Wachezaji wa Yanga wataendelea kushangilia ushindi kama hivbi kesho kwa Coastal Union? |
Na Boniface Wambura
MWAMUZI Simon Mberwa ndiye atakayezichezesha timu za Yanga na Coastal Union katika pambano lao namba 172 la Ligi Kuu Tanzania Bara inayoingia raundi ya 25 kesho kwa michezo mitano tofauti katika miji ya Dar es Salaam, Turiani, Morogoro na Mlandizi.
Licha ya kuwa tayari Yanga imetawazwa kuwa mabingwa wa VPL msimu huu (2012/2013), mechi dhidi ya Coastal Union itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni moja kati ya zitakazovuta macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu nchini.
Mechi hiyo namba 172 itachezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Said Mnonga na Charles Chambea wote wa Mtwara wakati mwamuzi wa mezani atakiwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam. Kamishna wa mechi hiyo ni David Lugenge kutoka Iringa.
Viingilio katik mechi hiyo itakayoanza saa 10.15 jioni ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 8,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mchezo.
Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa African Lyon katika mechi namba 170 itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana wa Dodoma kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. Nayo Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 7,000 uko tayari kwa mechi kati ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons. Nayo Ruvu Shooting itakuwa nyumbani kwenye uwanja wake Mabatini ulioko Mlandizi, Pwani kuikabili Oljoro JKT kutoka Arusha.