Hatari!
Ni mamilioni yatokanayo na makato U/Taifa
Viongozi wakuu wa TFF, Rais Leodger Tenga (kulia) na Angetile Osiah (kushoto) |
WIZARA inayoshughulikia michezo nchini imekuwa
ikifanya kitendo hatari cha kutuma maafisa wake kwenda kubeba mamilioni
ya fedha zitokanazo na mgawo wake utokanao na makato ya Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam bila ya ulinzi wowote ule kama taratibu za
usafirisha fedha zinavyoelekeza, imefahamika.
Aidha, malipo ya mamilioni hayo ya fedha za serikali kutoka katika
ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hufanywa kwa fedha taslim na
wala siyo kwa njia nyingine salama kama ya hundi, huku anayehusika
kuzibeba ni afisa mmoja tu ambaye ni wazi kwamba anahatarisha usalama
wake binafsi na pia wa fedha za umma.
Uchunguzi uliofanywa kwa siku kadhaa na NIPASHE umebaini kuwa
utaratibu huo unaopingana pia kwa kiasi kikubwa na taratibu za malipo ya
fedha za umma umekuwa ukifanyika kwa muda mrefu, hata kabla ya kuanza
kutumika kwa Uwanja wa Taifa.
MAMILIONI YANGA v OLJORO
Juzi (Jumapili), mwandishi alishuhudia mmoja wa maafisa wa Wizara
ya Michezo akifika katika ofisi za TFF na kubeba kienyeji (bila ya
kusindikizwa na askari yeyote mwenye silaha) kiasi cha Sh. 7,552,500
zilizotokana na asilimia 15 ya uwanja katika mapato ya mechi ya Ligi Kuu
ya Tanzania Bara kati ya Yanga na Oljoro JKT iliyochezwa Jumamosi na
kuingiza Sh. milioni 63.17.
Afisa huyo alionekana akitinga kwenye ofisi za TFF zilizopo Karume
jijini Dar es Salaam saa 4:38 asubuhi, akiwa peke yake kwenye gari aina
ya Suzuki Vitara (namba tunazihifadhi) na kuondoka peke yake pia kwenye
gari hilo mishale ya saa 5:22 asubuhi.
Kibaya zaidi, afisa huyo aliyekuwa amevaa shati la mikono mifupi
lenye rangi nyeupe, kaptula yenye mifuko mingi na viatu vya raba vyenye
mchanganyiko wa rangi nyeupe na nyeusi, hakuwa na ulinzi wowote wakati
akiingia na kutoka kwenye ofisi ya fedha ya TFF.
"Ofisi imefunguliwa leo Jumapili kwa sababu kuna mechi ya Simba
dhidi ya Azam. Ni kweli afisa wa wizara amechukua fedha za mgawo wa
uwanja. Mtafute afisa habari (Boniface Wambura) au katibu mkuu (Angetile
Osiah)... wao wanaweza kuzungumzia kwa kina sababu za uchukuaji fedha
kwa mtindo huu wa malipo ya fedha taslim," alisema mmoja wa watu
waliokutwa katika maeneo ya ofisi za TFF kwa sharti la kutotajwa jina
lake.
MAMILIONI SIMBA v AZAM
Kwa kutambua kuwa juzi kulikuwa na mechi kali ya ligi kati ya Simba
na Azam, NIPASHE ilipiga tena kambi jana asubuhi kwenye ofisi za TFF
ili kuona kama utaratibu wa kuchukua mamilioni hayo ya serikali kwa
malipo taslim utaendelea, na tena bila ya mbebaji kuambatana na askari
wa kumlinda.
Ilipofika saa 3:11 asubuhi, afisa yule yule aliyejihatarisha
Jumapili ndiye aliyetinga tena kwenye ofisi za TFF akiwa peke yake
kwenye gari lilelile aina ya Suzuki Vitara.
Mwandishi alifuatilia kwa karibu nyendo za afisa huyo. Ni kwamba,
baada ya kupaki gari lake, alionekana akisalimiana na maafisa kadhaa wa
TFF, akiwamo kocha wa timu ya taifa (Taifa Stars), Mdenmark Kim Poulsen.
IIimchukua takriban dakika 26 afisa huyo kukamilisha zoezi hilo maana
saa 3:57 asubuhi ndipo alipoingia ndani na kwenda moja kwa moja kwenye
chumba cha malipo na kubeba mamilioni yanayokadiriwa kuwa ni Sh.
