Zahoro Pazi (kushoto) akiwa uwanjani akichuana na Jerry Santo aliyekuwa Simba enzi hizo |
Pazi, anayefahamika kwa jina la utani kama 'Cristiano Ronaldo', alisema kitendo kilichofanywa na Kim kuwapanga wachezaji karibu wote vijana ndio chachu ya ushindi wa mabao 2-0 iliyopata mbele ya Sudan na kuwataka watanzania wamuunge mkono kwani jambo hilo litailetea manufaa Tanzania siku za baadae.
Alisema kupewa nafasi kwa vijana kunawapa nafasi ya kupata uzoefu na kuondoka woga na hivyo kuweza kulitumikia taifa wakiwa Taifa Stars kama mashujaa wa Tanzania jambo ambalo limekuwa likililiwa kwa muda mrefu.
"Kwa kweli nimefurahishwa na uamuzi wa kocha Kim kuwapanga karibu vijana wote katika kikosi cha Kili Stars, kwani nadhani ndio chachu ya ushindi na pia italisaidia taifa kuweza kufanya vema zaidi kwani vijana hao ndio wanaoweza kuivusha Tanzania katika michuano mikubwa zaidi ya kimataifa," alisema.
Pazi, mtoto wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Idd Pazi 'Father' alisema kilichofanywa na Kim kinawatia moyo wachezaji vijana kama yeye ambao walikuwa wakipuuzwa Stars ilipokuwa chini ya Jen Poulsen aliyetimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Kim.
"Hata mimi ambaye nimekuwa nje ya timu ya taifa tangu Maximo alipoondoka nimepata moyo na kuamini nikijibidiisha naweza kurejea tena Stars," alisema.
Aliongeza kwa kuwataka Watanzania wamuunge mkono kocha huyo toka Denmark kwa madai anaonekana ni kocha mwenye mipango na maendeleo ya mbali kaa alivyokuwa Maximo hivyo aachiwe afanye kazi kwa raha zake na kwa muda mrefu ili Tanzania ivune matunda yanayoanza kuonekana.
Kilimanjaro Stars leo inatarajiwa kutupa karata yake ya pili katika michuano hiyo ya Chalenji kwa kuvaana na Burundi, ikiwa inachekelea ushindi iliyopata dhidi ya Sudan kwa mabao ya John Bocco 'Adebayor'.
No comments:
Post a Comment