Wazee kama hawa wanahitaji kusaidiwa |
Na Suleiman Msuya
KATIKA kuhakikisha kuwa usawa unakuwepo katika jamii
yote kwa pamoja Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ipo kwenye mapitio ya mfumo
wa sheria ya huduma ya jamii kwa wazee (elderly social care).
Hayo yalisemwa na Afisa Habari wa tume hiyo Munir
Shemweta wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii leo jijini Dar es
Salaam.
Alisema mapitio hayo yana lengo la kubaini mapungufu
yaliyoko kwenye mfumo huo na kutoa mapendekezo stahiki ili kuweza kuwa na mfumo
mzuri wa sheria utakaolenga ustawi na
hifadhi kwa wazee wote wenye miaka zaidi ya 60 wa mjini na vijini.
Shemweta alisema utafiti unaonyesha kuwa wazee
wakishafikisha miaka 60 na kuendelea uwezo wao wa kufanya kazi unakuwa mdogo
hali ambayo inawafanya wakose mahitaji muhimu kama chakula, mavazi,malazi
pamoja na kupungua nguvu kazi kwa Taifa.
“Tume ipo katika mchakato wa kufanyia mapitio ya
mfumo wa sheria ya huduma ya jamii kwa wazee kwani kuna dalili za kufanya wazee
wawe katika maisha magumu,” alisema.
Afisa Habari huyo alisema pamoja na kuwa na sera ya
Taifa ya Wazee (National Ageing Policy 2003) Tanzania haina sheria maalumu
katika eneo hilo, hali ambayo inachangia mgawanyiko baina ya kundi hilo.
Alisema sheria mbalimbali za mafao zinawagusa wazee
wanaostaafu kazi Serikalini na sekta binafsi ambao ni sehemu ndogo ya kundi la
wazee wengi wanaokosa huduma muhimu za maisha.
“Ikumbukwe kuwa wazee hawa ni wale waliotumikia
Taifa kwa nguvu na moyo wote kwenye ngazi mbalimbali wakati wakiwa na nguvu zao
hivyo wanapokuwa wamezeeka ni muhimu wakawekewa mfumo bora wa kisheria ili
kuhakikisha wanaishi maisha mazuri bila kujali kupungua kwa uwezo wao wa
kujishughulisha katika kazi,” alisema.
Shemweta alisema Tume inaendelea na rasimu ya awali
ya kuangalia hali halisi ya Tanzania kuhusiana na suala zima la wazee ikiwemo
mikataba ya kimataifa, mifumo ya kisheria na jamii pamoja na sera.
Alisema matarajio ya Tume ya Kurekebisha Sheria
Tanzania ni kuwa baada ya kukamilika kwa
mapito ya mfumo huo wa kisheria kuhusiana na huduma za jamii kwa wazee, Tume
itakuja na mapendekezo ya kisheria na yasiyo ya kisheria ambayo yataleta tija
kwa Taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment