STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, April 21, 2013

Serikali yafafanua madai ya walimu




                          THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UFAFANUZI WA SERIKALI KUHUSU MADAI YA BWANA GRATIAN MUKOBA JUU YA MAZUNGUMZO YA SERIKALI NA CWT
____________________________________________________
            Jumanne, tarehe 09 Aprili, 2013, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bwana Gratian Mukoba, alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari, likiwamo Gazeti la Mwananchi ambalo katika Uk. 3 liliandika habari hiyo chini ya kichwa cha habari, CWT: Serikali inakaribisha mgomo mwingine.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, Bwana Mukoba alitoa madai yafuatayo:-
·        Kwamba Serikali imekataa kukaa meza moja na CWT ili kuzungumzia nyongeza ya mishahara na posho za walimu pamoja na kwamba CWT yenyewe iko tayari kwa mazungumzo;
·        Kwamba Serikali imepuuza amri ya Mahakama inayotaka pande hizo mbili kukaa meza moja kujadili madai ya walimu;
·        Kwamba kikao hasa kilichokataa kuzungumzia mishahara na posho ni kile kilichofanyika tarehe 02 Aprili, 2013 chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue;
·        Na kwamba kwa sababu ya yote hayo, Bwana Mukoba amelitaka Bunge na wazazi kuingilia kati uamuzi wa Serikali kukataa kukaa meza moja na CWT.
            Serikali inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa madai haya yote hayana chembe ya ukweli na hayana nia njema, maana yanaweza kujenga chuki na mazingira ya kuzua mgogoro mwingine na Serikali usio na sababu wala maslahi kwa walimu wenyewe na Taifa.
·        Serikali haijakataa majadiliano na CWT, na wala haijapuuza amri ya Mahakama inayotaka pande zote mbili kurudi kwenye meza ya majadiliano. Tangu amri ya Mahakama itolewe tayari vimefanyika vikao vinne vya Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Walimu. Vikao viwili vilifanyika mwaka jana tarehe 12 Septemba, 2012 na 05 Desemba, 2012. Vikao viwili tayari vimefanyika mwaka huu tarehe 09-10 Januari na 22 Machi, 2013.
·        Kilichochelewesha suala la mishahara na posho kujadiliwa katika vikao hivyo si kwamba Serikali haikutaka mjadala huo. Sababu hasa ni kuwa CWT kilikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, katika kesi Na. 96/2012, na Serikali iliwasihi sana viongozi wa CWT kuwa wafute rufaa hiyo ili kuruhusu majadiliano ya mishahara na posho, lakini walikataa. Kitendo hicho hakionyeshi nia njema upande wao. Nia njema (good faith) ni sharti muhimu kwenye majadiliano haya. Kwa upande wake, ili kuonyesha utayari na nia njema, Serikali sasa imekubali majadiliano hayo yaendelee licha ya CWT kukataa kufuta rufaa yao.
·        Sababu ya pili iliyochelewesha majadiliano ya maslahi ya walimu ni madai ambayo awali viongozi wa CWT walikuja nayo kuwa iteuliwe timu maalum ya kuzungumzia maslahi badala ya Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Walimu ambalo ndilo lipo kisheria kwa majadiliano haya. Ni kwenye kikao cha tarehe 09 – 10 Januari, 2013 ndipo walipokubali kurejesha majadiliano kwenye Baraza hilo.
·        Si kweli vilevile kuwa kikao kilichofanyika Ikulu, tarehe 2 Aprili, 2012 chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, ndicho kilikataa majadiliano kuhusu maslahi ya walimu. Kauli hiyo ni upotoshaji  wa makusudi usio na nia njema. Viongozi wa CWT wanajua vema kuwa Katibu Mkuu Kiongozi si sehemu ya mfumo wa majadiliano kuhusu maslahi ya walimu. Hivyo, kikao kinachoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi hakiwezi kuwa mahali pa majadiliano ya mishahara, posho na maslahi ya walimu.
·        Pili, mkutano huo wa tarehe 02 Aprili, 2013 uliitishwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa maombi rasmi ya uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) ambao walitaka kujulishwa jinsi utaratibu wa majadiliano ya mishahara ya wafanyakazi wote utakavyokuwa kufuatia kuanzishwa kwa mzunguko mpya wa bajeti ya Serikali. Kikao hicho kisingeweza kugeuka na kuwa kikao cha kujadili mishahara na posho za walimu.
·        Tunapenda wananchi na walimu wajue pia kuwa Bwana Gratian Mukoba hakuwepo kwenye hicho kikao cha tarehe 02 Aprili, 2013. Aidha, kikao hicho kilikuwa cha TUCTA, hakikuwa cha CWT.
Serikali inapata taabu kuelewa nia na dhamira ya viongozi wa CWT kupotosha kwa makusudi wananchi na walimu kwa mambo yaliyo wazi. Serikali imeonyesha nia na dhamira ya wazi ya kujadiliana na CWT, pamoja na vyama vyote vya wafanyakazi, kuhusu maslahi ya wafanyakazi. Vikao vingi vilivyofanyika na vinavyoendelea kufanyika kwenye Mabaraza ya kisekta na Baraza Kuu ni ishara ya wazi ya nia njema ya Serikali. Aidha, Serikali imekwisha kusema kutakuwepo na nyongeza nzuri kwenye mishahara, hasa mishahara ya watumishi wa ngazi za chini katika mwaka ujao wa fedha. Tunajiuliza, katika hali hiyo, juhudi hizi za viongozi wa CWT kuandaa mazingira ya mgogoro wa Serikali lengo lake ni nini hasa?
             
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
 19 Aprili, 2013

No comments:

Post a Comment