STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, April 24, 2013

JKT Ruvu yazishusha rasmi daraja Lyon, Toto African

JKT Ruvu waliozishusha daraja Lyon na Toto Africans

TIMU ya maafande wa JKT Ruvu wamezishusha rasmi timu za African Lyon na Toto African baada ya jioni ya leo kupata ushindi uliowavusha kwenye hatari ya kurudi Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.
Maafande hao waliokuwa wakiuguza kipigo cha mabao 3-0 toka kwa vinara wa ligi hiyo Yanga, ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Lyon katika pambano lililofanyika kwenye uwanja wa Chamazi na kuifanya kufikisha pointi 26 ambazo haziwezi kufikiwa na timu za Toto na Lyon.
Lyon na Toto zikishinda mechi zao zilizosalia katika ligi hiyo zitazifanya zifikishe pointi 25 tu na hivyo kuwa vigumu kwao kupona kwenye timu tatu za kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.
Lyon imesaliwa na mechi mbili ikiwa na pointi 19, ilihali Toto imesaliwa na mechi moja tu ikiwa na pointi zake 22, hali ambazo inazipa tiketi ya kurudi Ligi Daraja la Kwanza na kusubiri timu ya mwisho ya kuungana nao.
Miongoni mwa timu zilizopo katika janga hilo la kuzifuata klabu hizo ni Polisi Moro iliyosaliwa mechi tatu ikiwa na pointi 19, Mgambo Shootinmg yenye pointi 25 na kusaliwa na mechi mbili ikiwamo dhidi ya Simba.
Pamoja na ushindi huo wa bao 1-0 jioni ya leo bado haijaiweka salama JKT Ruvu kwani italazimika kupata ushindi kwa mechi zake mbili zilizosalia ili kuvuna pointi zaidi zitakazowatoa eneo hilo la hatari.
JKT Ruvu, Mgambo JKT, Polisi Moro na Prisons moja wapo inaweza kuungana na Lyon na Toto iwapo itazembea katika mechi zao zilizosalia.
Kipute cha ligi hiyo kitaendelea tena kesho kwa pambano moja kati ya Simba na Ruvu Shooting pambano litakalochezwa kwenye uwanja wa Taifa, kabla ya Ijumaa kushuhudiwa kipute kingine ambacho kinaweza kutangaza bingwa mpya nchini iwapo Azam itachemsha mbele ya wenyeji wao Coastal Union ya Tanga.
Pambano la timu hizo litachezwa uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga ambapo Azam italazimika kupata ushindi iwapo itataka kuwatia presha Yanga wanaosubiri kulitwaa taji hilo.
Azam wana pointi 47 na kama itashinda mechi zake tatu zilizosalia itafikisha pointi ambazo tayari Yanga imeshazikusanya ikiwa ina michezo miwili mkononi ukiwamo dhidi yua mahasimu wao Simba.

No comments:

Post a Comment