Na Boniface Wambura
TIMU ya soka ya Tanzania
(Taifa Stars) imeshindwa kufuzu Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa
Ndani (CHAN) kwa mara ya pili mfululizo baada ya leo (Julai 27 mwaka
huu) kufungwa mabao 3-1 na Uganda Cranes, hivyo kutolewa kwa jumla ya
mabao 4-1.
Stars
ambayo ilicheza fainali za kwanza zilizofanyika Ivory Coast mwaka 2009
ilimaliza kipindi cha kwanza katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa
Taifa wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Kampala ikiwa sare ya bao
1-1.
Wenyeji
ndiyo walioanza kufunga bao dakika ya saba katika mechi hiyo
iliyochezeshwa na Kanoso Abdoul Ohabee kutoka Madagascar. Frank Kalanda
alifunga bao hilo akimalizia mpira uliopigwa ndani ya eneo la hatari la
Tanzania.
Bao
hilo halikuonekana kuichangaza Taifa Stars, kwani ilitulia na
kufanikiwa kusawazisha dakika ya 18 mfungaji akiwa Amri Kiemba kutokana
na pasi nzuri ya Mrisho Ngasa kwenye kona ya eneo la mita 18.
Dakika
ya 32 nusura Taifa Stars ipate bao, lakini mkwaju maridadi wa Mrisho
Ngasa ambao tayari ulikuwa umempira kipa HAmza Muwonge uligonga mwamba
kabla ya kuokolewa na mabeki wa Uganda Cranes.
Mabao
mengine ya Uganda Cranes yalifungwa dakika ya 48 kupitia kwa Brian
Majwega na lingine dakika ya 63 mfungaji akiwa tenda Kalanda kutokana na
makosa ya Salum Abubakar kupokonywa mpira wakati akiwa katika nafasi
nzuri ya kutoa pasi kwa mwenzake.
Kocha
Kim Poulsen alifanya mabadiliko dakika ya 43 kwa kumuingiza Simon Msuva
badala ya Frank Domayo aliyeumia, na dakika ya 78 akawaingiza kwa mpigo
Haruni Chanongo na Vincent Barnabas badala ya David Luhende na John
Bocco. Hata hivyo mabadiliko hayo hayakubadili matokeo ya mchezo.
Kikosi
cha Stars kilipangwa hivi; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David
Luhende/Vincent Barnabas, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Athuman Idd,
Frank Domayo/Simon Msuva, Salum Abubakar, John Bocco/Haruni Chanongo,
Amri Kiemba na Mrisho Ngasa.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itarejea nyumbani kesho
(Julai 28 mwaka huu) saa 4 usiku kwa ndege ya PrecisionAir.
No comments:
Post a Comment