STRIKA
USILIKOSE
Thursday, September 26, 2013
TPBF yalia ngumi kudhalilishwa
Na Suleiman Msuya
SHIRIKISHO la Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBF) limesema linasikitishwa na watu ambao wanadhalilisha mchezo wa ngumi hapa nchini kwa maslahi yao binafsi.
Kauli hiyo ya masikitiko imetolewa na Rais wa TPBF Chatta Michael wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam.
Rais huyo alisema baada ya pambano la bondia Francis Cheka kupigana mwezi mmoja uliopita yameibuka makundi ya watu ambao wanaonekana kuwa na mikakati yao binafsi jambo ambalo halipaswi kunyamaziwa kwani linaweza kuleta picha mbaya kwa nchi.
Alisema kitendo cha Cheka kuibuka bingwa katika mpambano huo wa dunia ingetakiwa iwe ni sehemu ya nchi kuungana ili kuhakikisha kuwa fursa hiyo haiondoki kirahisi na iwe ni moja kufungua njia ya ujio wa mabondi wengine.
Michael alisema baada ya mpambano huo hadi sasa wamejitokeza mabondia kutoka nchi za Mexico na Australia kuhitaji kupambana na Cheka kutokana na kuridhishwa na kiwango chake.
“Napenda kutumia fursa hii kuzungumza na jamii ya kitanzania ambayo inafuatilia mchezo huu wa ngumi kuwa ni vema kuachana na maneno ya baadhi ya watu ambao wapo kwa nia ya kupotosha hali ambayo inaweza kuathiri dhima nzima za wadau wenye nia ya kukuza mchezo huo,” alisema.
Rais huyo alisema mikakati ambayo ipo ni kuhakikisha kupitia shirikisho la Ngumi la Dunia (WBF) Tanzania inapata mapambano mengi makubwa ya kimataifa ili kuweza kukuza vipaji vya vijana ambao wapo tayari.
Alisema TPBF imejipanga vilivyo ili kuweza kushirikiana na WBF ili kuhakikisha kuwa mchezo wa ngumi Tanzania unapiga hatua kwani ni moja ya mchezo ambao unatoa fursa za mafanikio kwa haraka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment