Shafii Dauda mmoja ya waliotoswa jumla ya TFF |
KAMATI
ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetangaza
hukumu ya mashauri nane yaliyowasilishwa mbele yake kwa kumsafisha
mlalamikiwa mmoja, kutowaadhibu zaidi washtakiwa sita na kuahirisha
kusikiliza shauri moja baada ya mlalamikiwa kutokuwepo.
Riziki
Juma Majala, ambaye ni Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani
(COREFA) ndiye pekee aliyesafishwa na Kamati ya Maadili dhidi ya
mashtaka ya kutoa kauli zilizosababisha kufunguliwa kwa kesi dhidi ya
TFF.
Vilevile
Kamati imesita kuwachukulia hatua Shafii Dauda, Nazarius Kilungeja,
Wilfred Kidao, Omar Isaak Abdulkadir na Kamwanga Tambwe kutokana na
kuridhika kuwa wameshaadhibiwa kwa kuenguliwa kwenye uchaguzi, hivyo
hawawezi kuadhibiwa mara mbili.
Pia
imesema haiwezi kumuadhibu Richard Julius Rukambura, aliyeshtakiwa kwa
kukiuka Katiba ya TFF kwa kosa la kufungua kesi mahakamani, baada ya
kubaini kuwa si mwanafamilia wa TFF kutokana na kuenguliwa kwenye
uchaguzi.
Hoja
hiyo pia ilitumika kutomchukulia hatua Dauda na mwamuzi wa zamani Omar
Abdulkadir kwa hoja kuwa walipoteza sifa za kuwa wanafamilia wa TFF
baada ya kuenguliwa kwenye uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi.
Shauri
la Omary Mussa Mkwaruro la tuhuma za kutumia cheti cha elimu
kisichotambuliwa na mamlaka husika, limeahirishwa kutokana na
Mlalamikiwa kutowasilisha utetezi wake, hivyo Kamati imeagiza
Sekretarieti kuwasiliana naye ili awasilishe maelezo yake.
Watu
hao walifikishwa mbele ya Kamati ya Maadili baada ya kujitokeza kuwania
nafasi mbalimbali za uongozi wa TFF na baada ya usaili walibainika kuwa
na matatizo ya kimaadili, hivyo ili iamue juu ya hadhi yao katika
familia ya mpira wa miguu kwa kuwachukulia hatua au kuwaweka huru.
Katika
hukumu iliyotolewa leo (Septemba 26 mwaka huu), Kamati ya Maadili
imeeleza kuwa Majala hakiuka Kanuni za Maadili kwa kuwa vielelezo
vilivyowasilishwa na TFF vinaonyesha kuwa klabu ya Kiluvya United
imesajiliwa na Serikali na vyama wanachama wa TFF.
Kuhusu
Rukambura, ambaye alilalamikiwa kwa kuipeleka TFF kwenye mahakama ya
kiraia, hivyo kukiuka Kanuni ya 73 (3) (b) ya Kanuni za Maadili, Kamati
imesema ushahidi uliowasilishwa na TFF hauonyeshi kama mgombea ni
mwanafamilia wa TFF; alishaondolewa katika uchaguzi na hivyo si kati ya
wagombea na hivyo mikono ya Kamati kufungwa kwa mujibu wa kanuni ya pili
ya Kanuni za Maadili.
Kamati
pia imeeleza kuwa Kanuni ya 73 (3) ambayo ingepaswa kutumika
kumchukulia hatua, chimbuko lake ni Ibara ya 75 ya Katiba ya TFF ambayo
inawalenga wanachama tu na hivyo kuamua kuwa malalamiko hayo hayana
mashiko na kwani Rukambura alishapoteza sifa za kuwa mwanafamilia na
hivyo kushindwa kumchukulia hatua.
Kidao
alishtakiwa kwa kosa la kumiliki nyaraka za Kamati ya Utendaji kinyume
na taratibu na pia kuwasilisha malalamiko yake Shirikisho la Kimataifa
la Mpira wa Miguu (FIFA) bila ya kufuata taratibu, lakini Kamati imesema
kwa vile mlalamikiwa ameenguliwa kwenye uchaguzi, anatumikia adhabu ya
kinidhamu na hivyo haiwezi kumuadhibu mara mbili.
Kuhusu
Shafii Dauda, Kamati imesema malalamiko dhidi yake hayana mashiko kwa
kuwa si mwanafamilia wa TFF na kwamba lalamiko dhidi yake linatupiliwa
mbali kwa kuwa tayari ameshaondolewa kwenye uchaguzi kutokana na kosa la
kinidhamu.
Kamati
iliona hakukuwa na haja ya kushughulikia mashauri dhidi ya Nazarius
Kilungeja, ambaye alishtakiwa kwa kukaidi maagizo ya vyombo halali vya
TFF, na Kamwanga Tambwe kwa kuwa tayari wawili hao wanatumikia adhabu ya
kufungiwa na Kamati ya Nidhamu.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment