyo maana Waswahili wana msemo kuwa Kazi ya Mungu haina makosa.
ALIIBIWA KILA KITU
Watu wasiojulika waliiba kila kitu kutoka kwa msanii huyo baada ya kupata ajali ya gari na kufariki papo hapo.
Wezi hao walimuibia msanii huyo vitu vyote na kumbakisha na pensi ya ndani ambayo alikutwa nayo na polisi katika sehemu ya tukio akiwa tayari ameshakufa.
Ripoti zinasema kuwa baada ya kufa, vibaka wa eneo hilo la kijiji cha Maguzoni walimuibia viatu, mkufu, nguo, fedha.
Wakizungumza na NIPASHE mashuhuda katika eneo la tukio walisema kuwa walisikia kishindo kikubwa cha gari hiyo kuanguka kabla ya vijana ambao hawakutambulika kulivamia na kuanza kupora bila ya kutoa msaada kwa msanii huyo hadi watu walipojaa na kusaidia.
Hii ni ajali ya pili kwa Sharo kupata mwaka huu baada ya Januari 5 kunusurika katika ajali ya basi alilokuwa amepanda likitokea Burundi kuelekea Dar es Salaam kupinduka katika eneo Mikese, Morogoro saa 2:30 asubuhi.
Sharo ambaye alikuwa amekaa kwenye siti ya mbele kabisa alipoteza simu tu katika ajali hiyo ambayo ilijeruhi abiria wengine vibaya.
Kifo cha Sharo kinafuatia vifo vya wasanii wengine wawili wa filamu nchini ndani ya wiki moja, Mlopelo aliyetamba na kundi la Kaole na John Maganga aliyetamba na filamu ya 'Mrembo Kikojozi' aliyocheza na Aunt Ezekiel. John Maganga alizikwa jana mchana kwenye makaburi ya Kinondoni. Vifo hivyo pia vinakumbushia msiba wa Steven Kanumba, ambaye pia alifariki ghafla mwaka huu pia katika kilichodaiwa kuwa ni ugomvi wa kimapenzi.
Sharo atakumbukwa kwa ubunifu wake katika uigizaji akitoka kama mchekeshaji msafi tofauti na wachekeshaji wengi waliomtangulia ambao waliamini vichekesho ni lazima kuvaa kama katuni, kujaza nguo tumboni ili kuonekana na matumbo makubwa ama kujipaka masizi.
Akipendeza kwa mavazi nadhifu, Sharo Milionea alipata umaarufu kwa msemo wake wa "kamata mwizi meeen" na "Ooooh mamma!" huku akijipangusa mabega katika pozi za 'kibrazameni'.
Katika siku za karibuni amekuwa akitawala vioo vya televisheni kutokana na kushiriki tangazo la kampuni ya huduma za simu ya Airtel akiwa na mchekeshaji mkongwe King Majuto, ambapo msemo wake mwingine wa "umebugi meen!" umetawala hasa midomoni mwa watoto.
Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mbando, alisema jana kuwa wameshtushwa na kusikitishwa na kifo cha ghafla cha Sharo ambaye waliingia naye mkataba hivi karibuni ili kutangaza huduma za kampuni hiyo.
"Tunaungana na familia, ndugu na jamaa na wadau wa burudani kutokana na kifo cha Sharomilionea. Alikuwa ni kijana mdogo, mchangamfu na aliyekitumia vema kipaji chake cha sanaa na tulikuwa bado tunamtegemea," alisema Mbando.
Wasanii wengine waliowahi kufanya kazi na msanii huyo walisema kuwa wanashindwa kuamini kama amefariki.
Mchekeshaji mwenzake maarufu kwa jina la Kitale alisema siku tatu zilizopita alipigiwa simu na Sharo akimtaka aende nyumbani kwake.
