STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, July 27, 2013

Javu achekelea kutua Jangwani

Husseni Javu

MSHAMBULIAJI mpya wa klabu ya Yanga, Hussein Javu amesema amefurahi mno kusajiliwa na mabingwa hao wa kandanda nchini kutokana na kiu yake ya muda mrefu ya kuchezea timu kubwa.
Anasema hakuwa na furaha kutokana na ukimya uliokuwa ukiendelea tangu alipofuatwa na viongozi wa Yanga kumshawishi kutua Jangwani na kitendo cha kumsainisha mkataba wa miaka miwili kimempa furaha.
Javu, alimaliza na Yanga juzi kwa kusaini mkataba huo baada ya kuvunjwa kwa mkataba wake wa mwaka mmoja uliokuwa umesalia ndani ya klabu yake ya zamani, Mtibwa Sugar.
"Nimefurahi baada ya kuona ndoto na maombi yangu yakitimia ya kutua katika moja ya klabu kubwa nchini," alisema.
Javu alisema kwa mchezaji yeyote mwenye kiu ya maendeleo ndoto zake ni kucheza timu kubwa za nchi soka la kulipwa na kwake anaamini kutimiza lengo moja ni sababu ya kufunguka kwa nafasi ya kwenda nje ya nchi kusakata kandanda la kulipwa.
Mshambuliaji huyo aliyeitungua kwa misimu mitatu Yanga katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwamo ushindi wa mabao 3-0 iliyopata Mtibwa dhidi ya Yanga katika mechi ya duru la kwanza kwa kufunga mabao mawili, anasema anaamini kiwango chake kitazidi kukua kwa kutua kwake Jangwani ambako tayari ameshaanza mazoezi tangu juzi asubuhi.
"Kwa muda mchache wa kuanza mazoezi nimeona mazingira niliyopo yatasaidia kuinua kiwango changu kutoka mahali kilipo, japo bado nahitaji muda kuzoeana na wachezaji wenzangu wa Yanga, ili kuweza kuitumikia vyema klabu yangu mpya, " alisema.
Kusajili kwa Javu Jangwani kunafanya atimize idadi ya washambuliaji sita ndani ya kikosi hicho wengine wakiwa ni Didier Kavumbagu, Jerson Tegete, Said Bahanuzi, Shaban Kondo (aliyesajiliwa toka Msumbiji) na Realintus Lusajo (kutoka Machava- Moshi).

No comments:

Post a Comment