STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, September 26, 2013

Mtibwa Sugar wapo tayari kwa vita sasa

Mecky Mexime
KOCHA Mkuu wa timu ya Mtibwa Sugar, Mecky Mexime amesema makosa yaliyoiponza timu yake kushindwa kupata ushindi katika mechi zao tatu mfululizo wameyafanyia kazi tayari kwa vita vya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Aidha kocha huyo alisema pamoja na Ashanti United kuonekana kama timu dhaifu katika ligi hiyo watashuka dimbani katika mechi baina yao siku ya Jumapili kwa tahadhari kubwa na bila kuidharau ilimradi kuhakikisha wanapata ushindi.
Akizungumza na MICHARAZO, Mexime, nahodha wa zamani wa timu hiyo ya Mtibwa na Taifa Stars, alisema benchi lao la ufundi tayari limeshagundua wapio walipokuwa wamekosea katika mechi zao zilizopita na kujipanga upya kuianza ligi.
Mexime, alisema kipigo cha mabao 2-0 toka kwa Simba na sare mbili dhidi ya timu za Mbeya City na Prisons za Mbeya vimewafanya wajipange upya kwa kurekebisha makosa yao na sasa wapo tayari kwa vita katika ligi hiyo.
"Tumejipanga upya kwa kuangalia wapi tulipokuwa tunakosea na kurekebisha na sasa tupo tayari kwa vita, hatutakubali kuona tukipoteza tena pointi japo hatuwezi kuidharau Ashanti United tutakaovaana nao Jumapili hii jijini Dar," alisema.
Kocha huyo alisema wataenda uwanja wa Chamazi kwa tahadhari kubwa dhidi ya Ashanti Utd bila kuidharau kwani wanaamini ni timu ngumu na inayoweza kufanya lolote iwapo watawapuuza katika pambano hilo.
Kuhusu kikosi chake, Mexime alisema kinaendelea vyema na hakuna mchezaji yeyote majeruhi kitu kinachompa faraja kwamba watapata pointi tatu muhimu kwa ajili ya kuwatoa nafasi ya tisa waliopo na kurejea nafasi za juu walizokuwa awali.
Mtibwa Sugar katika mechi zake tano ilizocheza mpaka sasa imeshinda mechi moja tu na kupoteza moja huku tatu ikipata sare na kukusanya pointi 6 sawa na Yanga walioopo juu yao wanaotofautiana nao kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

No comments:

Post a Comment