Meneja
Matukio wa Capital Plus, Mathew Kasonta (kulia) akifafanua jambo wakati
wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Katikati
ni Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mmbando na Ofisa Uhusiano CP, Geofrey Nangai.
Meneja
Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson Mmbando akionesha fomu za
kujisajili kushiriki mbio hizo. Kulia ni Meneja Matukio wa Capital
Plus, Mathew Kasonta na Ofisa Uhusiano CP, Geofrey Nangai.
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Airtel ya Tanzania kupitia huduma yake ya Airtel Money kwa mara ya tano mfululizo imetangaza kudhamini mbio za Rock City Marathon za mwaka huu zilizopangwa kufanyika mkoani Mwanza tarehe 27, Oktoba 2013 ikiwa na lengo la kukuza maendeleo ya mchezo wa riadha nchini.
Airtel
imekuwa mdhamini mkuu kwa upande wa mawasiliano katika mbiyo hizo,
wakishirikiana na wadhaminiwa wengine kama NSSF, Africa Barrick Gold
(ABG), Precision Air, Bank M, PPF, Nyanza Bottling Ltd, New Mwanza
Hotel, Sahara Communications pamoja na Umoja Switch, ili kutoa fursa ya
kuinua mchezo wa riadha inchini.
Akizungumza
wakati wa tukio fupi lililofanyika katika makao makuu ya Airtel jijini
Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Bw. Jackson
Mmbando alisema kampuni yake imejidhatiti kusaidia shughuli mbali mbali
za maendeleo ya jamii na mbio za Rock City Marathon pia ni fursa pekee
ya kukuza vipaji katika michezo huo kwa ujumla.
“Kampuni
ya Airtel Tanzania kwa mwaka wa tano mfululizo, leo hii tunatangaza
udhamini wa mbio za Rock City Marathon za mwaka huu ikiwa ni sehemu ya
jitihada zetu za kusaidia maendeleo ya michezo nchi nzima.
“Tunaamini
kuwa mchango wetu utasaidia katika kuvumbua vipaji vipya
vitakavyoshiriki si tu kwa mashindano ya kitaifa lakini pia na ya
kimataifa,” alisema.
Mmbando
aliongeza kuwa washiriki kwa mwaka huu wataweza kusajili moja kwa moja
kupitia huduma ya kampuni yake ya Airtel Money kwa kutuma malipo yao kwa
neno MARATHON na kuhifadhi ujumbe kwa ajili ya kuuonyesha wakati wa
kuchukua fomu katika vituo mbali mbali.
Kwa
upande wake mratibu wa mbio za Rock City Marathon 2013, Bw. Mathew
Kasonta wakati wa tukio alisema kuwa mbio za mwaka huu zitakuwa kubwa na
bora zaidi kwa kuleta pamoja washiriki kutoka ndani ya nje ya nchi.
“Kwa
mwaka huu tumeungana na kampuni ya Airtel lakini kupitia Airtel Money
ili kutanua wigo wa ushiriki zaidi. Katika miaka iliyopita, watu wengi
wamekuwa wakikosa nafasi ya kushiriki au wakilazimika kusafiri umbali
mkubwa kwenda kwenye vituo vichache tulivyoviandaa ili waweze kununua
fomu za usajili, kwa kupitia Airtel Money zoezi hili litakuwa
limerahisishwa kwa kiasi kikubwa,” alisema Kasonta.
Kasonta
aliongeza, “ukishamaliza zoezi hilo, utapokea ujumbe utakaouonyesha
pale utakapokwenda kuchukua fomu za usajili katika ofisi za makao makuu
ya Airtel jijini Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mbeya, Arusha na
Mwanza.”
Alisema
kuwa washiriki wenye vigezo pia wataweza kusajili kwa kupata fomu
zipatikanazo katika uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza, na katika ofisi
za kampuni ya Capital Plus International zilizopo ghorofa ya tatu,
upande wa kulia katika jengo la ATC, Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam.
Kasonta
alibainisha kuwa fomu za usajili zitapatikana katika viwango vya bei
vifuatavyo; shilingi 5,000 kwa mbio za km 21 (kwa watu wote), shilingi
3,000 kwa mbio za km 5 (mbio kwa makampuni na taasisi).
Alisema
kuwa fomu kwa mbio za kilometa 3 (kwa wazee kuanzia miaka 55 na watu
wenye ulemavu wa ngozi) na mbio za kilometa 2 kwa watoto (wenye umri wa
miaka 7 mpaka 10) zitapatikana bure.
No comments:
Post a Comment