7,925,600, kiasi ambacho ni sawa na asilimia 15 ya mgawo wa uwanja
kwani mechi hiyo ya Simba dhidi ya Azam iliyochezwa juzi iliingiza Sh.
milioni 66.855.
Baada ya kubeba fedha hizo, afisa huyo alionekana akifungua mlango
wa nyuma wa gari alilokuwa nalo na kuweka begi linalodhaniwa kuwa na
fedha hizo kabla ya kuondoka.
Hiyo ilikuwa ni saa 4:03 asubuhi. Mwandishi alijaribu kumfuatilia
kwa nyuma. Saa 4:07, afisa huyo aliingia ndani ya Shule ya Sekondari
Benjamin William Mkapa iliyopo umbali mfupi kutoka TFF.
Saa 4:12, afisa huyo aliondoka kwenye shule hiyo na kurejea tena
TFF na kuingia ndani ambapo akiwa na begi lake dogo lenye fedha, bila
kuwapo na ulinzi wowote, alikaa kwa dakika 23, baadaye alitoka na
kuingia kwenye gari na kuondoka saa 4:35.
TFF wanena
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu
wa TFF, Osiah alikiri kuwa serikali hutuma maafisa wake kubeba fedha
hizo kwa malipo taslim kila siku moja baada ya mechi na utaratibu huo
umekuwapo kwa muda mrefu.
"Ni kweli kwamba hata sisi tunatambua kuwa si vizuri kuwalipa pesa
taslimu, tena ni kinyume cha sheria... lakini utaratibu huo umekuwapo
kwa miaka mingi na sasa imekuwa kama desturi yetu," alisema Osiah.
Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa hata fedha za
klabu zinachukua mgawo wake kwa njia hiyo, licha ya kuwapo kwa taarifa
za tukio la kuporwa kwa Sh. milioni 10 za Simba katika eneo la Sinza
Makaburini.
MICHAEL WAMBURA
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF),
Michael Wambura alisema jana kuwa utaratibu wa TFF kutoa fedha taslimu
badala ya hundi kwa serikali ni kosa, lakini akasema kuwa imezoeleka
hivyo na kwamba hata wakati wa uongozi wao (FAT), walikuwa na mfumo huo
ambao anaamini kwamba siyo sahihi.
"Wakati tukiwa madarakani, tuliwahi kuamua kutumia utaratibu wa
hundi lakini ulileta matatizo. Kuna watu hawakutaka kabisa utaratibu
huo. Nafikiri kuna haja ya kufanya uchunguzi kujua ni kwanini hawataki
utaratibu huo," alisema Wambura.
KAMANDA WA POLISI
Alipotafutwa na NIPASHE jijini Dar es Salaam kuzungumzia taratibu
za usafirishaji wa fedha, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles
Kenyela, alisema ni kosa kwa mtu yeyote kusafirisha kiasi kikubwa cha
fedha za umma bila kuwa na ulinzi.
"Ni kosa kusafirisha fedha za umma na hata za watu binafsi
pasipokuwa na ulinzi wa polisi ama vyombo vingine vya usalama vya
serikali au kampuni za ulinzi za watu binafisi zinazotambuliwa
kisheria," alisema Kenyela.
"Inashangaza kuona TFF na wizara hawatumii utaratibu wa benki
(hundi) kulipana. Kulipana fedha taslimu, tena mamilioni ya fedha ni
kuhatarisha usalama wa fedha na watu wanaozisafirisha," aliongeza
Kenyela.
Wakati wa tukio la kudaiwa kuporwa kwa fedha za Simba baada ya
mechi yao dhidi ya Black Leopards ya Afrika Kusini iliyochezwa Desemba
29, 2012, aliwahi kuonya kuwa hivi sasa, likitokea tukio lolote la
kuporwa fedha huku wahusika wakiwa hawajaomba ulinzi, watakuwa wakianza
kwa kuwakamata watu hao
waliobeba fedha hizo kiholela.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella
Mukangara, alisema jana kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu
hakuwa katika mazingira mazuri ya kuzungumza kupitia simu kwa kuwa
alikuwa safarini kuelekea jijini Dar es Salaam.
Hivi karibuni, watu kadhaa waliuawa katika tukio la uporaji wa Sh. milioni 150
zilizokuwa zikisafirishwa bila ulinzi wa askari rasmi katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment