ATHENS, Ugiriki
KIVUMBI cha Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champion League) kinatarajiwa kuendelea tena leo na kesho kwa mechi nne za kumalizia mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora kuwania kucheza Robo Fainali ya michuano hiyo.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester United ambayo imefufuka kwenye ligi ya nyumbani leo itakuwa ugenini nchini Ugiriki kuvaana na Olympiakos Piraeus wiuki moja baada ya timu za Manchester City na Arsenal kupoteza mechi zao za nyumbani dhidi ya Barcelona na Bayern Munich.
Mechi nyingine ya leo itazikutanisha timu za Zenit St Petersburg dhidi ya wana fainali wa mwaka jana, Dortmund ya Ujerumani.
Katika mechi ya Manchester United dhidi ya Olympiakos Piraeus, wagiriki hao hawajawahi kufanya vyema mbele ya Mashetani Wekundu, japo wenyewe wamenukuliwa wakiapa kwamba piga ua leo ni lazima waigaragaze vijana wa David Moyes.
Mashetani Wekundu waliopata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Crysral Palace kwenye mechi yao ya ligi mwishoni mwa wiki, itahitaji kufanya vyema leo ugenini ili kufufua matumaini ya timu za England kuvuka katika hatua hiyo.
Hata hivyo itakuwa na kazi ngumu kuhakikisha wanaifunga vinara hao wa Ligi Kuu ya Ugiriki ambao wamefika hatua hiyo ya mtoano kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka minne.
Wagiriki hao wataweka historia kama wataifunga United baada ya kupoteza mara nne katika michuano ya hivi karibuni ilipokutana nayo.
Hata hivyo, kwa sasa Olympiakos Piraeus ipo katika kiwango kizuri baada ya kucheza mechi 26 za ligi bila kupoteza huku ikiongoza kileleni mwa Ligi Kuu ya Ugiriki maarufu kama Super League.
Wakati United Jumamosi ikishinda 2-0 dhidi ya Crystal Palace, Olympiakos iliichapa OFI Crete mabao 4-0 huku Mserbia Marko Scepovic aliyesajiliwa hivi karibuni akifunga mara tatu ‘hat-trick’ yake ya kwanza katika maisha yake kisoka.
"Ningependa kuona hali kama hii, na hamu ya wachezaji wangu dhidi ya United kama walivyoonyesha dhidi ya OFI," kocha Michel alisema wakati timu yake ikipata ushindi wa 24 katika mechi 26 za ligi ilizocheza.
"Kila mechi tunakabiliana nayo kwa umakini sana na tunaamini tutapata matokeo mazuri sana Jumanne (leo)," alisema mshambuliaji huyo wa zamani na wa Real Madrid na Hispania ambaye kwa sasa ana miaka 50.
"Tumegeuza ukurasa mpya na akili zetu sasa tunazielekeza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya United, ninaweza kuona hamu ndani ya macho na katika sura ya wachezaji wangu; wako tayari kwa hilo," aliahidi katika ukurasa wake wa Facebook juzi.
Michel atawakosa baadhi ya wachezaji wake wakongwe baada ya mshambuliaji wa zamani wa Argentina Javier Saviola kuwa majeruhi wa mguu. Kukosekana kwa Saviola inamaana Mnigeria Michael Olaitan mwenye miaka 21 kwa sasa, ambaye amefunga mabao nane katika mechi 15 alizocheza, atapata nafasi ya kuanza sambamba na kiungo mshambuliaji wa Argentina Alejandro Dominguez atakayecheza nyuma yake.
United imesafiri kwenga Ugiriki hiyo ikiwa nafasi pekee kwao msimu huu ya kutwaa kombe lakini hata hivyo matarajio hayo ni madogo sana kwa ubora wao kwa sasa.
Katika mechi hiyo, United itakuwa ikimtegemea zaidi Wayne Rooney (pichani) aliyepewa mkataba mnono wa paundi 300,000 kwa wiki huku akifunga bao safi mwishoni mwa wiki.
Pia, kocha David Moyes atakuwa na uwanja mpana zaidi wa kumjumuisha Marouane Fellaini katika kikosi chake cha kwanza baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Juu ya pambano la Zenit dhidi ya Dotmund, mashabiki wa timu ya Ujerumani watapewa ofa ya chai na vitafunwa kwa Zenit St Petersburg leo, lakini ukarimu huo hautakuwapo dimbani kwani miamba hiyo ya Urusi imepania kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza.
Kocha wa Zenit, Luciano Spalletti anafurahia kiwango cha timu yake kwa sasa; "Tumecheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa muda mrefu sasa, na tumepigana vema msimu huu. Tumekuwa na wachezaji wengi bora jambo linalomaanisha tunaweza kucheza kwa kiwango hiki."
Aliongeza: "Tulitoka sare nyumbani na Porto tulipopaswa kushinda, na ilikuwa hali kama hiyo dhidi ya Austria Vienna, tulipocheza tukiwa 10 uwanjani zaidi ya sasa moja.
"Tulipaswa kunyakua pointi nyingi zaidi, lakini kwa ujumla tunaweza kuwa na furaha kwa kiwango chetu."
Dortmund ilisonga mbele baada ya kuwa kinara wa kundi lao lilokuwa likizijumuisha Napoli, Arsenal na Olympique Marseille kwa kufikisha pointi 12 sawa na vijana wa Arsene Wenger na wa Rafa Benitez lakini wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa ndiyo yaliyoibeba miamba hiyo ya Ujerumani ambayo msimu huu haitisha kwenye ligi ya nyumbani.
Baada ya kutwaa ubingwa wa Bundesliga 2011 na 2012 na kumaliza ya pili msimu uliopita, imekuwa ikipanda na kushuka msimu huu na kwa sasa inashika nafasi ya tatu.
Jumamosi ilipata kipigo kikubwa zaidi ugenini msimu huu baada ya kuchapwa 3-0 na Hamburg SV lakini kocha Juergen Klopp anaamini watafanya vizuri leo.
"Tumewahi kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufanya vibaya kwenye ligi ya nyumbani," alisema.
"Ni mashindano tofauti kabisa," aliongeza kiungo Nuri Sahin. "Tutajiandaa vema huko St Petersburg na tunahitaji kupata matokeo mazuri na kurudi nayo Dortmund."