Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman.
|
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Barakael Masaki, jana aliwaeleza waandishi wa habari kuwa tukio la kijana kumchinja mama yake mzazi limetokea juzi majira ya saa 1:00 jioni katika kijiji cha Chobwe wilayani Ileje.
Alimtaja mwanamke aliyetuhumiwa kuwa ni mchawi na kisha kuchinjwa na mwanae kuwa ni Anna Panja (60) mkazi wa kijiji cha Chobwe.
Akisimulia tukio hilo, Masaki aliema kijana huyo aitwaye Michael Panja akiwa na mwenzake ambaye bado hajafahamika, walimvamia mama huyo nyumbani kwake akiwa amelala na mumewe Basale Panja (76), wakamchukua mama huyo na kumchinja shingoni kwa kutumia kisu na kusababisha kifo chake papo hapo.
Alisema baada ya kutenda unyama huo, Michael na mwenzake walitoroka na kwenda kusikojulikana.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watuhumiwa hao ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.
Aidha, alitoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wajenge utamaduni wa kufikisha malalamiko na kero zao kwa vyombo husika ili yaweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Katika tukio la pili, kundi la wananchi wenye hasira wakitumia silaha za jadi walimuua Lufingano Nsinge (32), baada ya kumtuhumu kujihusisha na matukio ya mauaji ya watoto wadogo yaliyokuwa yakitokea katika kijiji chao.
Kamanda Masaki alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 3:00 usiku katika kijiji cha Ndala, kata ya Kandete kwenye kitongoji cha Katumba wilayani Rungwe.
Akisimulia tukio hilo, Masaki alisema marehemu Nsinge siku ya tukio aliingia ndani ya nyumba ya John Mwansamaleba (53) kwa nia ya kufanya uhalifu na ndipo alipokutwa na wananchi hao.
walioamua kuchukua sheria mkononi kwa kumshambulia kwa silaha za jadi kama vile mipini, shoka, kuni na mapanga na kusababisha kifo chake papo hapo.
Alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu wanne kuhusiana na tukio hilo.
Aliwataja watu hao kuwa ni John Mwasamaleba, Angolisye Mwakalinga (30), Lukas Mwasamaleba (40) na Leah Ndemange (45), wote wakazi wa kijiji cha Ndala.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment