Chelsea inayomkuna Wenger |
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger |
KASI ya klabu ya Chelsea imemfanya, kocha wa Arsenal, Arsene Wenger kukiri kwamba hakuna klabu yoyote kwa sasa inayoweza kuisimamisha wakali hao wa Darajani.
Wenger amenukuliwa akisema kuwa hakuna timu inayoweza kuwapata vinara wa Ligi Kuu Chelsea msimu huu kwa jinsi ilivyo katika kiwango cha kuvutia zaidi.
Arsenal walichapwa mabao 2-1 ugenini na Swansea City juzi na kuteleza nyuma zaidi ya Chelsea ambao hawajafungwa msimu huu kwa tofauti alama 12.
Chelsea wameshinda michezo yao tisa kati ya 11 msimu huu na kujikusanyia alama 29, nne zaidi ya Southampton wanaoshika nafasi ya pili katika msimamo huo, ambao wamekuwa na mafanikio makubwa tofauti na ilivyotarajiwa na wengi baada ya kumpoteza kocha na wachezaji karibu 10 nyota waliosajiliwa timu mbalimbali za Ligi Kuu ya England.
Katika mahojiano, Wenger amesema kama Chelsea wakiendelea na makali yao hayo hadhani kama kuna timu ya kuwashika msimu huu kwani inaonekana hakuna timu inayoweza kupambana nao kwa sasa.
Chelsea walipambana na kuhakikisha wanatoka nyuma na kuifunga Liverpool mabao 2-1 katika Uwanja wa Anfield Juzi na Wenger anaamini kikosi chao kimejitengenezea hali ya kujiamini.
Hata hivyo kocha huyo aliwahi kunukuliwa wiki chache zilizopita akisema ni ngumu kwa Chelsea kuweza kufikia rekodi yao ya msimu wa 2003-2004 waliocheza mechi 49 bila kupoteza kwa madai ni mapema mno.
No comments:
Post a Comment