"Nilipofika akaniambia hii ni 'suprise' huku akinionyesha ufunguo wa gari, aliniambia amenunua gari mpya na akanipa Sh.200,000 huku akiniambia kwamba kuna 'dili' ameniunganishia ya kwenda naye nje ya nchi kufanya kazi ya sanaa," alisema Kitale.
Muigizaji Masai Nyota Mbofu alisema itamchukua muda mrefu kumsahau Sharo aliyetamba naye kwenye filamu na kipindi cha 'Vituko Show' wakati wakiwa katika kampuni ya Al Riyamy.
Naye mtayarishaji wa filamu nchini Mustafa Wazir 'West' alisema atamkumbuka daima kwa kipaji Sharo wakati mchekeshaji mwingine aliyekuwa akiigiza na Sharo, Ally Boffu 'Man Bizo', alisema hadi sasa haamini kama amefariki.
VIPAJI TELE
Sharo alikuwa ni msanii mwenye vipaji vingi na aliyejitambulisha pia kama "bonge la rapa" na muimbaji wa Bongofleva.
Baada ya kukosa mafanikio kwa nyimbo zake za awali za awali kabisa za 'Nahesabu Namba' na 'Tusigombane', Sharo ambaye alianza sanaa ya kikazi kipya tangu mwaka 2004, alirekodi nyimbo nyingine za 'Tembea Kisharobaro', aliurekodi katika studio ya Andrew Music ya jijini Tanga na 'Sondela' alioupika katika studio ya Ally's Records ya Tanga pia.
Aliiambia NIPASHE katika mahojiano enzi za uhai wake kwamba pamoja na kumudu miondoko mbalimbali ya muziki kama kwaito, hip hop, na kadhalika, aliamua kugeukia kuimba.
"Nimeamua niimbe kwa sababu naona wengi wananikubali zaidi ninapoimba," alisema msanii huyo ambaye aliliacha jina la Sharobaro na kuhamia Sharomilionea.
CHANZO CHA SHARO-MILIONEA
Wakati akianza sanaa yake ya ucheshi, msanii huyu alijiita Sharobaro, jina ambalo pia ni la studio ya kurekodi muziki inayomilikiwa na msanii na mtayarishaji wa muziki, Bob Junior, aliyemtoa msanii Diamond Platinumz.
Lakini baada ya kilichoripotiwa kuwa ni bifu baina yake na Bob Junior, msanii huyo aliliacha jina la "Sharobaro" na kuanza kujiita "Sharo Milionea".
"Sina ugomvi na Bob Junior, ila watu wa pembeni ndio waliokuwa wakiongea vibaya kutaka kutugombanisha, ndio maana nikamweleza kwamba ni vyema nibadili jina, ndo nikaanza kutumia Sharomilionea, lakini hatuna ugomvi," alisema Mkieti katika mahojiano na NIPASHE wakati wa uhai wake.
Alitamba katika filamu kadhaa za ucheshi ikiwamo ya 'Sharobaro' na 'Mtoto wa Mama', ambamo alitoa msemo wake uliompa umaarufu mkubwa wa "kamata mwizi meeen" pale alipoibiwa simu na kibaka, ambapo badala ya kumkimbiza alionyesha kwamba yeye "brazameni" hawezi kukimbiza mwizi hiyo akiwataka wengine wamsaidie huku akitoa msemo huo.
Baadaye alitamba katika filamu ya kampeni ya kupambana na malaria ya 'Chumo' akiigiza pamoja na Yusuph Mlela na Jokate Mwegelo ambayo ilikuja baada ya filamu yake nyingine ya ucheshi ya 'Back From New York', ambamo aliigiza kama kijana aliyerejea kutoka Marekani na kujumuika na baba yake (wa maigizo) King Majuto, ambaye naye akamgeuza kuwa 'mzee Sharobaro' anayevaa 'kibrazameni' na anayetemba huku akidunda kama vijana wa mjini.
Sharo Milionea enzi za uhai wake akiwa kapigilia kanzu |
No comments:
Post a Comment