Wachezaji wa timu ya Kilimanjaro wakitania kwenye mazoezi ya timu yao, ambapo jioni ya leo inavaana na Burundi |
Na Somoe Ng'itu, Kampala
WAKATI wenyeji Uganda jana walikuwa wa kwanza kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Chalenji baada ya kushinda 1-0 dhidi ya Ethiopia, timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) itatupa karata yake ya pili katika mechi ya kundi B dhidi ya Burundi leo.
Goli pekee kutoka kwa Brian Umony liliwafanya Uganda kufuzu baada ya kufikisha pointi sita katika kundi A, huku Kenya ambayo ilishinda 2-0 mapema jana dhidi ya Sudan Kusini ikishika nafasi ya pili baada ya mechi mbili. Ethiopia pia ina pointi tatu lakini iko katika nafasi ya tatu kutokana na tofauti ya magoli. Katika mechi ya kwanza Uganda ilishinda 1-0 dhidi ya Kenya, wakati Ethiopia iliifunga Sudan Kusini 1-0 katika siku ya ufunzi wa michuano hiyo inayofanyika kwenye Uwanja wa Namboole hapa Kampala.
Baada ya kushinda 2-0 dhidi ya Sudan katika mechi ya ufunguzi, Kilimanjaro Stars itashuka dimbani leo kuikabili Burundi kuanzia 12:00 jioni.
Burundi ndio kinara wa kundi hilo kutokana na kuwa na magoli mengi ya kufunga ambapo alipata ushindi wa 5-1 dhidi ya Somalia.
Akizungumza na gazeti hili jana baada ya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Makerere, Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen, alisema kwamba wachezaji wake wako vizuri na amejipanga kuikabili Burundi na hatimaye kuibuka na ushindi.
Kim alisema kwamba Burundi ni timu inayotumia nguvu lakini wachezaji wake wamejiandaa kutumia kasi waliyonayo kuwatoka wapinzani wao ambao wengi wana miili mikubwa wakiongozwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Selemani Ndikumana.
Alisema kuwa mashindano ni magumu na hakuna timu ya kuidharau hivyo amewaandaa wachezaji wake kupambana kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
"Kila mchezo tutaingia na mbinu tofauti, nimewasoma Burundi wakati walipokuwa wanacheza na Somalia...naamini tutawafunga ili tuongoze kundi letu," alisema Kim ambaye hii ni mara yake ya kwanza kufika Uganda na kuongoza timu kwenye michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea.
Aliongeza kwamba anafurahishwa na kikosi chake kucheza kwa kuelewana na anaamini kitafanya vizuri mechi zote zinazofuata na kutimiza malengo ya kurejea nyumbani na ubingwa.
Nahodha wa timu hiyo, Juma Kaseja, aliliambia gazeti hili kwamba jitihada za kila mchezaji ndiyo zinafanikisha matokeo mazuri na anaamini watasonga mbele katika hatua inayofuata.
Kaseja alisema kwamba mashindano haya yana upinzani na wao wamejiandaa kukabiliana na changamoto hiyo.
"Ni mashindano ambayo tunakutana wachezaji tunaofahamiana hasa Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda, yana ushindani na yanatufanya tujifunze zaidi kila mara, mwalimu aliiangalia Burundi hivyo ametupa maelekezo ya nini cha kufanya ili tufanye vizuri," alisema Kaseja.
Aliongeza kwamba ushindi walioupata katika mechi ya kwanza haukuwa wa kubahatisha na wanaamini mwaka huu watafika mbali.
Aliwataka mashabiki wa Tanzania waendelee kuwaombea ili wao wafanye kile walichotarajia na kurudi nyumbani na heshima.
Kilimanjaro Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) itakamilisha mechi za hatua ya makundi Jumapili kwa kuivaa Somalia kuanzia saa nane mchana kwenye uwanja utakaotajwa hapo baadaye.
Mchezo mwingine utakaochezwa leo mchana ni kati ya Somalia na Sudan ambazo zote zilipoteza mechi zao za kwanza.
No comments:
Post a Comment